Waziri Mkuu Mstaafu Edward
Lowassa akiwasili Ikulu jijini Dar es Salaam leo. PICHA ZOTE NA IKULU
|
Rais John Pombe Magufuli akiwa katika mazungumzo na Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa mara baada ya kuwasili Ikulu jijini Dar es Salaam. |
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 09 Januari, 2018 amekutana na
kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Edward Ngoyai Lowassa, Ikulu
Jijini Dar es Salaam.
Baada ya mazungumzo hayo Mhe.
Edward Ngoyai Lowassa amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya
na ametaja baadhi ya maeneo ambayo kazi kubwa imefanyika kuwa ni kutoa elimu
bila malipo, ujenzi wa mradi wa uzalishaji wa umeme katika maporomoko ya mto
Rufiji (Stiegler’s Gorge), ujenzi wa viwanda na ujenzi wa reli kwa
kiwango cha kisasa (Standard Gauge) ambavyo vinazalisha ajira nyingi kwa
Watanzania.
“Nimepata
faraja sana kuja hapa Ikulu kuonana na Mhe. Rais, tumezungumza nae na
nimempongeza kwa kazi nzuri anayoifanya, lazima tukiri anafanya kazi nzuri na
anahitaji kutiwa moyo.
“Moja kubwa
ambalo ni la msingi sana ni la kujenga ajira, katika kuanza ujenzi wa reli ya
kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro hapo anajenga ajira, na kwenye nchi yoyote
inayoendelea suala muhimu ni kujenga ajira, Stiegler;s Gorge ni kujenga ajira
na mingine ya aina hiyo, lazima kuwepo na kipaumbele cha kusema kwamba
tunajenga ajira, jingine ni la elimu, ni muhimu sana, hauwezi kuacha elimu
katika mambo yako unayofanya, hili nalo lazima lisemwe vya kutosha, kwa kweli
nakushukuru Mhe. Rais, you made my day” amesema Mhe. Lowassa.
Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli
amempongeza Mhe. Edward Ngoyai Lowassa kwa kutambua kazi kubwa inayofanywa na
Serikali na amesema Mhe. Lowassa ni mmoja wa viongozi ambaye kwa wakati wake
ametoa mchango wake katika nchi.
Mhe. Rais Magufuli ameongeza kuwa
Mhe. Lowassa ni mwanasiasa mzuri kwani hata wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu
uliopita ambao naye aligombea kiti cha Urais, hakuwahi kumtukana.
“Mhe. Lowassa
ameniomba mara nyingi nikutane nae, na leo nimekutana nae, tumezungumza mambo
mengi, ameniambia ya kwake na mimi nimemwambia ya kwangu, kwa ujumla Mhe. Lowassa
ni mwanasiasa mzuri na tuendelee kuwaenzi wazee hawa ambao kwa nyakati fulani
walifanya mambo mazuri, na mimi napenda kumpongeza Mhe. Lowassa ambaye kama
alivyosema hapa kuwa tumefanya mambo mazuri mengi.
“Ametaja
miradi mbalimbali tunayotekeleza, ametaja mradi wa Stiegler’s Gorge
utakaogharimu zaidi ya Shilingi Trilioni 7, amezungumzia juu ya elimu bure,
amezungumzia juu ya maji ambayo kwa bahati nzuri yeye alikuwa Waziri wa Maji na
anafahamu sasa tumefikia wapi, amezungumza juu ya umeme tulivyosambaza katika
vijiji mbalimbali, elimu bure, huduma za hospitali na mengine” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
IKULU
Dar es Salaam
09 Januari, 2018
Rais John Pombe Magufuli akiwa katika mazungumzo na Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa mara baada ya kuwasili Ikulu jijini Dar es Salaam. |
No comments:
Post a Comment