Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Khalfan Haule |
Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Khalfan Haule amethibitisha
kufariki kwa wagonjwa saba wa kipindupindu katika Wilaya ya Sumbawanga huku
wagonjwa wengine 44 wakibaki wodini kuendelea kupatiwa matibabu na wagonjwa 115
wakiruhusiwa kurudi nyumbani.
Amesema kuwa ugonjwa huo umelipuka tarehe 6 Mei, 2018 katika
Kijiji cha Mayenje, kata ya Milepa katika bonde la ziwa Rukwa na kusambaa
katika meneo mengine ya Wilaya na hatimae kupatikana kwa wagonjwa wawili katika
hospitali ya rufaa ya mkoa.
“Sasa hivi katika bonde la ziwa Rukwa kuna shughuli za uvunaji
wa mpunga na hivyo watu wengi hutokea huku juu kwenda bondeni kutafuta vibarua
vya kuvuna mpunga kwenye maeneo hayo yaliyoathirika na kipindupindu, maji
yanayotumika huko ni machafu kutoka katika madimbi na mito nawaomba viongozi wa
dini watoe tahadhari kwa waumini hasa katika maeneo yale yalioathirika zaidi,”
Alisema.
Alisema hayo alipopewa nafasi ya kutoa taarifa hiyo ya ugonjwa
wa kipindupindu na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo wakati wa Mkutano
uliowakutanisha wadau wa afya Mkoani hapa kwaajili ya kuzungumzia tahadhari ya
ugonjwa wa Ebola uliopo katika nchi ya jirani ya Kongo.
Kwa upande wake Mh. Wangabo alisema kuwa elimu ya tahadhari
itatolewa kwa wananchi kupitia mikutano mbalimbali ya hadhara ya wakuu wa
wilaya, madiwani pamoja na wakurugenzi ili ifikie hatua ya kusema “kipindupindu
sasa basi”.
No comments:
Post a Comment