Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kulia). |
RUKWA
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewatoa mashaka
wanarukwa juu ya kutokuwepo kwa ugonjwa wa Ebola katika Mkoa na kutahadharisha
yeyote anaejaribu kuleta hofu ya ugonjwa huo katika Mkoa na kuwataka wananchi
wasijengewe hofu bali waendelee kuchukua hatua za tahadhari za kujikinga na
ugonjwa huo.
Amesema kuwa Mkoa unaendelea kushirikiana na sekta mbalimbali
katika kuimarisha ufuatiliaji na kutekeleza mikakati ya udhibiti ikiwemo kutoa
taarifa na elimu kwa jamii kwa kadiri itakavyohitajika ili ugonjwa huo usiingie
katika mkoa.
“Katika kipindi hiki ambacho tunatakiwa kuchukua tahadhari
kubwa, wananchi wote wa Mkoa wa Rukwa ni lazima tuwe na mshikamano, umoja na
tahadhari kubwa sana na hasa maeneo yale ya Ziwa Tanganyika ambako kuna
muingiliano wa watu kutoka Zambia, DRC, Rwanda na Burundi. Lakini pia wanaotokea
maeneo mengine ya nchi, la muhimu ni kuchukua tahadhari kubwa sana,” Alisema
Ameongeza kuwa wenyeviti wa vijiji wajizatiti katika
kuboresha taarifa za wakazi wao kwenye madaftari yao na kuwa makini na wageni
wanaoingia kwenye maeneo yao pamoja na kuitaka idara ya uhamiaji kuhakikisha
wageni wote wanaingia katika njia zilizo rasmi.
Ameyasema hayo alipokuwa akifungua kikao cha wadau wa afya Mkoa
kilichoitishwa na Mganga Mkuu wa mkoa ili kutoa elimu kwa wawakilishi wa
makundi mbalimbali ya jamii ikiwemo waandishi wa habari juu kusambaza ujumbe
huo wa kujihadhari na ugonjwa huu hatari wa Ebola.
Mmoja wa wadau hao akiwakilisha kundi la wazee, Zeno Nkoswe
amesema kuwa serikali ya Mkoa haina budi kuhakikisha elimu hiyo inafikishwa kwa
viongozi wote wa dini kwani wao wanauwezo wa kuwafikia wananchi wengi zaidi na
kwa muda ufupi na ujumbe hatimae kutimiza malengo ya kufisha ujumbe huo kwa
wananchi.
Akichangia mjadala huo mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Rukwa, Sadrick Malila amesema kuwa serikali haina
budi kutumia redio zilizopo Mkoani Rukwa ili kufikisha ujumbe huo kwa watu wote
na maeneo yote ya Mkoa na mikoa ya jirani ili watu waweze kujikinga na ugonjwa
huo.
Ugonjwa wa Ebola upo katika nchi ya jirani ya Jamhuriya watu wa
Kongo katika mji wa Biroko, jimbo la Equator na kwa taarifa za shirika la afya
duniani, hadi kufikia tarehe 17 Mei, 2018 watu 44 walikuwa wamebainika kuwa na
ugonjwa huo na watu 23 kufariki.
No comments:
Post a Comment