Tangazo

June 5, 2018

KIGWANGALLA AAGIZA MSAKO MKALI KWA WALIOUA SIMBA TISA SERENGETI

 Baadhi ya simba kati ya tisa waliouwawa kikatili kwa kulishwa sumu, kukatwa na kuchomolewa baadhi ya viungo vyao na wananchi katika kijiji cha Nyichoka, wilaya ya Serengeti mkoani Mara.

Na Hamza Temba-Dodoma
............................................................
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla ameagiza Kikosi Kazi Dhidi ya Ujangili cha Taifa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya Serengeti kuwasaka watu waliohusika na mauaji ya simba tisa katika kijiji cha Nyichoka, wilaya ya Serengeti mkoani Mara na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Dkt. Kigwangalla ametoa agizo hilo ofisini kwake Jijini Dodoma jana baada ya kupokea taarifa rasmi ya mauaji hayo ya kikatili yaliyoripotiwa hivi karibuni kwa simba hao kulishwa sumu kali katika kijiji hicho huku mmoja akikatwa miguu, mkia, ngozi ya juu ya mgongo na kuchukuliwa baadhi ya viungo vyake ambapo amesema mauaji hayo hayavumiliki kwa kuwa yana athari kubwa kiikolojia, kiutalii na uchumi wa Taifa kwa ujumla.

"Bahati mbaya sana ni kuwa anapouawa simba kwa sumu hafi peke yake, inakufa familia nzima ya simba, na mara nyingi wanakufa pia wanyamapori wengine wanaodowea nyama na wanaokula mizoga. Walipouawa simba wa Ruaha hivi karibuni walikufa fisi zaidi ya 70 na ndege mbeshi zaidi ya 100, achilia mbali wadudu," amesema Dkt. Kigwangalla kwa masikitiko makubwa.

Amesema pamoja na faida kubwa za simba kwa Taifa kiuchumi, Kijiji cha Nyichoka pekee walikouwawa simba hao ni katika sehemu iliyofaidika sana na miradi ya ujirani mwema kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

"Wanyama hawa jamii ya paka wakubwa ni muhimu sana kwa kuweka mizania ya ikolojia sawa, maana wanadhibiti idadi ya wanyama wala nyasi kwa kuwala, bila hivyo hifadhi zote zinaweza kugeuka kuwa jangwa. 

"Hakuna mtalii atakayekuja hifadhini asitamani kumuangalia simba, mfalme wa pori. Wanapouawa maana yake tunashusha hadhi ya hifadhi zetu kiutalii na hivyo kutishia kupoteza mapato yanayotokana na utalii" amesisitiza Dkt. Kigwangalla. 

Amesema tukio hilo la kuuwawa kwa Simba wa Ikolojia ya Serengeti sio la kwanza kutokea hapa nchini ambapo mwishoni mwa mwaka jana simba wengine watano waliuawa pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha. 

"Mwaka huo huo mwanzoni simba watatu nao walipigwa risasi kikatili wilayani Serengeti huku mwaka 2015 simba 7 wakauwawa tena kwa sumu, huko huko Serengeti".

Akizungumzia sababu za ujangili huo amesema mara nyingi ni kwa ajili ya kulipiza kisasi baada ya ng’ombe wa wananchi kuliwa na simba, changamoto ambayo husababishwa na wananchi wenyewe kusogelea na kuweka makazi karibu kabisa na mipaka ya hifadhi za wanyamapori kwa lengo la kulisha mifugo pembezoni na wakati mwingine ndani ya hifadhi hizo kinyemela.

Simba ambao wanakadiriwa kuwa zaidi kidogo ya 22,000, pamoja na wanyama wengine jamii ya paka wamepungua sana miaka ya hivi karibuni kiasi cha kuwekewa tishio la kutoweka hapa duniani. Duma nao wanakadiriwa kubaki 1,200 pekee.
 Askari wa wanyamapori wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wakikusanya miili ya simba  tisa waliouwawa kikatili kwa kulishwa sumu, kukatwa na kuchomolewa baadhi ya viungo vyao na wananchi katika kijiji cha Nyichoka, wilaya ya Serengeti mkoani Mara  hivi karibuni kwa ajili ya kuwafanyia uchunguzi kubaini chanzo cha vifo vyao.
 Askari wa wanyamapori wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wakikusanya miili ya simba  tisa waliouwawa kikatili kwa kulishwa sumu, kukatwa na kuchomolewa baadhi ya viungo vyao na wananchi katika kijiji cha Nyichoka, wilaya ya Serengeti mkoani Mara  hivi karibuni kwa ajili ya kuwafanyia uchunguzi kubaini chanzo cha vifo vyao.

No comments: