Tangazo

Showing posts with label Utalii. Show all posts
Showing posts with label Utalii. Show all posts

June 5, 2018

WALINZI WA WANYAMAPORI WATAKIWA KUWA MAKINI NA WAADILLIFU


Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori nchini (TAWA), Meja Jenerali  mstaafu Hamisi Semfuko (wa pili kushoto mwenye miwani), akizungumza na walinzi wa wanyamapori katika maeneo yanayozunguka Pori ya Akiba la Maswa mkoani Simiyu alipokua akikagua shughuli za uhifadhi na ulinzi katika maeneo hayo juzi.
Xxxxxxxxxxxx

MARA

WALINZI wa wanyamapori katika maeneo yanayozunguka Pori ya Akiba la Maswa yanayopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wametakiwa kuwa makini na waadilifu kutokana na kuongezeka kwa wanyama adimu wanaofika maeneo yao.

Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori nchini (TAWA) Meja Jenerali  mstaafu Hamisi Semfuko alipokua akikagua shughuli za uhifadhi na ulinzi katika maeneo hayo.

Meja Jenerali Semfuko, alisema kazi ya kupambana na ujangili inahitaji uvumilivu, uadilifu na ujasiri mkubwa kutokana na mazingira hatarishi yaliyopo.

"La muhimu kuna taatifa maeneo haya wameanza kuja wanyama adimu hivyo ningependa muongeze jitihada hizi mara dufu wanyama hao wasidhurike," alisema.

Katika ziara hiyo wajumbe wa Bodi ya TAWA walipokea taarifa ya timu ya pamoja kati ya TAWA, Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), Frankfurt Zoological Society  ( FZS), TAWIRI na Friedkin Conservation Fund (FCF) katika kuhifadhi na kulinda na kuhifadhi wanyama adimu.

Taarifa hiyo iliyowasilishwa na wataalamu Philbert Ngoti wa TANAPA na Gerald Nyaffi wa FZS katika  eneo la kitalu kilichopo Maswa Mbono kinachoendeshwa na kampuni ya Tanzania Game    Tracker Safaris  (TGTS).

Wataalam hao walisema wamefanikiwa katika mradi huo kwa ufadhili wa familia ya Friedkin inayomiliki TGTS ililiyofadhili fedha, vifaa pamoja na helikopta, kazi ijayotarajiwa kuendelea katika maeneo mengine.

Katika ziara hiyo TAWA  imeridhishwa na utendaji wa Makampuni ya uwindaji na upigaji picha za kitalii, yaliyopo katika maeneo yake kwa kusimamia uhifadhi na ulinzi pamoja na kuchangia miradi ya maendeleo ya wananchi yenye thamani zaidi ya sh 40 bilioni.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya  Usimamizi wa Wanyamapori nchini (TAWA), Dk James Wakibara akizungumza na waandishi wa habari juu ya mchango kwa jamii, uhifadhi na kiuchumi wa  makampuni ya uwindaji wa kitalii zilizowekeza katika maeneo yao.

Maeneo yaliyotembelewa na TAWA ni pamoja  na Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori(WMA) ya Makao wilayani Meatu inayosimamiwa na kampuni ya Mwiba Holdings Limited.

Dk Wakibara alisema, licha  mchango wa makampuni kwenye jamii, pia TAWA kupitia malipo  ya kampuni hizo, imekuwa ikitoa  takriban sh 6.5 bilioni kila mwaka kwa vijiji vyenye wawekezaji hao na halmashauri.

Makampuni hayo yamewekeza katika baadhi ya maeneo ya vitalu 159   vilivyopo nchini na maeneo ya hifadhi za jamii za wanyamapori (WMA) 38 zilizopo nchini.

"Hizi kampuni za kitalii zina mchango mkubwa sana pia katika uhifadhi wa maeneo haya, hasa katika vita dhidi ya ujangili ikizingatiwa asilimia 95 ya maeneo yaliyohifadhiwa nchini yapo chini ya TAWA"alisema

Alisema kwa sasa mapato ya TAWA kutokana na shughuli za uhifadhi, yamefikia dola milioni 20 lakini kuna mikakati ya kuongeza mapato hayo mara nne zaidi hadi kufikia dola milioni 80.


"kuna dhana potofu kuwa uwindaji wa kitalii ni kumaliza wanyama hili sio kweli, kwani haya makampuni hayajawahi kufikia hata robo  kiwango cha kuwinda wanyama ambacho kinatolewa kila mwaka na TAWA na mashirika ya kimataifa"alisema

Mwenyekiti wa bodi ya TAWA, Meja Jenerali  mstaafu Hamisi Semfuko alisema mamlaka hiyo ipo katika mabadiliko  makubwa ili kuhakikisha jamii inanufaika zaidi ya uhifadhi wa wanyamapori,katika kusaidia miradi ya kijamii ya maji, afya Elimu na uhifadhi.

Mwenyekiti huyo na bodi yake ambao walitembelea pori la Makao, lilipo mpakani mwa Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro na Meatu,alisema wameridhishwa na utendaji wa kampuni ya Mwiba Holding katika eneo hilo.

KIGWANGALLA AAGIZA MSAKO MKALI KWA WALIOUA SIMBA TISA SERENGETI

 Baadhi ya simba kati ya tisa waliouwawa kikatili kwa kulishwa sumu, kukatwa na kuchomolewa baadhi ya viungo vyao na wananchi katika kijiji cha Nyichoka, wilaya ya Serengeti mkoani Mara.

Na Hamza Temba-Dodoma
............................................................
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla ameagiza Kikosi Kazi Dhidi ya Ujangili cha Taifa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya Serengeti kuwasaka watu waliohusika na mauaji ya simba tisa katika kijiji cha Nyichoka, wilaya ya Serengeti mkoani Mara na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Dkt. Kigwangalla ametoa agizo hilo ofisini kwake Jijini Dodoma jana baada ya kupokea taarifa rasmi ya mauaji hayo ya kikatili yaliyoripotiwa hivi karibuni kwa simba hao kulishwa sumu kali katika kijiji hicho huku mmoja akikatwa miguu, mkia, ngozi ya juu ya mgongo na kuchukuliwa baadhi ya viungo vyake ambapo amesema mauaji hayo hayavumiliki kwa kuwa yana athari kubwa kiikolojia, kiutalii na uchumi wa Taifa kwa ujumla.

"Bahati mbaya sana ni kuwa anapouawa simba kwa sumu hafi peke yake, inakufa familia nzima ya simba, na mara nyingi wanakufa pia wanyamapori wengine wanaodowea nyama na wanaokula mizoga. Walipouawa simba wa Ruaha hivi karibuni walikufa fisi zaidi ya 70 na ndege mbeshi zaidi ya 100, achilia mbali wadudu," amesema Dkt. Kigwangalla kwa masikitiko makubwa.

Amesema pamoja na faida kubwa za simba kwa Taifa kiuchumi, Kijiji cha Nyichoka pekee walikouwawa simba hao ni katika sehemu iliyofaidika sana na miradi ya ujirani mwema kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

"Wanyama hawa jamii ya paka wakubwa ni muhimu sana kwa kuweka mizania ya ikolojia sawa, maana wanadhibiti idadi ya wanyama wala nyasi kwa kuwala, bila hivyo hifadhi zote zinaweza kugeuka kuwa jangwa. 

"Hakuna mtalii atakayekuja hifadhini asitamani kumuangalia simba, mfalme wa pori. Wanapouawa maana yake tunashusha hadhi ya hifadhi zetu kiutalii na hivyo kutishia kupoteza mapato yanayotokana na utalii" amesisitiza Dkt. Kigwangalla. 

Amesema tukio hilo la kuuwawa kwa Simba wa Ikolojia ya Serengeti sio la kwanza kutokea hapa nchini ambapo mwishoni mwa mwaka jana simba wengine watano waliuawa pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha. 

"Mwaka huo huo mwanzoni simba watatu nao walipigwa risasi kikatili wilayani Serengeti huku mwaka 2015 simba 7 wakauwawa tena kwa sumu, huko huko Serengeti".

Akizungumzia sababu za ujangili huo amesema mara nyingi ni kwa ajili ya kulipiza kisasi baada ya ng’ombe wa wananchi kuliwa na simba, changamoto ambayo husababishwa na wananchi wenyewe kusogelea na kuweka makazi karibu kabisa na mipaka ya hifadhi za wanyamapori kwa lengo la kulisha mifugo pembezoni na wakati mwingine ndani ya hifadhi hizo kinyemela.

Simba ambao wanakadiriwa kuwa zaidi kidogo ya 22,000, pamoja na wanyama wengine jamii ya paka wamepungua sana miaka ya hivi karibuni kiasi cha kuwekewa tishio la kutoweka hapa duniani. Duma nao wanakadiriwa kubaki 1,200 pekee.
 Askari wa wanyamapori wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wakikusanya miili ya simba  tisa waliouwawa kikatili kwa kulishwa sumu, kukatwa na kuchomolewa baadhi ya viungo vyao na wananchi katika kijiji cha Nyichoka, wilaya ya Serengeti mkoani Mara  hivi karibuni kwa ajili ya kuwafanyia uchunguzi kubaini chanzo cha vifo vyao.
 Askari wa wanyamapori wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wakikusanya miili ya simba  tisa waliouwawa kikatili kwa kulishwa sumu, kukatwa na kuchomolewa baadhi ya viungo vyao na wananchi katika kijiji cha Nyichoka, wilaya ya Serengeti mkoani Mara  hivi karibuni kwa ajili ya kuwafanyia uchunguzi kubaini chanzo cha vifo vyao.

May 21, 2018

MAKAMPUNI 380 KUONESHA BIDHAA ZAO KATIKA MAONESHO MAKUBWA YA KIMAITAFA UTALII YA KARIBU KILIFAIR MJINI MOSHI

Mkurugenzi wa Kampuni ya Kilifair Ltd ,Tom Kunkler akizungumza mbele ya waandishi kuhusu tukio la Maonesho ya Kimatifa ya Utalii ya KAribu Kilifair yanayotaraji kufanyika mjini Moshi ,June 1 hadi 3 mwaka huu.
Viongozi wa Kampuni ya uokoaji ya Kilimanjaro SIR wakifuatilia maelezo juu ya manesho hayo yaliyokuwa yakitolewa kwa wanahabari.
Mkurugenzi Mwenza wa Kampuni ya Kilifair inayoratibu maonesho ya Karibu  Kilifair ,Dominic Shoo akizungumzia tukio hilo kubwa la Kitalii.
Baadhi ya Wanahabari wakifuatilia maelezo yaliyokuwa yakitolewa.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Uokoaji ya Kilimanjaro SIR ,Ivan Brown akizungumza wakati wa kikao na wanahabri kuhusu tukio hilo.
Baadhi ya Wanahabari.
Meneja Mauzo wa Shirika la Ndege la Ethiopian Airlines ,Fitsimt Dejene ambao ni miongoni mwa wadhamini wa Maonesho ya Kimataifa ya Karibu Kilifair yanayotaraji kufanyika mjini Moshi. 
Waratibu wa Maonesho ya Karibu Kilifair wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wadhamini wa maonesho hayo.

Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii,Kanda ya Kaskazini .

MAKAMPUNI 380 yanayojishughulisha na Utalii yanataraji kushiriki Maonesho ya Kimataifa ya Karibu Kilifair huku kampuni ya Kilifair Ltd inayoratibu maonesho hayo ikitangaza kuandaa safari za kifamilia zitakazoshirikisha watu kutoka nchi mbalimbali Duniani kujionea vuvitio vya utalii kwa lengo la kuvitangaza kimataifa.

Maonesho ya kimataifa ya Utalii yaliyopewa jina la Karibu Kilifair yanafanyika kwa mwaka wan ne sasa yakiwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya Utalii wa Tanzania na nje ya nchi ,kwa lengo la kutangaza bidhaa mbalimbali za Utalii ikiwemo vivutio mbalimbali.

Kwa mara ya kwanza Kampuni ya Kilimanjaro SIR inayojishughulisha na ukoaji wa wageni waliopata matatizo katika maeneo yenye miinuko kama Mlima Kilimanjaro na Meru inataraji kushiriki katika maonesho hayo huku Shirika la ndege la Ethiopian Airlines likitangaza kutumia maonesho hayo kutangaza vivutio vya Utalii kwa wageni watakaosafiri na ndege wa shirika hilo.

Maonesho ya Karibu Kilifair yanayoratibiwa na Kampuni ya Kilifair Ltd awali yalijukiana kama Kilifair yakidhaminiwa na Kampuni mbalimbali za ndani na nje ya nchi.

May 14, 2018

WAZIRI KIGWANGALLA AMTEUA MISS JOURNALISM TANZANIA 2018 KUWA BALOZI WA UTALII WA PORI LA AKIBA SELOUS

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na Miss Journalism Tanzania, 2018, Witness Teddy Kavumo (21) ambaye pia ni mshindi wa mwaka jana wa mataji manne ya Uanamitindo nchini Afrika ya Kusini, alipomtembelea ofisini kwake Jijini Dodoma mwishoni mwa wiki kwa ajili ya kuomba ufadhili wa kushiriki mashindano ya Dunia ya Miss Journalism yatakayofanyika Jijini Arusha mwezi Oktoba mwaka huu. Aidha, amemteua mwanamitindo huyo kuwa balozi wa utalii wa Pori la Akiba Selous. 

Na Hamza Temba-WMU-Dodoma
.............................................................................
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla amemteua mshindi wa taji la Miss Journalism Tanzania, 2018, Witness Teddy Kavumo (21) kuwa balozi wa utalii wa Pori la Akiba Selous.

Amefanya uteuzi huo mwishoni mwa wiki Jijini Dodoma baada ya mazungumzo na mwanamitindo huyo aliyemtembelea ofisini kwake kwa ajili ya kuomba ufadhili wa kuandaa  mradi wa kijamii ambao ni sehemu ya shindano atakaloshiriki la taji la Dunia la Miss Journalism 2018 litakalofanyika Oktoba 27 Jijini Arusha.

Kufuatia uteuzi huo, Dk. Kigwangalla amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania, Devotha Mdachi kuandika barua ya uteuzi kwa balozi huyo mpya sambamba na kumkabidhi hati ya uteuzi ili pamoja na mambo mengine aweze kunadi vivutio vya utalii vya pori hilo.

Wakati huo huo, Dk. Kigwangalla amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA, Dk. James Wakibara kuandaa safari maalum ya balozi huyo mteule aweze kutembelea Pori la Akiba Selous kwa ajili ya kuona na kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu hifadhi hiyo kwa ajili ya utangazaji.

Sambamba na pori hilo atatembelea pia mapori mengine ikiwemo BBK (Burigi, Biharamulo na Kimisi) mkoani Kagera na Mpanga Kipengele mkoani Njombe ambapo  atatumia fursa hiyo kufanya mahojiano na wasichana wa vijiji jirani na hifadhi hizo kwa ajili ya mradi wa kijamii wa kuwainua ikiwa ni sehemu yenye alama muhimu kwenye shindano hilo la Dunia la Miss Journalism 2018.

Awali akiwasilisha ombi lake kwa Waziri Kigwangalla la ufadhili wa safari yake ya ushiriki wa mashindano hayo, Witness pia aliomba kupewa fursa ya kuwa balozi wa Tanzania kwenye moja ya sekta ikiwemo Misitu, Nyuki au Utalii.

Mbali na kushikilia taji la Miss Journalism Tanzania 2018, Witness amesema amewahi kushinda mataji mengine manne makubwa ya kimataifa ya ulimbwende nchini Afrika ya Kusini anakosomea urubani kwa sasa.

Anasema, "Miongoni mwa mataji hayo ni Miss Garden Route 2017, ambalo ni taji la kitaifa la kuhamasisha na kukuza sekta ya Maliasili na Utalii nchini humo, licha ya kuwa ugenini nilitumia fursa hiyo kunadi vivutio vya utalii vya Tanzania. 

"Mashindano haya yalihusisha washiriki 600 na wote walikuwa na asili ya kizungu, mimi peke yangu nilikuwa na asili ya kiafrika na niliibuka mshindi". 

Aliyataja mataji mengine kuwa ni Miss Bees Cape Town 2017 kwa ajili kuhamasisha uhifadhi wa sekta ya nyuki na mataji mawili ya kimkoa ambayo ni Miss Asla Capetown 2017 na Miss Carnival Mosselbay 2017.

Mataji mengine ya kitaifa aliyowahi kushinda Witness hapa nchini ni pamoja na Miss Arusha Higher Learning 2014 na Miss Northern Zone 2014.

Mashindano hayo ya Dunia ya Miss Journalism 2018 yanahusisha pia uhamasishaji wa maendeleo ya utalii, utamaduni wa amani, uandishi wa habari na kupiga vita ugonjwa wa ukimwi na Malaria.

Pori la akiba Selous ndio hifadhi kubwa kuliko zote nchini ikiwa na ukubwa wa kilomita za mraba takriban 50,000 katika mikoa ya Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara na Ruvuma. Mwaka 1982, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Uneso) lilitangaza eneo hilo kuwa moja ya eneo la Urithi wa Dunia na kuanza kuhifadhiwa.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akionyeshwa taji la urembo la "Miss Garden Route South Africa 2017" ambalo ni maalum kwa ajili ya kuhamasisha utalii nchini Afrika ya Kusini na Miss Journalism Tanzania 2018, Witness Teddy Kavumo (21) aliyeshinda taji hilo na mataji mengine matatu nchini humo mwaka jana, alipomtembelea ofisini kwake mwishoni mwa wiki kwa ajili ya kuomba ufadhili wa kushiriki kwenye mashindano ya Dunia ya Miss Journalism yatakayofanyika Jijini Arusha mwezi Oktoba mwaka huu. Aidha, amemteua mwanamitindo huyo kuwa balozi wa vivutio vya utalii vya Pori la Akiba Selous. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiwa kwenye picha ya pamoja na Miss Journalism Tanzania, 2018, Witness Teddy Kavumo (21) ambaye pia ni mshindi wa mwaka jana wa mataji manne ya Uanamitindo nchini Afrika ya Kusini, alipomtembelea ofisini kwake Jijini Dodoma mwishoni mwa wiki kwa ajili ya kuomba ufadhili wa kushiriki mashindano ya Dunia Miss Journalism yatakayofanyika Jinini Arusha mwezi Oktoba mwaka huu. Aidha, amemteua mwanamitindo huyo kuwa balozi wa vivutio vya utalii vya Pori la Akiba Selous.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiagana na Miss Journalism Tanzania, 2018, Witness Teddy Kavumo (21) ambaye pia ni mshindi wa mwaka jana wa mataji manne ya Uanamitindo nchini Afrika ya Kusini, baada ya mazungumzo ofisini kwake Jijini Dodoma alipomtembelea mwishoni mwa wiki kwa ajili ya kuomba ufadhili wa kushiriki mashindano ya Dunia ya Miss Journalism yatakayofanyika Jinini Arusha mwezi Oktoba mwaka huu. Aidha, amemteua mwanamitindo huyo kuwa balozi wa wa utalii wa Pori la Akiba Selous. 

May 11, 2018

DK. KIGWANGALLA AFUNGUA WARSHA YA KITAIFA YA MAPITIO YA RASIMU YA SERA YA TAIFA YA UTALII YA MWAKA 2018

Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Hamisi Kigwangalla akifungua Warsha ya Kitaifa ya Mapitio ya Rasimu ya Sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 2018 Jijini Dodoma leo.
............................................

WAZIRI wa Maliasili na Utalii,Dk.Hamisi Kigwangalla amesema  Serikali itaendelea kutekeleza sera ya Taifa ya Utalii  kwa ushirikiano na wadau katika usimamizi, uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za maliasili na utalii nchini.

Dk. Kigwangalla ametoa kauli hiyo Jijini Dodoma leo wakati akifungua warsha ya kitaifa ya mapitio ya rasimu ya Sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 2018.

Amesema mafanikio ya sekta ya utalii yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na uwepo wa Sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 1999 na juhudi za Serikali katika kutekeleza sera hiyo.

“Sera hiyo kwa ushirikiano na Wadau katika usimamizi, uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za utalii, utangazaji katika masoko mbalimbali ya utalii duniani na mazingira bora ya uwekezaji.

“Wote tunaelewa ya kuwa Utalii ni moja wapo ya sekta zinazokua kwa kasi na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa nchi na kupunguza umasikini wa kipato”.

Amesema ukuaji wa sekta hiyo, umedhihirika pale ambapo katika miaka ya hivi karibuni mapato yatokanayo na utalii yaliongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 1.7 mwaka 2012 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 2.2 mwaka 2017.

Amesema ongezeko la mapato hayo ni kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watalii kutoka 1,077,058 mwaka 2012 hadi kufikia watalii 1,327,143 mwaka 2017.

Waziri Kigwangalla amesema sekta ya utalii inachangia takriban asilimia 25 ya mapato yote ya fedha za kigeni (foreign exchange earnings).

Akizungumzia mambo yaliyowekewa mkazo katika rasimu hiyo amesema ni pamoja na Serikali kuendelea kushirikiana na wadau wote wa utalii katika kuhifadhi rasilimali za utalii.

“Kuendeleza rasilimali watu, kuimairisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa, kuimarisha mnyororo wa thamani katika mazao ya utalii, kuongeza wigo wa mzao ya utalii kama vile kuendeleza utalii wa fukwe na utalii wa mikutano, kuweka mkazo katika kutangaza Tanzania kama kituo bora cha utalii kimataifa.

“Napenda kusisitiza kuwa, Sera hii itakuwa na nyenzo nyingine muhimu za kuitekeleza ambazo ni Mkakati wa utekelezaji wa Sera na Progamu ya Maendeleo ya Utalii nchini.

“Tayari Wizara imeanza maandalizi ya awali ya kukamilisha nyenzo hizo na mtashirikishwa kikamilifu katika kuziandaa na kuitekeleza wake,”alisema.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi amesema sera ya Taifa ya Utalii iliyopo hivi sasa ilifanyiwa mapitio kwa mara ya mwisho mwaka 1999 ambapo ni takribani miaka 18 iliyopita.

Amesema kwa kutambua hilo, Wizara iliona kuna umuhimu mkubwa kupitia upya Sera hiyo ili kuhakikisha ukuaji wa Sekta ya Utalii nchini unaenda sambamba na mabadiliko mbalimbali yanayotokea duniani ikiwamo mabadiliko ya teknolojia, kijamii, kiuchumi, kisiasa na kimazingira.

Aidha,alisema kwa kuzingatia kuwa msingi mkuu wa kuandaa Sera yeyote ni kuwashirikisha wadau ambao ndio watekelezaji wa Sera hiyo, mapitio ya Sera hii, yameshirikisha wadau wote muhimu tangu hatua za awali.

“Kazi hii ilipangwa kufanyika kwa awamu tano (5) ambazo ni kukusanya maoni ya wadau katika kanda saba za Tanzania Bara na Zanzibar, uchambuzi wa maoni na kuandaa rasimu ya Sera, kuwasilisha rasimu ya Sera kwenye warsha ya kitaifa ambayo inafanyika leo na hatimaye kuandaa rasimu ya mwisho ya Sera na Mkakati wa Utekelezaji,” alisema.

Warsha hiyo imejumuisha wadau mbalimbali wa sekta ya umma na binafsi wanaohusika maendeleo ya sekta ya utalii nchini.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Hamisi Kigwangalla akifungua Warsha ya Kitaifa ya Mapitio ya Rasimu ya Sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 2018 Jijini Dodoma leo.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi akizungumza katika warsha hiyo.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi akizungumza katika warsha hiyo.
Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Wizara ya Maliasili na Utalii Deogracious Mdam akizungumza katika warsha hiyo.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa ESRF, Deodatus Sagamiko akizumza katika warsha hiyo. ESRF ni moja ya wadau wakuu waliofadhili zoezi hilo la kuhuisha sera ya taifa ya utalii.
 Baadhi ya wadau katika wa warsha hiyo.
 Baadhi ya washiriki wa warsha hiyo.
 Meza kuu.
 Wadau. 
  
 Picha ya pamoja.
 Picha ya pamoja.
 Picha ya pamoja.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi (katikati) akifurahia jambo na Naibu Katibu wa Wizara hiyo, Dk. Aloyce Nzuki (kulia) na Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Deogracious Mdam wakati Warsha ya Kitaifa ya Mapitio ya Rasimu ya Sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 2018 Jijini Dodoma leo.
 Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Hamisi Kigwangalla akiteta jambo na mdau wa utalii, Dk. Leaky Abdallah wakati wa Warsha ya Kitaifa ya Mapitio ya Rasimu ya Sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 2018 Jijini Dodoma leo.
Baadhi ya wadau wa utalii kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii. (Picha na Hamza Temba - Wizara ya Maliasili na Utalii)

May 8, 2018

TANZANIA YATAJWA KUWA BUSTANI YA EDEN NA CHIMBUKO LA MWANADAMU WA KALE DUNIANI


Hatimaye utata uliokuwa ukiendelea duniani kwa watafiti wa mambo ya kale kuhusiana na mahali mwanadamu wa kwanza alipotokea umemalizika baada ya jopo la wataalam liloundwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kufuatia ushahidi wa vinasaba kubaini kuwa binadamu huyo alitokea barani Afrika huku ikidaiwa kuwa ni Tanzania eneo la Olduvai Gorge.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga wakati wa mkutano wa wadau wa sekta ya ufugaji nyuki aloiutisha kujadili maendeleo ya sekta hiyo Jijini Dodoma mwishoni mwa wiki.

Amesema  utafiti huo umeshirikisha wataalamu kutoka mataifa mbalimbali duniani na kuwa kumalizika kwake kutaiwezesha sekta ya utalii nchini kukua kwa kasi sambamba na kuongeza pato la taifa.

May 7, 2018

WAINGEREZA WAVUTIWA KUWEKEZA SELOUS, DK. KIGWANGALLA AAGIZA KUWEKWA MAKUBALIANO YA AWALI (MOU)

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akimuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA, Dk. James Wakibara (hayuko pichani) kushirikiana na wawekezaji kutoka nchini Uingereza kuandaa mkataba wa makubaliano ya awali (MoU) ya uwekezaji katika sekta ya utalii kwenye Pori la Akiba Selous, ofisini kwake Jijini Dodoma juzi. Wawekezaji hao pichani ni Eva Sanchez na Nicholas Negre.

Na Hamza Temba-WMU-Dodoma
..............................................................

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla ameagiza uandaliwe mkataba wa makubaliano ya awali (MoU) ya utekelezaji wa mradi wa kuendeleza utalii wa picha katika Pori la Akiba Selous.

Mkataba huo wa makubaliano utahusisha wawekezaji kutoka Jiji la London nchini Uingereza na Serikali ya Tanzania kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA na  utakapokamilika utasainiwa na pande zote mbili.

Dk. Kigwangalla ametoa agizo hilo juzi ofisini kwake Jijini Dodoma kufuatia maombi yaliyowasilishwa kwake na wawekezaji hao, Eva Sanchez na Nicholas Negre.

Akiwasilisha maombi hayo, Sanchez amesema mradi huo utakuwa wa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA ambao ndio wasimamizi wakuu wa Pori la Akiba Selous utakapoanzishwa mradi huo. 

Amesema pamoja na mambo mengine mradi huo wa utalii wa picha pia utasaidia kupiga vita ujangili na kukuza uchumi wa jamii zinazozunguka pori hilo.

Dk. Kigwangalla amewataka wawekezaji hao kuwasilisha andiko la mradi huo, kufanya utafiti wa kina na tathmini ya athari za kimazingira zitakazoweza kujitokeza kutokana na uanzishwaji wa mradi huo.

Amesema kwa sasa Serikali inafanya marekebisho ya Sheria mbalimbali zitakazoiwezesha Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA  kutekelezaji majukumu yake ipasavyo ikiwemo uwekezaji wa aina hiyo kwenye sekta ya Utalii wa Picha na Uwindaji wa Kitalii.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA, Dk. James Wakibara amesema mamlaka hiyo itatoa ushirikiano wa kutosha kwa wawekezaji hao ili kutimiza azma ya Serikali ya kushirikisha wadau, watu binafsi na wawekezaji katika kukuza sekta ya utalii nchini.

Pori la akiba Selous ndio hifadhi kubwa kuliko zote nchini ikiwa na ukubwa wa kilomita za mraba takriban 50,000 katika mikoa ya Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara na Ruvuma. Mwaka 1982, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Uneso) lilitangaza eneo hilo kuwa moja ya eneo la Urithi wa Dunia na kuanza kuhifadhiwa.
  Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na muwekezaji kutoka Jiji la London nchini Uingereza, Eva Sanchez ofisini kwake Jijini Dodoma juzi alipowasilisha ombi lake la kuwekeza kwenye sekta ya utalii wa picha katika Pori la Akiba Selous.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA, Dk. James Wakibara (kulia) akifafanua jambo kuhusu uwekezaji huo.
 Mkurugenzi wa Utalii na Huduma za Biashara wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA, Imani Nkuwi (aliyesimama) akifafanua jambo kuhusiana na uwekezaji huo.
 Waziri Kigwangalla akisisitiza jambo katika kikao hicho.
 Waziri Kigwangalla akitoa maelekezo katika kikao hicho.
   Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiagana na muwekezaji kutoka Jiji la London nchini Uingereza, Eva Sanchez ofisini kwake Jijini Dodoma juzi baada ya kupokea ombi lake la kuwekeza kwenye sekta ya utalii wa picha katika Pori la Akiba Selous.
Picha ya pamoja ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla,  Wawekezaji wanaotaka kuwekeza kwenye utalii wa picha katika Pori la Akiba Selous Eva Sanchez na Nicholas Negre, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA, Dk. James Wakibara (kushoto) na Mkurugenzi wa Utalii na Huduma za Biashara wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA, Imani Nkuwi (kulia).