Mbunge wa Bahi (CCM), Omary Ahmed Badwel akitoka Mahakamani huku akiwa chini ya ulinzi wa askari polisi baada ya kusomewa shtaka la rushwa ya sh. milioni moja kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Jonathan Liana.
***************************
MBUNGE wa Jimbo la Bahi (CCM), Omary Ahmed Badwel (43) leo
amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam,na
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru), kwa makosa ya rushwa
ya shilingi Milioni moja toka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya
ya Mkuranga,Jonathan Liana.
Wakili
wa Takukuru, Janeth Machullia na Ben Lincoln walidai mbele ya Hakimu
Mkazi Faisal Kahamba kuwa mshtakiwa huyo anakabiliwa na makosa mawili ya
rushwa.
Wakili
Machullia alidai kuwa kosa la kwanza ni la rushwa kinyume na kifungu
cha 15(1) (a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na.11 ya mwaka
2007, kuwa kati ya Mei 30 na Juni 2 mwaka huu katika maeneo tofauti
jijini Dar es Salaam , Badwel akiwa ni Mbunge wa Bahi na Mjumbe Kamati
ya Hesabu za Serikali za Mitaa(LAAC) na wakati huo akiwa ni ofisa wa
serikali kwa maana ya sheria ya Takukuru, alitenda kosa la kushawishi
ili apewe rushwa ya jumla ya Shilingi milioni nane toka kwa Sipora Liana
ili kiasi hicho cha fedha aweze kuwapelekea wajumbe wenzake wa Kamati
hiyo ya Bunge ili waweze kuipitisha ripoti ya fedha ya mwaka 2011/2012
ya Halmashauri hiyo.
Wakili
Machullia alidai shitaka la pili ni kwamba kati ya Juni 2 mwaka huu,
katika Hoteli ya Peacock,mshitakiwa akiwa na nyadhifa zake zote hizo
alipokea rushwa ya Milioni moja kutoka kwa Liana ili aweze kwenda
kuwashawishi wajumbe wa Kamati hiyo ili waweze kuipitisha ripoti ya
fedha ya Halmashauri ya Mkuranga huku akijua kufanya hivyo ni kosa.
Hata
hivyo mshitakiwa huyo anayetetewa na wakili wa kujitegemea Mpare Mpoki
alikanusha mashtaka yote na wakili wa Machullia alidai kuwa upelelezi wa
shauri hilo umekamilika.
Kwa
upande wake Hakimu Mkazi Kahamba alisema ili mshitakiwa apate dhamana
ni lazima awe na wadhamini wawili wa kuaminika ambao kila mmoja atasaini
bondi ya shilingi milioni nne na kusalimisha hati zao za kusafiria
mahakamani, sharti ambalo lilitimizwa na mshitakiwa huyo na akapata
dhamana. Hakimu Kahamba ameahirsha kesi hiyo hadi Juni 18 mwaka huu,
kesi hiyo itakapokuja kwa ajili ya kutajwa na kupangiwa tarehe ya kuja
kumsomea maelezo ya awali mshitakiwa huyo.
|
No comments:
Post a Comment