Tangazo

June 25, 2012

Mlipuko wa Bomu waua mtu mmoja Mombasa

Mtu mmoja ameuwawa katika mlipuko uliotokea katika baa moja iliyoko viungani mwa mji wa Mombasa nchini Kenya.

Polisi wamesema zaidi ya watu wanane wamejeruhiwa kufuatia shambulio hilo lililotokea saa nne, Jumapili usiku.

Shambulio hilo limejiri siku moja baada ya ubalozi wa Marekani nchini Kenya kuonya kuwa ''kulikuwa na tisho la kutokea shambulio la kigaidi'' katika eneo hilo.

Mapema wiki hii, maafisa wa polisi wa Kenya waliwakamata raia wawili wa Iran waliotuhumiwa kuhusika na mtandao wa kigaidi unaopanga kutekeleza mashambulizi mjini Mombasa.

Siku ya Jumamosi, polisi katika mji mkuu Nairobi, walisema kuwa walipata vifaa vinavyo shukiwa kutumika katika kutengeneza bomu.

Aliyehusika hajakamatwa bado

Mkuu wa polisi wa mkoa wa pwani, Aggrey Adoli, hata hivyo amesema hawezi kuhusisha moja kwa moja shambulio hilo la Mombasa na ilani iliyotolewa na Marekani.

''Taarifa tulizopata ni kwamba kifaa hicho ambacho tunashuku ni gruneti, kilirushwa na mtu mmoja aliyekuwa akiburudika kwenye baa hiyo. Hatukuweza kumnasa mtu huyo lakini tunaendelea na uchunguzi,'' Adoli aliambia kipindi cha Amka na BBC.

Mtu mmoja aliyeshuhudia tukio hilo amesema kuwa , wakati mlipuko huo ulipotokea, baa hiyo ilikuwa na wateja wengi waliokuwa wakitizama mechi ya robo fainali kati ya Uingereza na Italia, katika michuano ya kombe la taifa bingwa bara Ulaya.
 
Ufaransa pia ilitoa tahadhari

Mbali na Marekani, ubalozi wa Ufaransa mjini Nairobi pia umeonya raia wake '' kuwa waangalifu'' wakiwa katika mji huo wa Mombasa.

Marekani iliwatahadharisha raia wake kutozuru Mombasa hadi Julai mosi.

Mwezi Mei, mtu mmoja aliuwawa wakati kilipuzi kiliporushwa ndani ya mkahawa mmoja mjini humo.

Kumekuwa na msururu wa mashambulizi ya gurunedi tangu Kenya ilipopelekwa wanajeshi wake nchini Somalia kuwasaka wapiganaji wa kundi la kigaidi la Al- Shabab, mwezi Oktoba mwaka jana.

No comments: