Tangazo

October 19, 2012

Kariakoo na Maeneo ya Jirani Kimenuka: Polisi v/s Waislamu

DAR ES SALAAM

Vurugu kubwa zimetokea mchana huu katika maeneo yanayozunguka eneo la Kariakoo na kusababisha hofu kubwa na Polisi wamelazimika kutumia mabomu ya machozi na kutawanya mikusanyiko ya watu waliokuwa wamejiandaa kuandaamana kuelekea katika Ikulu ya Magogoni jijini.

Maduka yote katika maeneo hayo yamefungwa na shughuli mbalimbali zimesimama pamoja na Ofisi mbalimbali zimefungwa kutokana na hofu kubwa iliyotanda.

Kwa mujibu wa matangazo ya moja kwa moja ya Redio One wananchi wanakimbizana hovyo kukimbia mabomu ya machozi yaliyokuwa yakipigwa na Polisi kuwatawanya waumini waliokuwa wakitoka msikitini.

Hata hivyo taarifa kutoka eneo la tukio zinasema kuwa, waumini hao wameweza kutawanywa na hali bado tete huku magari ya jeshi la Polisi yakielekea katika maeneo ya Kinondoni ambapo kunadaiwa kuwa hali si shwari na vurugu kama hizo zinaendelea.

Na habari zilizotufikia sasa hivi Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limepeleka vikosi vyake katika maeneo ya Kariakoo ambapo vurugu zimekuwa kubwa ili kutuliza hali ya uvunjifu wa amani.


No comments: