Tangazo

October 29, 2013

Redd’s Uni-Fashion Bash sasa Moshi



Na Mwandishi Wetu, Mwanza

MAMBO YANAENDELEA! Tamasha la wanamitindo na wabunifu walio katika vyuo vikuu lijulikanalo kama ‘Redd’s Uni-Fashion Bash’, mwishoni mwa wiki hii linatarajiwa kufanyika mkoani Kilimanjaro, baada ya Mwanza kufungua pazia.

Tamasha hilo linalochochea vipaji ndani ya vyuo hivyo, mbali na Mwanza na Kilimanjaro pia litahusisha vyuo vilivyopo katika Mikoa ya Dar es Salaa na Iringa.

Akizungumzia tamasha hilo, Meneja Masoko wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Fimbo Butallah alisema, linatarajiwa kufanyika Jumapili ndani ya ukumbi wa Glessius uliopo mjini hapa.

Fimbo alisema, wanafunzi wa vyuo vyote vya elimu ya juu walio na mapenzi katika ubunifu na mitindo wanatarajiwa kushiriki shindano hilo, huku akiamini kukiwa na upinzani mkali zaidi ya ule wa Mwanza.

“Siku zote tunaamini katika kukuza vipaji zaidi, ila siku hiyo kutakuwa na burudani kali kutoka kwa msanii Jon Makini,” alisema Butallah.

Katika tamasha la awali lililofanyika Mwanza, kulikuwa na ushindani mkali katika mitindo ambapo Fahad Rajab kutoka Chuo Kikuu cha St. Augustine (SAUT) aliibuka mshindi akifuatiwa na Lucy Charles kutoka pia chuo hicho.

Fahad kwa ushindi huo alijinyakulia Sh 500,000 huku Lucy akitwaa Sh 400,000 na mshindi wa tatu Ally Thabit wa Chuo cha Biashara (CBE) akiondoka na Sh 300,000 huku Joseph Mmari wa SAUT aliyeshika nafasi ya nne pamoja na Victoria Newton pia kutoka chuo hicho aliyeshika nafasi ya tani kila mmoja akipata Sh 100,000.

Kwa upande wa wabunifu mshindi wa kwanza alikuwa Dotto Elius wa CBE aliyejitwalia Sh 700,000, akifuatiwa na Fahad Rajab wa SAUT aliyepata Sh 500,000 akifuatiwa na Rafaka Mtani wa Taasisisya Uhasibu (TIA) aliyeondoka na Sh 300,000.

Washindi wa nne na watano walikuwa ni Amedias Amedia wa SAUT na Elizabeth Mtani wa TIA ambao kila mmoja aliondoka na Sh 100,000.

Meneja Habari na Mawasiliano wa TBL, Edith Mushi alisema katika tamasha la leo, kwa upande wa wabunifu mshindi wa kwanza ataondoka na Sh 700,000 wa pili Sh 500,000 watatu Sh 300,000 huku wa nne na watano kila mmoja akiondoka na Sh 100,000.

“Tunataka kuinua vipaji vya wanafunzi wa vyuo katika tasnia ya mitindo, kwa sasa wanafunzi katika mikoa iliyobaki wanatakiwa wajiandae mno, maana kuna upinzani mkubwa,” alisema Edith.

Alisema, ana imani kubwa watafanikiwa kuinua vipaji vya wanafunzi walio wanamitindo na wabunifu.

“Tuna imani kubwa zawadi hizi pia zitaongeza chachu kwa wabunifu na wanamitindo kuendeleza fani hii ya mitindo. Lakini matamasha haya pia yatahusisha burudani za aina mbalimbali za kuvutia.

“Hii itakuwa sehemu muhimu ya kuwakutanisha wanafunzi wa vyuo na kada mbalimbali katika kufurahia na kubadilishana mawazo juu ya masuala ya ubunifu na mitindo, kwani kinywaji cha Redd’s Original kimekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza tasnia ya urembo, ubunifu na mitindo hapa nchini,” alisema Edith.

Kinywaji cha Redd’s Original pia ndicho kinachodhamini shindano la Redd’s Miss Tanzania na kinazalishwa na kusambazwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).

No comments: