Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
Dar es salaam.
Serikali imesema kuwa itaendelea
kuunga mkono juhudi za uzalishaji mali zinazofanywa na wananchi waliojiunga
katika vikundi mbalimbali vya uzalishaji mali katika maeneo mbalimbali
nchini.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar
es salaam na Waziri wa Nchi , Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji na
Uwezeshaji Dkt. Mary Nagu wakati akizindua Baraza jipya la Taifa la
Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ..
Amesema kuwa serikali inatambua na
inaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na wananchi katika kujiletea
maendeleo kupitia ushiriki walio nao katika vikundi mbalimbali walivyovianzisha
katika maeneo yao na kufafanua kuwa serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu
inaendelea kuunga mkono juhudi hizo kwa kuanzisha Baraza la Taifa
la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi.
Dkt. Nagu amesema Baraza hilo lina
jukumu kubwa ya kusimamia na kuratibu utekelezaji wa sera ya Taifa ya
Uwezeshaji wananchi kiuchumi ya mwaka 2004 na kufafanuam kuwa utekelezaji
wa mikakati na malengo ya Dira ya maendeleo ya mwaka 2025 ya kuiwezesha
Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati itaweza kufikiwa iwapo watanzania
watashiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Ameongeza kuwa Baraza hilo
lina jukumu la kuwaelimisha wananchi kuhusu tafsiri ya uwezeshaji
Wananchi kiuchumi ambayo kwa muda mrefu imekua ikipotoshwa na kusisitiza kuwa
dhana ya uwezeshaji sio kupitia mitaji pekee bali ni kujenga uwezo wa wananchi
kuweza kuziona fursa zinazowazunguka na kuweza kuzitumia kwa maendeleo yao.
“ Nchi zinazoweza kuendelea ni zile
ambazo zimejenga uwezo kwenye ushirika, lazima tujenge uwezo wa vikundi vyetu
ili tuweze kugundua wapi tunakwama na kutatua changamoto zilizopo ili tupige
hatua maana uwezeshaji sio kupitia mitaji au kupewa mkopo maana kuna watu
tayari wana mitaji lakini hawawezi kufanya kitu hao tunachokifanya tunawajengea
uwezo” Amesisitiza Dkt. Nagu.
Ameeleza kuwa ipo haja kwa vikundi
mbalimbali vilivyojiunga katika ushirika kuendelea kujenga uwezo ili viweze
kufanya makubwa na kuaminiwa na wadau mbalimbali pamoja na serikali huku akitoa
mfano wa uamuzi wa serikali kununua samani zinazotengenezwa na
watanzania.
Dkt. Nagu amesema kuwa serikali
imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya uboreshaji wa miundombinu inayolenga
kuwawezesha wananchi kiuchumi ikiwemo huduma za afya na elimu na kuwataka
wajumbe wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kuweka umuhimu katika maeneo
yatakayoleta matokeo ya haraka na yanayogusa maisha ya wananchi wengi hususan
kwenye kilimo, Ufugaji, Uvuvi, Misitu,Ufugaji Nyuki na Utalii.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza
hilo Bw. Omari Issa akizungumza mara baada ya kuzinduliwa kwa baraza hilo
amesema baraza hilo litaendelea kuwajengea uwezo wananchi kuzitumia fursa
zinazowazunguka kujiletea maendeleo.
Amesema baraza litaendelea kutoa
elimu kwa wananchi kwa kuwahamasisha kujenga uwezo katika vikundi vya ushirika
ili waweze kumiliki uchumi wa nchi huku akifafanua kuwa wananchi walio wengi
wanahitaji elimu kuhusu dhana ya uwezeshaji Kiuchumi na namna ya kutumia fursa
na mikopo wanayopata kutoka katika taasisi mbalimbali za fedha kupata faida .
Baraza hilo lenye wajumbe 9 litadumu
kwa miaka 3 huku likiwa na jukumu la kuhakikisha linawasaidia wananchi
kumiliki na kunufaika na fursa za kiuchumi zilizopo nchini.
No comments:
Post a Comment