Tangazo

January 21, 2014

Baba, mama, mtoto wafa ajalini mkoani Singida

Gari aina ya Noah iliyopata ajali kwa kugongana na lori katika eneo la Kijiji cha Isuna, mkoani Singida na kusababisha vifo vya abiria 13, jana.
Singida na Same
Familia inayowajumuisha baba, mama na mtoto ni miongoni mwa abiria 25 walipoteza maisha katika ajali za barabarani zilizotokea katika mikoa ya Singida, Lindi na Kilimanjaro.

Omari Shaban (44), mke wake Salma Omari na mtoto wao Nyamumwi Omari (10) wakazi wa Itigi, Singida, walifariki dunia baada ya gari walilokuwa wakisafiria aina ya Noah kugongwa na lori aina ya Scania katika ajali iliyosababisha vifo vya watu 13 mkoani humo.

Ajali hiyo ilitokea saa 1:32 asubuhi katika Kijiji cha Isuna, Wilaya ya Ikungi, Barabara Kuu ya Singida-Dodoma, ambapo watu watatu walinusurika na kupata majeraha madogo madogo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Geofrey Kamwela alisema Noah lilikuwa likitoka Itigi, wilayani Manyoni kwenda Singida Mjini na kwamba miili ya watu 10 walikuwa wameshatambuliwa na ndugu zao hadi jana mchana.

Alisema magari hayo yalikuwa yakipishana, lakini ghafla lori lilihama upande wake na kulifuata Noah upande wa kushoto mwa barabara, ambako lililigonga, kisha kuliburuza.

“Kwa sasa bado hatujajua chanzo cha ajali hiyo mbaya ingawa baadhi ya watu wanadai kuwa huenda dereva wa lori alisinzia na kusababisha lori hilo kuhama upande wake na kulifuata Noah. Uchuguzi utakapokamilika, tutatoa taarifa,” alisema Kamwela.

Aliwataja wengine waliofariki katika ajali hiyo kuwa ni Mkazi wa Msisi, Haji Mohammed (29), Wakazi wa Sajaranda; Mtunku Rashidi (68), Salehe Hamisi (28), Athumani Kalemba (38) na Ramadhan Mkenga, Mkazi wa Puma, Samir Shaban (20) na Mwaleki Nkuwi (35) ambaye ni mkazi wa Ikungi.

Miili ya abiria hao pamoja na watatu ambao walikuwa hawajatambuliwa, imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Mkoa wa Singida.

Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Banuba Deogratius amekiri kupokea miili ya watu 13 na kwamba kati yao, watoto ni wawili.

JK atuma salamu 

Rais Jakaya Kikwete ametuma salamu za pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Perseko Kone kutokana na vifo vilivyotokea katika ajali hiyo.

“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa mno na taarifa za vifo vya watu 13 akiwemo mtoto wa miezi minne,” alisema Rais Kikwete katika taarifa iliyotolewa na Ikulu jana.

No comments: