Tangazo

September 1, 2014

MTEMVU: CCM ITAUPUKUTISHA UPINZANI TEMEKE UCHAGUZI WA MITAA, SIYO KWA KUTUMIA NGUVU ILA MATUNDA YA UTEKELEZAJI ILANI


Na Bashir Nkoromo
Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu ametamba kuwa, CCM itapukutisha kwa kishindo upinzani wote katika jimbo hilo kwa kushinda mitaa yote katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

"Wala hatutatumia nguvu bali tutaichukua mitaa yote hata hiyo michache iliyopo sasa chini ya upinzani, kwa kutumia mtaji wa mafanikio makubwa tuliyoonyesha katika utekelezaji wa ilani ya CCM katika kipindi hiki", alisema Mtemvu.

Mtemvu alitoa tambo hizo wakati akihutubia mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Jumuia ya Wanawake Tanzania, Kata ya Azimio, kwenye Viwanja vya Shule ya Msingi Sokoine, katika Kata hiyo, Temeke jijini Dar es Salaam.

Alisema, CCM inao uhakika wa kutwaa viti vyote hadi kurejesha vichache vilivyopo sasa chini ya upinzani kwa kuwa mengi ambayo CCM iliahidi kupitia yeye wakati akiomba kuwa mbunge wa jimbo hilo katika uchaguzi mkuu uliopita yamefanyika.

Mtemvu alitaja baadhi ya yaliyotekelezwa kuwa ni pamoja na ujenzi wa barabara katika maeneo mbalimbali ambazo karibu zote zimeboreshwa kwa kujengwa kwa kiwngo cha lami tofauti na awali ambapo ilikuwa kero kubwa kwa kuwa zilikuwa hazipitiki kutokana na ubovu tena za vumbi.

"Zamani nilikuwa kila nikisimama jukwaani mnaniolea matatizo na kero lukuki hasa kuhusu hizi barabara, sasa leo hatuzungumzii matatizo ya barabara, tunazungumzia tu sasa kuboresha taa kwenye mitaa na barabara hizi", alisema Mtemvu.

Alisema, kuanzia mwezi huu Septemba, taa zote katika barabara na mitaa kwenye jimbo hilo zitawaka ambapo sasa zinafanyiwa maboresho ili zitumie nishati ya jua (solar) ili kupunguza changamoto ya gharama za malipo ya umeme wa taa hizo.

Mtemvu alisema, kukamilika kwa taa hizo itakuwa janga kwa vibaka ambao wamekuwa wakitumia fursa ya giza kujificha wakati wakivizia kuiba kwenye nyumba za watu na pia kukwapua wapitanjia nyakati za usiku.

Alisema mbali na kuboresha barabara CCM pia kupitia uongozi wake imeweza kuboresha hali za wananchi hasa kina mama na vijana kwa kuviwezesha vikundi vyao vya ujasiriamali kwa kuwakopesha fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali ambapo sasa zaidi ya vikundi 100 vimenufaika.

Mtemvu aliahidi kuendelea kushirikiana na wabunge wengine wa Temeke na mkoa wa Dar es Salaam kwa jumla kuhakikisha watendaji wabovu serikalini wanakabwa koo ili wawajibike ipasavyo kutumikia wananchi.

Pia aliahidi kuhakikisha anaedelea kupigania kupatikana kwa mazingira bora ya kufanya kazi zao mamalishe na bodaboda kwa kuwa wana mchango mkubwa katika maendeleao ya jamii.

"Najua haiwezekani bodaboda zote zikaingia mjini, lakini tunachofanya ni kupigania kuhakikisha unakuwepo utaratibu mzuri utakaowezesha baadhi kufika mjini bila kuharibu taratibu na sheria zilizopo. Pia Mamalishe kwa kuwa lazima waendelee na shughuli zao tunawatafutia utaratibu bora kufanya shughuli zao kwa amani badala ya kukimzwa kimbizwa na mgambo kila mara", alisema Mtemvu.

Katika mkutano huo, uliosheheni burudani mbalimbali ikiwemo msanii Omari Tego kuimba wimbo maalum wa CCM ambao ulikonga nyoyo za waliohudhuria, Mtemvu aligawa kadi kwa wanachama wapya 45 wa UWT.

No comments: