Mkurugenzi Mwendeshaji ZSTC, Mwanahiji Almas Ali |
.
Serikali inatoa bure miche 1,000,000 Unguja na Pemba
.Azma
ya Serikali ni kuendelea kuwapatia wakulima bei nzuri
Zanzibar
ZANZIBAR
ni visiwa vinavyosifika kwa uzalishaji wa karafuu bora duniani. Katika miaka 30
ya nyuma pia ilisifika kwa uzalishaji karafuu nyingi, zaidi ya tani 6,000
zilikuwa zikizalishwa kwa mwaka.
Wazee
wetu wakati huo walikuwa wakizijali, wakizithamini na wakizipenda sana karafuu
ukilinganisha na kizazi cha sasa. Walihakikisha karafuu zao wakiuza vituoni
tena zikiwa safi, zimekauka vizuri na kupata daraja la kwanza.
Zao
la karafuu linaongoza katika kuingiza kipato kwa wananchi na Taifa miongoni mwa
mazao yanayozalishwa Zanzibar na linaendelea kuwa chanzo muhimu cha fedha za
kigeni kwa Taifa baada ya sekta ya utalii.
Kwa
sababu hiyo, ndio zao hilo linaendelea kuwa chini ya udhibiti na uangalizi
makini wa Serikali kupitia Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC), chini
ya sheria namba 39 ya mwaka 1968 ili zao hili liendelee kuwa na tija zaidi kwa
wakulima, wananchi na Taifa kwa jumla.
Kutokana
na umuhimu huo wa zao la karafuu kwa maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa
wananchi, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imechukua jitihada zote kuliimarisha
zao hili ili kuongeza uzalishaji, tija na ubora katika soko la dunia.
JITIHADA
ZA ZSTC
-
Katika kuongeza kiwango cha uzalishaji, usafirishaji na ubora wa karafuu
Serikali imeongeza bei ya karafuu na mkulima anapata asilimia 80 ya bei ili
kumuwezesha mkulima kumudu gharama za uzalishaji kama vile kupanda miche na
kuishughulikia hadi izae na kusafisha mashamba.
-
Kupitia Wizara ya Kilimo na Mali Asili Zanzibar na Shirika la ZSTC, Serikali inazalisha
miche 1,000,000 na kutolewa bure kwa Wakulima Unguja na Pemba kila mwaka ambapo
wakulima wanahimizwa kuipanda na kuishughulikia hadi izae.
-
ZSTC inatoa mikopo nafuu kwa wakulima katika kurahisisha shughuli za uchumaji.
Mikopo hiyo ni kwa ajili ya maandalizi ya awali ya uchumaji kama vile kujenga
kambi, kununua majamvi na kuwalipa vibarua.
-
ZSTC imeviimarisha vituo vya zamani na kujenga vituo vipya vya manunuzi karibu
na wakulima ili kurahisisha shughuli za usafirishaji wa karafuu. Katika vituo
hivyo kuna huduma zote muhimu kama vile umeme, vyoo, vikalio, ulinzi na
wakulima wanapata huduma ya tende na kahawa katika vituo hivyo.
-
Sambasamba na uimarishaji huo wa vituo vya manunuzi, ZSTC imeweka mizani mpya
pamoja na kuimarisha huduma nyengine katika vituo vya manunuzi ambapo vituo
hivyo vinalingana na hadhi na thamani ya karafuu.
-
Serikali inaendelea na mpango wa kuifanya karafuu ya Zanzibar ijuulikane dunia
nzima kutokana na sifa zake za kipekee za ubora kupitia mradi wa Tasnia ya Mali
Bunifu (BRANDING). Mradi huu utaongera thamani na ubora wa karafuu ya Zanzibar
duniani.
MAMBO
YA KUFANYA
Wakulima
na wadau wa zao la karafuu ni vyema wakaunga mkono jitihada hizi za Serikali
kwa kuhakikisha sifa nzuri za ubora wa karafuu
za Zanzibar zinaendelea kwa kufanya yafuatayo:
-
Tuhakikishe karafuu zinauzwa katika vituo vya ZSTC na karafuu hizo tuhakikishe zinakuwa
safi na zisiwe na zaidi ya asilimia 2% ya takataka.
-
Tuhakikishe karafuu zinazopelekwa kuuzwa katika vituo vya ZSTC zinakauka
ipasavyo na zisiwe na zaidi ya asilimia 14% ya unyevu.
-
Tutumie jua kwa kuanikia karafuu na si kuzikaanga au kutumia mbinu nyengine
kuzikausha.
-
Tuhakikishe karafuu zinazopelekwa kuuzwa katika vituo vya ZSTC hazichanganywi
na unga wa makonyo, matende, mpeta na vitu vyengine visivyohitajika.
-
Tuhakikishe karafuu zinachumwa zikiwa zimepevuka vizuri.
-
Tuhakikishe karafuu tunazianika katika sehemu nzuri na safi kwa kutumia
majamvi.
-
Tuhakikishe hakuna magendo ya miche ya mikarafuu wala karafuu zenyewe ili
kulinda pato la Taifa linalotokana na zao la karafuu.
-
Kama ilivyo kawaida ya muda wa kazi, Vituo vinafunguliwa saa 1:30 asubuhi hadi
9:30 jioni, tunatakiwa tufuate utaratibu wa mda wa Vituoni.
-
Tuhakikishe kila Mdau wa zao la karafuu anatimiza wajibu wake ipasavyo ili
ubora wa karafuu za Zanzibar usipotee kirahisi.
AZMA
YA SERIKALI
Sera
ya serikali ya zao la karafuu ni kumnufaisha mkulima zaidi hivyo Serikali itaendelea na azma yake ya kutekeleza uamuzi
wake wa kuwapatia wakulima bei ya karafuu ya asilimia 80 ya bei ya soko la nje.
Hiyo
ilikuwa ni kauli ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.
Ali Mohamed Shein, wakati alipokuwa akizindua rasmi msimu wa ununuzi wa karafuu
wa mwaka 2014/2015 uliofanyika Mkoani, Kusini Pemba.
Alibainisha
kuwa huo ni uamuzi wa kisera na kwamba Serikali haitarudi nyuma kwa kuwa lengo
lake ni kuhakikisha kuwa zao la karafuu linaendelea kuwa zao la biashara kwa
Zanzibar.
Alieleza
kuwapatia wakulima bei hiyo ni miongoni mwa hatua nyingi zinazochukuliwa na
Serikali ya Awamu ya Saba kuhakikisha karafuu za Zanzibar zinaendelea kuwa na
ubora wake na kubakia kuwa kitambulisho cha Zanzibar.
Kwa
mujibu wa Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSTC Bi Mwanahija Almas Ali bei ya asilimia
80 imekuza usatawi wa wananchi na imetoa ari kwa wakulima kupanda mikarafuu na
pia imepunguza usafirishaji wa karafuu isivyo halali na imeongeza pato la Taifa.
Dk.
Shein alizitaja hatua nyingine kuwa ni pamoja na kuimarisha huduma za ununuzi
wa karafuu, kujenga barabara kwenye maeneo yenye karafuu nyingi, kutoa miche ya
mikarafuu kwa wakulima, kutafuta masoko ya nje na kuwatia mikopo wakulima.
Hatua
nyingine alieleza Dk.Shein, ni kufanya uamuzi wa kulifanyia marekebisho makubwa
shirika la ZSTC ili liweze kutekeleza majukumu yake kulingana na mazingira ya
sasa na matokeo yake mafanikio makubwa yameonekana tangu mabadiliko hayo
kufanyika.
Hata
hivyo Dk Shein alieleza kutoridhidhwa kwake na hatua ya baadhi ya wakulima
kutorejesha mikopo kwa Shirika hivyo alitoa wito kwa wakulima hao kurejesha
mikopo hiyo kwani Serikali haingependa kuwapeleka wananchi hao katika vyombo
vya sheria.
Dk.
Shein alihimiza jitihada zaidi kwa wakulima wa karafuu pamoja na wananchi kwa
jumla kutilia mkazo ulinzi katika mashamba ya karafuu ili kudhibiti wizi wa zao
hilo na kukemea vitendo vya baadhi ya wezi wa karafuu hukata matawi ya
mikarafuu wakati wakifanya vitendo hivyo viovu.
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alitumia fursa hiyo
kulipongeza shirika la ZSTC kwa kutekeleza mabadiliko makubwa ya muundo na
mfumo wa utendaji hadi kulifanya shirika hilo sio tu kujiendesha kibiashara,
lakini pia kupata ufanisi mkubwa katika shughuli zake.
Kwa
wa Waziri wa Biashara, viwanda na Masoko, Ahmed Mazrui, alirejea wito wa
Serikali kuwataka wakulima wa karafuu kuzingatia utunzaji mzuri wa karafuu
tangu wakati wa kuchuma hadi zinapopelekwa katika vituo vya ununuzi.
Aliwataka
wakulima kuzianika karafuu katika majamvi ili kulinda ubora wake na
kuwahakikishia kuwa serikali kupitia Shirika la ZSTC imejiandaa vya kutosha kwa
vifaa na masuala mengine muhimu kwa ajili kufanikisha kazi hiyo.
Waziri wa Biashara Nassor Ahmed Mazurui (wa pili kushoto). |
HISTORIA
YA KILIMO CHA KARAFUU
Historia
ya kilimo cha karafuu na hali ya upandaji wa mikarafuu visiwani Zanzibar
Karafuu
ni zao linalotokana na mkarafuu, ingawa karafuu hazimo katika kundi la vyakula
wala vinywaji, lakini ni kiungo muhimu sana. Karafuu zina matumizi kadha,
wakati fulani zinatumika kwenye utengenezaji wa sigara, upishi, utengenezaji wa
aina fulani ya dawa ya meno na pia mafuta yake hutumika kwa kuchua misuli.
Kutokana
na kitabu cha historia, mikarafuu ilianza kupandwa kwenye visiwa vya
Shelisheli, Mauritius na sehemu nyinginezo. Miche ya mkarafuu ililetwa Zanzibar
kutoka Mauritius mwaka 1818, miti hii imestawi zaidi Visiwani Unguja na Pemba
ambavyo vinatoa asilimia 80 ya karafuu zinazohitajika duniani. Uchumi wa visiwa
vya Zanzibar unategemea sana zao la karafuu.
Historia
ya upandaji wa karafuu visiwani Zanzibar inatuonyesha ilianza zamani sana.
Miche ya mikarafuu kuja kwake hapa ilitokana na visiwa vya Indonesia, mashariki
ya mbali, ilifika huko Madagasca na Shelisheli katika karne ya 19 na ndiyo
ikakuja Zanzibar na kupandwa wakati Wafalme wa Oman walipotawala.
Kimbunga
kiliwahi kutokea na na kiling'oa mikarafuu mingi, kwa hivyo kukawa na juhudi
mpya ya Wafalme wa wakati ule kupanda mikarafuu mipya. Ilikuwa si kitu hiari, bali ilikuwa jambo la lazima, watu wapande mikarafuu kwa
sababu kitu hicho kinasaidia uchumi.
Kabla
ya mapinduzi, mashamba ya mikarafuu yalikuwa ni ya watu binafsi, lakini baada
ya mapinduzi, serikali ilitaifisha ardhi na kuigawa kwa wananchi. Kila
mwananchi alipata eka tatu za kumuwezesha kulima, kupata chakula chake na
kupata mahitaji yake ili ajiendeleze na familia yake.
Hiyo
imeendelea mpaka leo, kwa hiyo sasa suala la karafuu linamilikiwa na wananchi
wenyewe. Idadi kubwa ya mashamba yalikuwepo ni ya wananchi wenyewe. Ingawa kuna
maeneo ya serikali, maeneo yanayomilikiwa na serikali ambayo yana karafuu na
serikali inawakodisha watu ambao wanataka kukodi, kuchuma na kuuza, mashamba
hayo yapo Zanzibar na Pemba.
Utaratibu
wa uatikaji, ugawaji na upandaji wa miche ya mikarafuu bado unashughulikiwa na
Wizara ya Kilimo ambayo ndiyo iliyopewa jukumu
hilo kwa kushirikiana na Shirika la Taifa la Biashara ZSTC, ZSTC waniwezesha
Wizara ya kilimo kwa kiipa fedha.
Serikali
kupitia ZSTC inachangia maendeleo ya zao la karafuu kwa kiwango kikubwa.
Inawalipa vibarua wanaoshughulikia kuendeleza upandaji wa mikarafuu mipya
katika sehemu mbalimbali ambazo mikarafuu imekufa, ZSTC inanunua zana za
kutengeneza miche na kupanda miche mpaka kuisambaza kwa wananchi.
Kwa
muntadha huo, ZSTC inajukumu kubwa la kuendeleza zao la karafuu na kulifanya likubalike
kimataifa na kuwainua wakulima visiwani humo huku mtazamo wa sasa wa hali ya
kibiashara ya nje ni kutafuta mazao zaidi ya karafuu pamoja na kuzalisha bidhaa
zitokanazo na zao hilo la karafuu (Packages).
ZSTC
kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo inaendelea kutekeleza mkakati wa
kuimarisha zao la karafuu kwa kuotesha miche mingi hadi kufikia milioni moja
kwa mwaka na kuwagaia wakulima.
Awali
ZSTC ilikuwa ikitumia si zaidi ya shilingi bilioni tano kununulia karafuu,
lakini, sasa linatumia zaidi ya bilioni 60 hali ambayo inathibitisha maendeleo
makubwa yaliofikiwa hadi sasa na shirika hilo la umma.
Malengo
ya baadae ya ZSTC ni kuendelea kuliimarisha zao la karafuu na kuhakikisha
linachukuwa nafasi ya kwanza katika kuchangia pato la taifa na fedha za kigeni
ambapo kwa sasa inashikiliwa na sekta ya utalii.
'KARAFUU
NI UHAI WA UCHUMI NA USTAWI WA ZANZIBAR'
No comments:
Post a Comment