Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam
(CBE) Prof. Emanuel Mjema akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu
maadhimisho miaka 50 ya chuo hicho yanayoendelea jijini Dar es salaam.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
Dar es salaam.
Hatua
iliyochukuliwa na uongozi wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam (CBE)
kuendelea kuweka msisitizo katika usimamizi wa maadili kwa wanafunzi imeanza
kuzaa matunda kufuatia kuogezeka kwa ufaulu wa masomo kwa wanafunzi wanaosoma
chuoni hapo.
Hayo
yamebainishwa leo jijini Dar es salaam na mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara
Dar es salaam (CBE) Prof. Emanuel Mjema wakati akitoa ufafanuzi kwa waandishi
wa habari kuhusu maadhimisho yanayoendelea ya chuo hicho kutimiza miaka 50
tangu kuanzishwa kwake Januari, 1965.
Amesema
suala la usimamizi wa maadili kwa wanafunzi na jamii nzima inayoingia chuoni
hapo limepewa kipaumbele kikubwa na uongozi wake tofauti na miaka iliyopita
hali ilinayokifanya chuo hicho kuwa mfano wa kuigwa vyuo pamoja na taasisi
nyingine za elimu ya juu hapa nchini.
“Chuo
chetu sasa ni mfano wa kuigwa na vyuo vingine hapa nchini kwa sababu tumeweza
kusimamia suala la maadili hasa uzingatiaji wa mavazi yenye staha kwa wanafunzi
hali iliyoongeza heshima kwa chuo chetu”.
Mbali na
suala la usimamizi wa mavazi kwa wanafunzi Prof amesema chuo hicho kimeendelea
kuhakikisha ulinzi na usalama kwa wanafunzi na jamii nzima inayoingia na kutoka
katika mazingira ya chuo hicho, kuimarisha ukaguzi katika maeneo yote muhimu ya
kuingilia wanafunzi na kuwatambua wanafunzi wote kwa kutumia vitambulisho vyao.
Amefafanua
kuwa chuo hicho sasa kinafurahia matunda ya mafanikio ya kutimiza miaka
50 tangu kuanzishwa
kwake yakiwemo mabadiliko na maboresho makubwa katika sekta ya elimu hasa ongezeko la udahili wa wanafunzi, ongezeko la fani za masomo
na kampasi za chuo hicho katika mikoa mingine nchini ikiwemo Dodoma, Mwanza,
Mbeya na Zanzibar.
Prof.
Mjema amefafanua kuwa chuo cha CBE sasa kinatimiza miaka 50 kikiwa chuo pekee
Afrika ya Mashariki na katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini
mwa Afrika (SADC) kinachotoa wanafunzi wa shahada ya vipimo.
“Chuo
hiki pekee ndicho kinachotoa mafunzo kwa ngazi ya shahada ya vipimo, ni chuo
kinachotegemewa sana katika ukanda huu wa nchi za Afrika Mashariki na SADC”
Amesisitiza.
Ameeleza
kuwa tangu kuanzishwa kwake Januari, 1965 na aliyekuwa Rais wa kwanza wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere , chuo hicho
kimepata mafanikio makubwa kwa kuongeza idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa kila
mwaka kutoka wanafunzi 25 mwaka 1965 hadi 14,000 mwaka 2014.
Mafanikio
mengine ni kuongezeka kwa kozi za masomo na ngazi za mafunzo hadi kufikia
shahada, kuongezeka kwa wakufunzi wenye shahada za uzamivu (PhD) chuoni
hapo pamoja na chuo kuanzisha
ushirikiano wa elimu na vyuo vikuu vingine nje ya nchi kikiwemo Chuo Kikuu cha
Eastern Finland katika utoaji wa mafunzo ya shahada za uzamivu kwa kutumia
TEKNOHAMA kwa nchi za SADC.
Ameongeza
kuwa katika kipindi cha miaka 50 ya
chuo hicho idadi ya kampasi imeongezeka kutoka 1 ya jijini Dar es salaam na
kufikia 4 katika mikoa ya Mbeya, Mwanza, Dodoma na upande wa Zanzibar huku
idadi ya wahitimu wa chuo hicho ikiongezeka kwa kipindi chote ikiwa zaidi ya
wanafunzi Laki moja.
Aidha,
katika kuhakikisha chuo hicho kinaendelea kuimarisha ubora wa elimu inayotolewa
kwa wanafunzi katika maadhimisho hayo,chuo kinaandaa matukio mbalimbali ya
ukusanyaji wa fedha kupitia chakula cha hisani, matembezi, midahalo ya wasomi
na mikutano wanafunzi wahitimu wa chuo hicho Zanzibar, Dodoma, Mwanza, Mbeya na
Dar es salaam kwa ajili ya ujenzi wa maabara, vyumba vya mihadhara ya wanafunzi
na madarasa.
Pia chuo
hicho kinaandaa mafunzo ya ujasiriamali yatakayotolewa kwa jamii ikiwa ni
sehemu ya kurudisha huduma kwa jamii kwa kuwajengea uwezo wajasiriamali, na kuwajengea uelewa wanafunzi ili waweze kuwa na
uchaguzi sahihi wa hatima yao ya baadaye pindi wanapohitimu mafunzo.
No comments:
Post a Comment