Tangazo

September 7, 2014

Watoto milioni 160 wanatumikishwa katika ajira mbalimbali Duniani

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akizindua rasmi kampeni ya kadi nyekundu katika kupambana na utumikishwaji wa mtoto hapa Tanzania wakati wa chakula cha jioni kilichoandaliwa na International Rescue Committee katika Hoteli ya Serena tarehe 5.9.2014.

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Na Anna Nkinda – Maelezo

Takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya watoto wanaotumikishwa Duniani inafikia milioni 169 kati ya hao wapo wenye umri wa miaka mitano, wanaotoka katika familia maskini ambao  hulazimika kufanya kazi ili waweze kuishi na hivyo kukoa fursa ya upata elimu na malezi bora.

Kwa upande wa Tanzania asilimia 27.5 ya watoto wenye  umri wa chini ya miaka 17 wanatumikishwa katika ajira hatarishi zikiwemo za kufanya kazi majumbani, sehemu za starehe, uvuvi, migodini, mashamba ya tumbaku na machungwa.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Mama Salma Kikwete wakati wa hafla ya chakula cha jioni kilichoandalia kwa ajili ya kampeni ya kupambana na utumikishwaji wa watoto  iliyoandaliwa na International Rescue Committee (IRC) na kufanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.

 Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema utumikishwaji wa  mtoto ni hali inayomkosesha mtoto  haki zake za msingi kama vile elimu, afya, malezi na kutokupata nafasi ya kucheza na watoto wenzake.

“Utumikishwaji wa mtoto unamadhara makubwa kwa mtoto mwenyewe, familia, jamii na taifa kwa ujumla. Kitendo hiki humsababishia mtoto kuathirika kiakili,kiafya kisaikolojia,kimakuzi na hata katika mazingira mengine hupelekea kifo chake”.

Pia husababisha umaskini kati ya kizazi hadi kizai, na hivyo kudidimiza maendeleo ya Taifa. Aidha mtoto anayetumikishwa  hukosa ndoto za maisha bora kwa siku za usoni kwa kuwa alikosa fursa hiyo akiwa mdogo.

Mwenyekiti huyo wa WAMA alisema mazingira mazuri ya kisera na kisheria yametayarishwa kwa ajili ya kuwalinda watoto dhidi ya unyanyasaji ukiwemo wa utumikishwaji katika ajira hatarishi kinachotakiwa ni juhudi za pamoja ili kuhakikisha watoto hawatumikishwi katika jamii.

Akimkaribisha Mama Kikwete ili aweze kuongea na wageni waliohudhuria hafla hiyo Mkurugenzi wa IRC Tanzania Elijah Okeyo alisema Ili kukabiliana na tatizo la ajira za watoto mwishoni mwa mwaka 2012 Serikali ya Marekani kupitia idara ya Kazi iliwapatia   dola milioni 10 kwa ajii ya mradi wa WEKEZA ambao unafanya kazi zake katika wilaya sita zilizopo katika mikoa ya Tanga na Kigoma.

Kupitia mradi huo watoto 15,000 walitoka  katika ajira hizo, walilindwa ili wasiweze kujihusha na ajira za watoto  na kuweza kurudi shuleni kuendelea na masomo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa IRC wa Kanda ya Afrika ya Mashariki na Pembe ya Afrika Kurt Tjossem alisema kazi ya kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi ni ya kila mtu na siyo ya mtu mmoja hivyo bsi wadau wote wa watoto waendelee kuwekeza katika elimu kwani ndiyo ukombozi wa maisha ya mtoto.

Alisema inasikitisha kuona mtoto anaacha shule na kwenda kufanya kazi ili aweze kuongeza kipato cha familia hali hiyo siyo kama inawaweka mbali na utoto wao bali inawaharibia maisha yao ya baadaye lakini kuna matumaini kwao ambayo yataanzia kwa jamii yao lakini ili waweze kufanikiwa ni lazima wadau wote wawaunge mkono.

Licha ya kufanya kazi zake hapa nchini IRC pia inafanya kazi katika nchi 40 za kuokoa maisha, kuwasadia  watu ili waweze kujenga upya maisha yao, kuwalinda watu ambao maisha yao yameathiriwa na vita pamoja na majanga ya asili.

No comments: