Na Anna Nkinda –
Maelezo
Kuwepo
kwa sheria na sera katika shule za
msingi na Sekondari na kutoa elimu kwa
wanajamii hasa wazazi na walezi kutapunguza mimba za utotoni zinasababisha
vijana wa kike kushindwa kuendelea na
masomo, kupoteza maisha yao na watoto watakaowazaa.
Hayo yamesemwa na Afisa
Elimu Sekondari wilaya ya Temeke Mwalimu Chavila Donald wakati akifungua
mafunzo ya elimu ya afya ya uzazi,
ujinsia na stadi za maisha kwa
wanafunzi na walimu wa shule za
Sekondari za wilaya hiyo yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa shule ya
Sekondari Kibasila.
Mwalimu Chavila alisema
wanafunzi ni watu wa muhimu wanategemewa
katika familia, jamii na taifa katika kuleta maendeleo na kupunguza umaskini. Pamoja na changamoto wanazozipata bado
wanawajibu wa kujilinda na kujitunza ili waweze kufikia ndoto zao.
“Kitu kikubwa
mnachotakiwa kikifanya ni kusoma kwa
bidii na kufanya vizuri katika masomo yenu ili muweze kuleta tofauti katika
jamii pamoja na kuwa na maisha bora na kujiwekea misingi imara ya maisha ya
baadaye”, alisema Mwalimu Chavila.
Kwa upande wa walimu
aliwahimiza kuwa msaada wa kitaaluma na
kijamii kwa wanafunzi na kuhakikisha watoto wanapata elimu bora itakayowakwamua
kifikra, kijamiii na kiuchumi.
Alisisitiza , “Elimu
ndiyo silaha na nyenzo pekee ya kusukuma maendeleo ya watu na ya vitu kwa Dunia
ya leo. Fikirieni na toeni mapendekezo ya jinsi ya kuishi kwenye ulimwengu wa utandawazi, hata
kama italazimu kurekebisha mitaala ili iendane na matakwa ya mazingira haya
mapya”.
Naye Meneja
Uraghibishi na Mawasiliano kutoka
Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) Philomena Marijani alisema mafunzo hayo
ya siku tano yako chini ya mradi wa kuzuia mimba za utotoni katika shule za
sekondari unaotelelezwa na Taasisi hiyo na Engender health kwa ufadhili wa Shirika
la Maendeleo la watu wa Marekani.
Aliyataja malengo ya
mradi kuwa ni kuimarisha uelewa na ujuzi kuhusu afya ya uzazi kwa vijana wenye
umri wa kati ya miaka 14-19,kuongeza uhusishwaji na ushiriki wa wazazi ,
walezi, walimu na jamii kupinga mimba za utotoni na maambukizi ya Ukimwi kwa
vijana na kufanya uraghibishi wa uelewa kwa njia za uzazi wa mpango ambazo
zitasaidia kupunguza vifo vya akina mama na mimba zisizotarajiwa.
Philomena alisema, “Baadhi
ya mafanikio yaliyopatikana katika mradi huu ni shule za Sekondari 40 zimepata
mafunzo ya afya ya uzazi na stadi za maisha ambayo yatamsaidia mtoto wa kike
kujikinga na mazingira hatarishi pamoja na kufanya vyema katika masomo yake na
kujiwekea malengo, klabu 40 zenye jina la jilinde
utimize ndoto yako za uelimishaji rika na stadi za maisha zimeanzishwa”.
Mikutano minne ya
uhamasishaji jamii yenye lengo la kuwaelewesha wanajamii wajibu wao katika
kuwalinda watoto wa kike na mimba za utotoni iliweza kufanyika na klabu 20 za kijamii zilizojumuisha wazazi,
wasanii, waandishi wa habari na viongozi wa dini zenye jina la wote tunawajibu wa kuleta mabadiliko katika jamii zilianzishwa”.
Aidha Afisa Miradi
kutoka Engender health Dkt. Martha Kisanga aliwapongeza wanafunzi hao pamoja na
walimu kwa kuwa miongoni mwa watu waliohudhuria mafunzo hayo ambayo yatawasaidia kupata elimu ya afya ya uzazi, ujinsia na stadi za maisha.
“Msikilize kwa umakini
yale yote mtakayofundishwa kwani baada ya hapa mtakwenda kutoa elimu kwa
wenzenu mliowaacha shuleni ili nao waweze kujiamini na kujua haki zao za msingi
ikiwemo haki ya uzazi kwa kijana”,
alihimiza Dkt.Martha.
Mradi wa kuzuia mimba za
utotoni katika Shule za Sekondari ulianzishwa mwaka 2010 -2012 na kufanyika katika mkoa wa Lindi kwenye wilaya za Lindi
vijijini na Kilwa, Mkoa wa Mtwara katika wilaya za Nanyumbu na Masasi na mwaka 2014-2015 mradi unatekelezwa katika mkoa
wa Dar es Salaam wilaya ya Temeke.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment