Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa hivi karibuni alimteua Dk. Ally Yahaya Simba (pichani), kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania, (TCRA) kufuatia mchakato wa kumpata Mkurugenzi Mkuu kama ilivyoainishwa
katika Sheria ya Kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mawasiliano ya 2003 kifungu cha 9 na
kifungu cha 13. (TCRA Act, 2003)
Dk. Simba aliteuliwa rasmi kushika wadhifa
huo mnamo tarehe 6 Jula1 2015 kwa kipindi cha miaka mitano. Kabla ya uteuzi huo,
Dk. Simba alikuwa Kaimu Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
(TEHAMA) Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia tangu Agosti 2013. Dk.
Simba ana uzoefu wa zaidi ya miaka 16 katika Sekta ya Mawasiliano ambapo
amefanya kazi kwa watoa huduma, Taaluma ya Utafiti, Udhibiti pamoja na Serikali
Kuu.
Mnamo mwaka 2011 hadi mwaka 2013, alifanya
kazi Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kama Meneja Mipango na Utafiti wa
Mamlaka.
Dk. Simba ametoa machapisho kadhaa
yaliyosambazwa kote duniani katika majarida ya kimataifa na amewasilisha
matokeo ya tafiti zake katika zaidi ya mikutano 30 ya kimataifa ndani na nje ya
Tanzania. Aidha Dk. Simba alikuwa Kiongozi wa timu ya wataalamu wa Kitanzania
iliyoandaa Sheria za Uhalifu wa Mitandao nchini iliyopitishwa na Bunge hivi
karibuni.
Dk. Simba ni Mhandishi Mahiri (Chartered Engineer), aliyesajiliwa
nchini Uingereza katika Baraza la
Uhandisi nchini humo na ni “Fellow” wa Taasisi ya Uhandisi na Teknolojia ya nchini
Uingereza, ambako alifanya kazi kama Mshauri wa Kimataifa wa Usajili wa Wanataaluma Wahandisi kutoka
Aprili 2011 mpaka Machi 2014. Pia Dk. Simba ni Mwanachama wa “Institute of
Electrical and Electronics Engineers” (IEEE). Hali kadhalika Dk. Simba amechapishwa
katika jarida la “Marquis Who's Who in
Science and Engineering” katika toleo la 11, la mwaka 2011–2012.
Dk. Simba ni miongoni waliopata Udhamini wa
Serikali ya Japan (Monbusho Scholarship) kutoka mwaka 2000 mpaka 2006.
No comments:
Post a Comment