Tangazo

March 2, 2016

WAZAZI WALALAMIKA KUFUNGWA KWA MATAWI YA CHUO KIKUU CHA ST. JOSEPH


Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii Kanda ya Kaskazini.

BAADHI   ya wazazi wa wanafaunzi waliokuwa wakisoma Chuo Kikuu cha St Joseph katika  matawi ya Arusha na Songea wametupa lawama kwa Tume ya vyuo vikuu nchini (TCU) kwa hatua yake ya kufuta vibali vya kuanzisha matawi hayo na kwamba hali hiyo imewathiri watoto wao.

February 26 mwaka huu ,tume ya vyuo vikuu ilitangaza kufuta kibali cha chuo kikuu cha St Joseph (SJUIT) tawi la Arusha ikiwa ni wiki moja imepita tangu kuchukuliwa kwa hatua kama hiyo kwa Chuo kikuu cha St Joseph tawi la Songea,vyuo vilivyoko chini ya shirika la kitawa la Dada wa Maria Imakulata (DMI).

Wakizungumza na mtandao huu kwa nyakati tofauti baadhi ya wazazi wameeleza kusikitishwa na hatua hiyo huku wakidai kuwaathili kisaikolijia watoto wao ambao wengine walikuwa katika maandalizi ya mitihani.

“Nadhani ingekuwa ni jambo la busara  kwa TCU kukaa meza ya mazungumzo na uongozi wa chuo badala ya kuchukua hatua ya kukifutia vibali….Chuo hiki kimekuwa kikitoa mchango mkubwa katika kuzalisha wataalumu mbali mbali.”alisema Mrisho Sume.

Nchi yetu ina wataalamu wachache  katika sekta ya Sayansi na Teknalojia ,chuo hiki kilikuwa ni kimojawapo kinachotoa wataalamu hao hivyo mchango wake unapaswa kuheshimika na kusaidiwa pale inapobidi,” aliongeza Sume ambaye mwanaye alikuwa akisoma katika chuo cha Sayansi ya kilimo katika chuo hicho tawi la Songea.

Mzazi mwingine alijitambulisha kama Mariam Ali alisema taarifa alizokuwa nazo ni kuwa uamuzi wa kufunga baadhi ya matawi hayo ulifikiwa bila ya kukipa taarifa chuo hicho juu ya mapungufu yaliyopo ikiwa ni pamoja na kukipa muda wa kuyafanyia kazi.

“Binti yangu alikuwa akisoma tawi la Arusha na nimepata taarifa kuwa  timu ya ukaguzi kutoka tume ilifika chuoni hapo   kwa ajili ya ukaguzi lakini cha kushangaza ni kuwa chuo hakikupewa taarifa ya mapungufu yaliyoonekana ili yafanyiwe kazi na badala yake kililetewa barua za kufutiwa vibali.”alisema Mariam.

Uamuzi ulifanywa ni wazi haukuzingatia haki na unatuumiza sisi wazazi pamoja na watoto wetu, tulitegemea TCU kukipatia chuo  ripoti ya mapungufu waliyoyagundua na kupewa muda wa kuyafanyia kazi  na endapo kingeshindwa kuyafanyia kazi katika muda ambao kimepewa tume ingekuwa na haki ya kutoa adhabu,” aliongeza Mariam.

Naye John Budigle alisema tangazo lilitolewa na TCU kuhusu kufunga vyuo hivyo lilisema moja ya matatizo yaliyopelekea kufungwa ni migomo ya wanafunzi huku akiongeza kuwa migomo yote  ilitokana na kucheleweshewa mikopo na siyo matatizo ya chuo .

“Mimi kwa mtizamo wangu naona kama TCU imetumia nguvu kubwa kwenye suala hili, kama chuo kilifanya makosa kilipaswa kupewa maelekezo ya kushughulukia kasoro au mapungufu kwani hakuna chuo kisichokuwa na mapungufu hata hivyo vya umma. “alisema Budigle.

“Hatua hii inawavunja moyo wawekezaji katika sekta ya elimu. Hawa ni wadau katika elimu na ni vizuri TCU wakatuchukuliwa hivyo. Wao ni wasimamizi ambao wanatakiwa kuwaongoza na kuwarekebisha pale wanapokosea. Kitendo cha kukifutia vibali bila kufuata haki kinawavunja moyo wadau wa elimu pamoja na wanafunzi pia,” aliongeza Budigle.

Akitangaza hatua hiyo hivi karibuni  Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Yunus Mgaya, alizitaja sababu za kufikia uamuzi huo kuwa ni matukio ya migogoro ya muda mrefu baina ya uongozi wa chuo hicho na wanafunzi na ukiukwaji wa sheria za uendeshaji wake kama ulivyobainishwa na Sheria ya Vyuo Vikuu.

No comments: