Tangazo

December 23, 2016

THE GUARDIAN LTD YAMLILIA MPOKI BUKUKU

Mpoki Bukuku enzi ya uhai wake
          Tumepoteza nguzo katika tasnia ya habari


 Leo, kama ilivyo kwa wengine wengi, nimepokea kwa mshtuko mkubwa na kutoamini, kuhusiana na kifo cha ghafla cha mmoja wa wapigapicha waandamizi wa The Guardian Limited, Bw. Mpoki Bukuku (44), aliyefariki asubuhi kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Kwa familia yake, wamempoteza baba, mume na zaidi ya yote rafiki wa kweli, lakini kwetu sisi The Guardian Limited, tumempoteza pia rafiki wa kweli na nguzo katika tasnia ya uandishi wa habari.

 Bukuku alikuwa ni mwanadamu tu kama ilivyo kwa yeyote kati yetu, lakini katika uandishi wa habari, alikuwa ni mtu aliyeipenda fani yake na hakuogopa kupambana alimradi apate habari nzuri. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana kuna wakati kiu yake ya kupata habari nzuri kuliko wengine wote ilimuweka matatani.

Wale wanaoelewa uandishi wa habari wa picha watabaini kwamba ujasiri na kuipenda kazi ni sifa kuu mbili za kila mpigapicha ili kupata habari nzuri na yenye nguvu. Bukuku alikuwa na sifa zote hizo mbili. Alikuwa shujaa na mwenye mapenzi na kazi yake hasa wakati akifuatilia habari kubwa kokote kule katika nchi hii.

 Alipigwa na hata kuteswa na maadui wa uhuru wa vyombo vya habari, lakini bado mahaba yake katika kufanikisha habari bora hayakuzimwa. Alikuwa ni mwandishi wa habari siyo kwa bahati mbaya, bali ni kwa kuchagua na ndiyo maana alikuwa na mapenzi wakati akitimiza wajibu wake wa kutekeleza kazi mbalimbali za kihabari alizopangiwa na wahariri wake.

Bukuku amemaliza safari yake duniani, kimwili hayuko nasi lakini kiroho na kiuweledi, mara zote atakuwa nasi daima.

Sisi katika Kampuni ya The Guardian Limited tunaungana na famila, ndugu na marafiki katika kippindi hiki kigumu, kuombeleza msiba wa mtu ambaye tumekuwa tukifanya naye kazi kwa miaka mingi. Kampuni itaiunga mkono kwa ukamilifu familia ya marehemu Bukuku.

Kwa niaba ya wafanyakazi wote wa The Guardian Limited, kwa heshima kubwa natoa salamu zangu za rambirambi kwa mjane wa Bukuku, Lucy, watoto na wadau wote wa tasnia ya habari nchini Tanzania, kwa kifo cha ghafla na kushtua cha mmoja wetu.

Richard Mgamba
Mkurugenzi Mtendaji,
The Guardian Limited
Desemba 23, 2016

No comments: