Tangazo

October 7, 2011

Malawi kuunda Tume ya kuchunguza Ghasia

Rais Bingu wa Mutharika
Rais wa Malawi Bingu wa Mutharika ameambia BBC kuwa ataunda tume ya kuchunguza ghasia zilizozuka mwezi wa Julai.

Karibu watu 19 walipigwa risasi na polisi wakati walipoandamana kupinga serikali katika miji mikubwa nchini Malawi.

Bwana Mutharika amesema polisi wasingeweza kuvumilia wakati watu wanachoma maduka.

Alisisitiza msimamo wake kuwa waandamanaji "waliongozwa na Shetani" kwa kuwa walikataa kujadiliana naye juu ya masuala yao na kuamua kwenda barabarani.

Bwana Mutharika alikuwa akizungumza katika mahojiano ya kipekee ya kipindi cha mjadala cha BBC, Africa Have Your Say ikiwa ni mahojiano yake ya kwanza ya kina tangu hali hiyo kutokea mwezi Julai.

" Hivi karibuni, katika muda wa saa 48 zijazo, tutatangaza tume huru ya kuchunguza nini hasa kilitokea," alisema.


Maandamano yalisababishwa na kile upinzani ilieleza kuwa hali mbaya zaidi ya uchumi iliyoikumba Malawi tangu walipopata uhuru, huku nchi ikiwa na uhaba wa mafuta, mgao wa umeme na kutokuwepo kwa pesa za kigeni za kutosha.

Bwana Mutharika aliwashtumu waandamanaji kwa kufanya uhaini na kutuma jeshi pamoja na polisi wa kukabiliana na ghasia kukabiliana nao.

Lakini katika mahojiano hayo ya BBC amekanusha madai ya waandamanaji kuwa yeye ni dikteta.

No comments: