Tangazo

January 17, 2012

Nahodha wa Meli iliyopinduka alaumiwa

Meli ya Consta Concordia ikititia majini.

Idadi ya watu wasiojulikana walipo baada ya meli ya kifahari kupinduka katika ufuo wa Italia Ijumaa iliyopita, imefikia watu 29, watu sita kati yao wakiwa wamethibitishwa kufariki.

Wakati shughuli za uwokozi zikiendelea, shirika la habari la Italia (Ansa), limeripoti kuwa nahodha wa meli hiyo Francesco Schettino, amelaumiwa kwa kukwepa juhudi za kuwaokoa waliokuwa wakizama katika meli hiyo.

Nahodha huyo anayehojiwa na maafisa wa polisi, pia amelaumiwa na mwenye meli kwa kuacha makusudi kufuata njia ya kawaida ya meli hiyo.

Hata hivyo nahodha huyo anasisitiza kuwa alifuata utaratibu sawa wakati wote alipokuwa katika meli hiyo. 
 
Nahodha akamatwa

Nahodha wa meli hiyo amekamtwa kwa tuhuma za mauaji na jaji anatarajiwa baadaye hii leo kuamua iwapo nahodha huyo mweye umri wa miaka 52 ataendelea kushikiliwa na polisi .

Italia imesema itatangaza hali ya tahadhari kufuatia kupinduka kwa meli hilo, na kwamba itatoa msaada kuzuia janga lolote kwa mazingira.

Waziri wa mazingira wa Italia anasema anahofia kuwa mafuta huenda yakavuja kutoka kwenye meli hiyo.

Watu ambao bado hawajapatikana ni pamoja na wafanyikazi wa meli hiyo pamoja na abiria kutoka Marekani, Ufaransa na Italia.
Source: BBC Swahili

No comments: