Tangazo

February 1, 2012

Wizara ya Maliasili kushirikiana na Idara mbalimbali za Serikali Kukomesha Usafirishaji Haramu wa Maliasili

Maimuna Tarishi
Na Mwandishi wa Jeshi la Polisi- Zanzibar

ZANZIBAR JUMATANO FEBRUALI 1, 2012. Idara ya Wanyamapori nchini kwa kushirikiana na Idara nyingine za Serikali vikiwemo Vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa pamoja vimekubaliana kudhibiti usafirishaji haramu wa nyara za Serikali na mazao ya Maliasili vikiwemo viumbe hai na miti ya uwoto wa asili.


Afisa Habari wa Jeshi la Polisi Zanzibat Inspekta Mohammed Mhina, amesema kuwa hayo yamesemwa leo mjini Zanzibar na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Bibi. Maimuna Tarishi, wakati akifungua mkutano wa siku mbili kwa Maafisa wa Idara 16 za Serikali kutoka Tanazania Bara na Visiwani.

Bi.Tarishi amesema kuwa Serikali imeazimia kuviunganisha vyombo mbalimbali kama wadau katika kudhibiti vitendo vya uhalibifu na matumizi mabaya ya maliasili zetu ili ziendelee kuwa urithi wa vizazi vya sasa na vijavyo.

Amesema changamoto zilizopo hivi sasa ni kuwa kumejitokeza makundi ya watu wachache ambao kwa uchu wao wa kutaka utajiri wa haraka haraka wamekuwa wakishirikiana na magenge ya watu wengine kuzihujumu maliasili zetu.

Katibu Mkuu huyo amesema wakati sasa umefika wa kuvishirikisha vyombo vyetu kuhakikisha kwamba kwa pamoja vinalinda maliasli hizo kwani maliasili ni suala mtambuka na linamgusa kila mmoja wetu.

Amewataka washiriki wa semina hiyo kuweka mikakati itakayoweza kusaidia kuimarisha ushirikiano kwa vyombo hivyo ili kwa pamoja vishiriki katika kulinda maliasili za nchi yetu zisitoroshwe kwenda nje ya nchi kwa manufaa ya watu wachache.

Awali Kaimu Mkurugenzi Idara ya Wanyamapori Wizara ya Maliasi na Utalii Bw. Paul Sarakikya, amesema kuwa idara yake imeanza kufanya utafiti wa kujua maeneo yenye bandari bubu zinazotumika katika kusafirishia maliasili baharini.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkataba wa Lusaka wa kuhifadhi wa Wanyamapori na mimea Bw. Timothy Rwegasira, amesema kuwa hali ya ujangili na usafirishaji kwa magendo nyara za serikali ni mkubwa.

Amesema Majangili wamekuwa wakishirikiana katika kufanikisha uhalifu huo, hivyo ipo haja pia kwa vyombo vyetu vya ulinzi na Usalama kushirikiana kwa karibu na maafisa wa maliasili katika kukomesha vitendo vya kijangili vinavyofanywa na magenge hayo ya kihalifu.

Naye Mwakilishi wa Jeshi la Polisi Zanzibar SP Omari Amiri Omari, amesema kuwa ipo haja ya Washiriki wa Semina hiyo wakaweka sawa masuala ya kisheria kwa mfano Zanzibar haina Tembo lakini Meno ya Tembo yanapitia Zanzibar.

SP Omari amesema kutokana na hali hiyo kuna haja ya kutajuta mlingano wa pamoja wa kisheria itakayosaidia katika kudhibiti usafirishaji haramu wa nyara za Serikali yakiwemo meno ya Tembo.

Semina hiyo inawashirikisha Maafisa kutoka idara mbalimbali za Serikali Kuu na SMZ wakiwemo Maafisa wa maliasili, Jeshi la Polisi, Mahakimu, Waendesha Mashitaka na TAKUKURU.

Wengine ni Usalama wa Taifa, KMKM, Shirika la Polisi wa Kimataifa Interpol, Bandari, Shirika la Meli Zanzibar, Viwanja vya Ndege na Kitengo cha Kuzuia Madawa ya Kulevya hapa nchini.

No comments: