Tangazo

October 19, 2012

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Sefue azungumzia Sekta ya Gesi Asilia Nchini

Meneja wa Sekta ya Kupunguza Umaskini na Kusimamia Maendeleo Ukanda wa Afrika wa Benki ya Dunia, Dkt Albert Zeufack, akiongea wakati wa mkutano na wanahabari Ikulu jijini Dar es salaam leo kuhusu sekta ya Gesi asilia nchini, akiwa ameongozana na mabalozi wa nchi kadhaa pamoja na Timu ya wataalam walioletwa na washirika wa maendeleo na  inayowakilisha Benki ya Maendeleo ya Afrika, Benki ya Dunia, Shirika la Fedha la Kimataifa, Jumuiya ya Nchi za Ulaya na Nchi za China, Uingereza na Ujerumani.

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akiongea wakati wa mkutano na wanahabari Ikulu jijini Dar es salaam leo kuhusu sekta ya Gesi asilia nchini. Nyuma yake mwenye laptop ni Meneja wa Sekta Kupunguza Umaskini na Kusimamia Maendeleo ukanda wa Afrika wa Benki ya Dunia Dkt Albert Zeufack.

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akitoa ufafanuzi kwa baadhi ya waandishi wa habari baada ya mkutano na wanahabari Ikulu jijini Dar leo.
 **************************** 
Katika miaka ya karibuni kumekuwepo kwa ugunduzi mkubwa wa gesi asili nchini Tanzania katika maeneo ya mwambao na maeneo ya kina kirefu cha bahari ambapo mpaka sasa jumla ya futi za ujazo trilioni 33 zimegunduliwa. Kazi ya utafutaji inaendelea na upo uwezekano wa ugunduzi zaidi.

Kiasi hicho kilichothibitika hadi sasa hakitoshi kutuingiza kwenye ligi ya wazalishaji gesi wakubwa duniani. Hata jirani zetu Msumbiji wanayo gesi asilia iliyothibitika nyingi zaidi kuliko sisi.

Lakini kiasi cha gesi asilia kilichothibitika katika nchi yetu kinatosha kutuwezesha kuwa wazalishaji muhimu wa gesi asilia, na tukijipanga vizuri na kuisimamia kwa umakini sekta hii ndogo, inaweza kutusaidia kuharakisha maendeleo.

Kinyume chake, tusipojipanga na kuisimamia vizuri tunaweza, kama nchi, tusipate faida kubwa. Mbaya zaidi ipo mifano ya kutosha ya nchi ambazo uvumbuzi wa gesi na mafuta umevuruga uchumi wao.

  Hivyo, kabla hatujaenda mbali ni muhimu kama taifa tuwe na uhakika wa tunachokitaka na tujijengee uwezo wa kufanya maamuzi sahihi ikiwemo kwenye kutunga sera, kuandaa mkakati na kutunga sheria itakayosimamia uendelezaji wa sekta ndogo ya gesi.

Katika kufanya hivyo, hatuna sababu ya kuvumbua upya gurudumu. Duniani upo uzoefu wa kutosha wa nchi ambazo hazikusimia vizuri sekta hii na kuharibiwa. Ipo pia mifano na uzoefu wa kutosha wa waliosimamia vizuri na kufanikiwa.

Sisi tunaoanza leo tuna fursa ya kuepuka makosa waliyofanya wengine na tuna fursa ya kuchukua uzoefu wa waliofanya vizuri. Lakini lazima tuchukue hatua sasa. Tukichelewa itakuwa vigumu kurekebisha makosa baadaye.

Serikali imepania tusifanye makosa na inaandaa utaratibu bora wa kusimamia uendelezaji wa sekta ndogo ya gesi asili. Tunataka kuhakikisha kunakuwepo uwajibikaji, uwazi na uongozi bora ili Taifa letu lipate mapato stahiki yatokanayo na uvunaji wa rasilimali hii, na mapato hayo yatumike vizuri kama msingi wa kujenga uchumi endelevu wa kisasa, utakaonufaisha wananchi wengi zaidi.

Mchakato wa kupata maoni ya wadau wote ndani ya nchi unaendelea, lakini pia tunahitaji uzoefu na ushauri kutoka kwingine duniani. Na ndio maana kwa karibu wiki moja sasa tumekuwa na ugeni wa Timu ya wataalam walioletwa na washirika wa maendeleo kutokana na maombi yetu. Timu hiyo inawakilisha Benki ya Maendeleo ya Afrika, Benki ya Dunia, Shirika la Fedha la Kimataifa, Jumuiya ya Nchi za Ulaya na Nchi za China, Uingereza na Ujerumani.

Tumekuwa na majadiliano kadhaa na Timu hii ambayo imekutana na wadau mbalimbali ikiwemo Serikali, taasisi za umma, makampuni ya utafutaji wa mafuta na gesi, sekta binafsi, asasi zisizo za kiserikali, wanazuoni, baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani na wenyeviti wa Kamati za Bunge.

Mikutano hii ililenga kuipa Timu hii mawazo na maoni wa wadau muhimu ndani ya Tanzania ili wayazingatie katika ushauri wao kwetu. Mazungumzo yote yalikwenda vizuri na yana manufaa makubwa.

Napenda kusisitiza mambo yafuatayo:-

(i) Timu hii tumeiomba sisi. Kama mnavyoona ina uwakilishi mpana wa Washirika wa Maendeleo. Hivyo, badala ya kujadiliana na mmoja mmoja tumepata fursa ya kuzungumza nao wote kwa pamoja.

(ii) Uamuzi wa mwisho kuhusu sera, mkakati na sheria zitakazotawala sekta hii, ni wetu kwa asilimia mia moja. Lakini katika kuamua tunataka tupate uzoefu wa wengine, ushauri wa kitaalam na taarifa zote muhimu za kutuwezesha kufanya maamuzi sahihi. Kwa mfano, tunachohitaji kutoka kwa Timu hii ni:-

(a)  Uzoefu wa nchi ambazo zimefanya vibaya katika kusimamia sekta zao za mafuta na gesi asilia. Lengo ni kuhakikisha hatufanyi makosa waliyofanya wengine.

(b)  Uzoefu wa nchi ambazo zimefanya vizuri katika kusimamia sekta hii. Lengo ni kuzingatia yale yote yaliyothibitika kwa wengine kuwa ni ya manufaa.

Mambo ya msingi kwa upande wa Serikali ni kuhakikisha:-

(a) Tunakuwa na mikataba bora inayolinda maslahi ya taifa lakini bila kukosa mvuto kwa wawekezaji. Hivyo tunahitaji kujenga uwezo mkubwa kwenye eneo hili.

(b) Tunahimiza wajasiriamali wetu wajiandae kutoa huduma kwa makampuni makubwa ya gesi ili kupata  manufaa zaidi kutokana na gesi.

(c) Tunaandaa watalaam na mafundi wanaoweza kuajiriwa na makampuni ya gesi.

(d) Tuna mfumo thabiti wa kusimamia matumizi ya mapato yakatakayotokana na gesi ili yasiyumbishe uchumi mkuu wa nchi bali yawe msingi wa uwekezaji katika kubadili mfumo wa uchumi wetu na maendeleo endelevu.

(e) Tuna mfumo thabiti na uwezo wa usimamizi na udhibiti.

Pamoja na hayo ni muhimu wananchi waelewe kuwa hatutakuwa matajiri mara moja. Hatutarajii mapato katika miaka michache ijayo. Isitoshe lazima tufikirie vizazi vijavyo. Sisi tulio hai leo ni wadhamini wa kile ambacho vizazi vijavyo vitarithi kutoka kwetu. Hivyo itabidi tufikiri vya kutosha na kuamua kiasi gani cha mapato tutakayopata kitumike leo na kiasi gani kitumike kujenga msingi wa maisha bora ya vizazi vijavyo hasa ikizingatiwa kuwa kuna siku gesi hiyo itakwisha.

Nawashukuru washirika wa maendeleo waliotoa wajumbe kushiriki kwenye timu hii. Pia nawashukuru wajumbe wenyewe kwa ushirikiano mzuri waliouonyesha wakati wa zoezi hili.

Aidha nawashukuru watanzania walioshiriki na kutoa maoni yao hata kufanikisha zoezi hili.

Kwa pamoja tuhakikishe Tanzania inakuwa mfano bora wa matumizi sahihi ya rasilimali hii kwa faida na maendeleo yetu na vizazi vijavyo.

No comments: