Tangazo

March 11, 2013

Mashindano ya Hisani ya Mbio za Mbuzi za Dar es Salaam 2013 kufanyika Juni Mosi

Kauli mbiu: ‘Mbuzi Mmoja tu Anaweza Kuleta Mabadiliko’         

MASHINDANO ya 13 ya Hisani ya Mbio maarufu za Mbuzi za Jiji la Dar es Salaam yatafanyika Juni 1 mwaka huu.

Tayari tukio hilo la kifamilia linalofanyika kila mwaka limeshafanikiwa kukusanya zaidi ya Shilingi milioni 660 kwa ajili ya zaidi ya vituo 60 vya kujitolea na mashirika ya kijamii tangu mbio za kwanza zilipofanyika mwaka 2001.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mbio Hizo, Karen Stanley alisema: “Mbuzi wako sokoni kwa sasa tayari kuuzwa kwa mtu yeyote (au timu) anayetamani kushiriki mashindano hayo na kuungana na wale wanaomiliki mbuzi mshindi.

“Mbali na mbuzi, siku hiyo ya mashindano huwa ni ya kuvutia sana. Tunadhani kwamba kwa kufanya mapema tukio hili mwaka huu kutatoa nafasi kwa watu wengi zaidi kujiunga nasi kufurahia siku hiyo na kuunga mkono juhudi zetu.

“Mwaka jana tuliweka rekodi ya kukusanya Shilingi milioni 115 kwa ajili ya mashirika 15. Mwaka huu tunatarajia kukusanya fedha nyingi zaidi.”

Watu 4,200 walifika kwenye mashindano hayo ya hisani ya aina yake mwaka jana na kuweka rekodi huku wakishuhudia mbuzi wakishindana kwenye njia maalumu, mashabiki wakishiriki michezo ya kubahatisha, wakashiriki kwenye mashindano ya kuvutia ya mavazi na wao na familia zao wakala aina mbalimbali za vyakula vya kienyeji kutoka kwa watayarishaji maarufu wa jijini hapa.

Mama Stanley alisema: “Mwaka huu tutakuwa na zawadi mpya za kuvutia kupitia droo maalumu, ikiwa ni pamoja na tiketi mbili za ‘business class’ kutoka Swiss Air. Kama ilivyo kauli mbiu ya mashindano ya mwaka huu isemayo ‘Viumbe wa Baharini na Mabaharia’ bila shaka italeta msisimko wa aina yake kwa wote watakaokuwapo na kuwahamasisha kuvaa mavazi na kushiriki kwenye shindano la mavazi na kisha vazi bora litazawadiwa.”

Watoto watakuwa na nafasi kubwa ya kufurahi kwa kutengewa eneo maalumu litakalokuwa na kila kitu kwa ajili yao, na wataingia bure eneo hilo mara baada ya kuingia uwanjani. Ni kawaida sasa kuwa kila mwaka kuna shughuli mbalimbali za watoto kama kupakwa rangi za usoni na hata mashindano ya mavazi.

“Eneo la michezo ya watoto mwaka huu litakuwa zaidi ya unavyofikiria. Kamati ya maandalizi inafanya juhudi kubwa ili mchana huo uwe wa kukumbukwa na wa kipekee kwa watoto,” alisema Mama Stanley.

Mbio za Mbuzi za Hisani za Dar huandaliwa na kamati ya watu wanaojitolea, lakini ni wazi mambo haya yasingeweza kufanikiwa bila ya kuwapo kwa wadhamini wengi, wanaojitolea fedha na utaalamu wao.

Mama Stanley alisema: “Mwaka huu kuna kundi kubwa la makampuni mapya yaliyojitolea kufanikisha shughuli hii. Ukarimu wa wadhamini ndio hutuwezesha kukusanya fedha nyingi kwa ajili ya watu wanaozihitaji hasa na wanastahili msaada wetu.

“Tusingefanikiwa bila wao, na hakika wao ndio wamiliki wa mashindano haya, ambapo kwa mwaka huu ni Southern Sun, Coca-Cola, Tanzanian Breweries Limited (TBL), Mantra Tanzania, Erolink, Benki ya FNB na Symbion.”

Kama unataka na wewe kuwa mmiliki wa mbio hizi, fuatilia kwenye mtandao wetu www.goatraces.com, au tuma barua pepe kwenda goatraces@goatraces.com.

Mbio za mwaka huu zitafanyika kuanzia saa sita mchana kwenye eneo la The Green, Kenyatta Drive. Tiketi ni Sh 5,000 na zitauzwa getini.

No comments: