Tangazo

March 14, 2013

Mjue Kiongozi mpya wa Kanisa Katoliki Duniani: Papa Francis I


Kardinali Jorge Bergoglio wa Argentina amechaguliwa kuongoza Kanisa Katoliki Duniani, akiwa ni wa kwanza kutoka barani Amerika na wa kwanza kutoka nje ya Ulaya kwa zaidi ya miaka 1,000.

Baada ya kuchaguliwa na makardinali wenzake 115, Kardinali Jorge Bergoglio (76) alichagua kufahamika kwa jina la Francis I.

Maelfu ya mahujaji, watalii na waumini wa Kanisa Katoliki waliokuwa wamejazana katika Viwanja vya Kanisa la Mtakatifu Petro, Vatican kushuhudia moshi mweupe uliofuka saa 4:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki kuashiria kuchaguliwa kwake, waliripuka kwa shangwe, nderemo na vifijo.

Muda mfupi baada ya moshi huo kutoka, kardinali mmoja alisimama katika ‘varanda’ ya Kanisa la Mtakatifu Petro na kutangaza “Habemus Papum” (tumepata papa mpya).
Papa Francis I alikuwa miongoni mwa waliokuwa wanawania nafasi hiyo na papa anayeondoka, Benedict XVI mwaka 2005, ambapo aliripotiwa kuibuka wa pili.

Kabla ya kuchaguliwa kwake, Papa Francis I ambaye kwa wadhifa wake pia anakwenda kuwa Askofu wa Roma, alikuwa Askofu Mkuu wa Jimbo la Buenos Aires, Argentine na kwa muda wote wa utumishi wa utumishi alikuwa huko huko nyumbani.

Anakuwa Papa wa 266 kuwahi kuongoza kanisa hilo lenye waumini zaidi ya bilioni 1.2 duniani.
Baada ya kutangazwa kwake, Papa Francis I alijitokeza kuzungumza  kwa mara ya kwanza kama Askofu wa Roma.

Akiwa amechaguliwa katika awamu ya tano ya upigaji kura, inaelezwa kuwa alikuwa miongoni mwa mapapa waliochaguliwa kwa haraka baada ya muda mrefu, akiwa sawa na Benedict XVI (2005) na Pius XII aliyechaguliwa mwaka 1939.

Mshindi alitakiwa kupata kuta 77 au robo tatu ya makardinali 115 walioshiriki uchaguzi huo.
Papa Francis I anachukua nafasi iliyoachwa na Papa Benedict XVI aliyejiuzulu Februari 28, mwaka huu, ikiwa  ni miaka 600 tangu Papa wa mwisho kujiuzulu.

Yeye ni nani

Papa Francis I, ni Papa wa kwanza kutoka Shirika la Jesuit ambaye ametumia muda wake mwingi wa utumishi nyumbani Argentina.

Anafahamika kwa utumishi uliotukuka kwa uangalizi wa kanisa na mapadri, mambo ambayo yanatajwa kuwa sifa kubwa ya kuchaguliwa kuwa Papa.

Papa huyo amedumu katika maisha ya kufundisha na kuongoza mapadri. Amefanya kazi Amerika ya Kusini ambako kuna Wakatoliki wengi. Kardinali Bergoglio anatambulika kwa kutamadunisha Kanisa la Argentina, lililokuwa miongoni mwa makanisa ya kihafidhina huko Amerika Kusini.

Amechagua jina la Papa Francis I, chini ya uangalizi wa Mtakatifu Francis wa Assisi.

Alizaliwa Buenos Aires katika familia ya mfanyakazi wa reli. Alipata upadrisho mwaka 1969.

Aprili 15, 2005, mwanasheria wa haki za binadamu alimfungulia mashtaka ya jinai  kwa kushirikiana na maofisa wa jeshi kuwateka mapadri wawili wa Jesuit mwaka 1976, akiwa kiongozi wao aliwafukuza katika utumishi kutokana na migogoro katika jumuiya hiyo.

Msemaji wake alikanusha vikali tuhuma hizo na hakuna uthibitisho uliotolewa kumhusisha na madai hayo.

Kauli yake ya kwanza

Baada ya kutangazwa kuwa Papa wa 266, Kardinali Jorge Bergoglio (76) aliwataka waumini wa Kanisa Katoliki duniani kumwombea.

Papa huyo aliyechagua jina la Francis I, alisema: “Kama mnavyofahamu, kazi ya mkutano wa uchaguzi ilikuwa ni kuchagua Askofu wa Roma,” Francis I  aliueleza umati uliokuwa unashangilia katika Viwanja vya Kanisa la Mtakatifu Petro, huku akiwapungia mikono.

“Ni mimi hapa. Ninadhani makardinali wenzangu wamenichagua mimi kutoka mbali...Niko hapa. Ninapenda kuwashukuru kwa kunipokea.”

Akiwa kardinali alipambana na Serikali ya Argentina chini ya Rais Cristina Fernandez de Kirchner kuhusu msimamo wake dhidi ya ndoa za mashoga na utoaji bure wa huduma za uzazi wa mpango, ambazo zimekuwa zikipingwa na Kanisa Katoliki duniani kote.

No comments: