Ujumbe wa ngazi za juu wa biashara kutoka Ujerumani uko ziarani katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 13 na 14 Machi, ili kutafiti fursa mpya za kibiashara, kufanya matayarisho kwa ajili ya uwekezaji zaidi wa nchi ya Ujerumani na kwa hali hiyo kuimarisha uhusiano wa karibu uliopo baina ya makampuni ya Kijerumani na yale ya Tanzania. Ujumbe huo unaongozwa na Mawaziri wa Nchi Anne Ruth Herkes (Wizara ya Uchumi na Teknolojia) na Bw. Harald Braun (Wizara ya Nchi za Nje).
Wakati wa ziara yao ujumbe huo wa wafanyabiashara ulipokelewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr. Mohammed Gharib Bilal, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, na Waziri wa Biashara na Viwanda, Dr. Abdallah Kigoda, kwa nia ya kuimarisha mahusiano ya kiuchumi yaliyopo baina ya nchi hizi mbili.
Baada ya kukutana na Makamu wa Rais, Waziri wa Nchi wa Ujerumani Harald Braun alidhihirisha wazi shauku kubwa: “Inaelekea ziara yetu imefanyika wakati muafaka. Ni msisitizo wa umuhimu uliofungamana na majadiliano ya kisiasa na mahusiano bora ya kibiashara na nchi ya Tanzania. Kutokana na misingi ya mahusiano haya thabiti yanayoendelea, tunapenda kuongeza vitega uchumi katika biashara na Tanzania. Uchumi wa Tanzania umeendelea kubaki katika kiwango chake cha ukuaji cha asilimia sita hadi saba katika muongo mmoja uliopita. Uwezo wa kiuchumi wa nchi ya Tanzania, wenye rasilimali za kiuchumi na, hususan kugunduliwa hivi karibuni kwa gesi asilia, ni mkubwa kabisa. Serikali ya Ujerumani inayasaidia kwa nguvu zote makampuni ya Kijerumani na Kitanzania katika kugundua fursa hizi kwa pamoja.”
Katika moyo huu, Hati ya Makubaliano ilisainiwa na Waziri wa Nishati na Madini, Dr. Muhongo, pamoja na Ujerumani ili kuimarisha pia utawala katika sekta ya gesi asilia. “Pamoja tutaisaidia Serikali ya Tanzania kutengeneza mfumo wa kisheria na uwezo ili kufanikisha mambo, ikiwa ni pamoja na ukuaji wa uchumi, maendeleo endelevu na kupunguza sana umaskini. Nchi ya Ujerumani inasaidia kwa dhati juhudi za nchi ya Tanzania kuwa nchi yenye mapato ya wastani.”
Makampuni ya Kijerumani yako tayari kuja nchini Tanzania na kuwekeza. Pamoja na Waziri wa Usafirishaji, Dr. Harrison Mwakyembe, Waziri wa Nchi Braun alizindua chumba cha maonesho cha kwanza kabisa cha kampuni kubwa kabisa ya Kijerumani ya utengenezaji magari ya VOLKSWAGEN nchini Tanzania. “Sherehe hizi za ufunguzi hivi leo ni ishara thabiti na zitafuatiwa na makampuni mengine ya Kijerumani!” alijinadi Waziri wa Nchi Braun.
Mawaziri hao wawili wa Nchi waliongozana na ujumbe mzito wa wafanyabiashara kutoka Ujerumani. “Ujumbe huu wa wafanyabiashara unaakisi uwezo wa kiuchumi wa makampuni ya Kijerumani,” alisisitiza Waziri wa Nchi Herkes. “Ujumbe huo unajumuisha makampuni makubwa yanayofahamika ulimwenguni, ikiwa ni pamoja na makampuni madogo madogo, ambayo yanaongoza katika masoko duniani katika maeneo yao ya utaalamu, na ni uti wa mgongo wa uchumi wa Ujerumani. Makampuni madogo na yale ya wastani hutengeneza ajira na huchangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji uchumi na mapato ya kodi. Makampuni hayo ni yenye ushindani wa hali ya juu na husafirisha bidhaa zao kwenda nchi zote duniani.
” Wakati wa mkutano na Waziri wa Biashara na Viwanda, Dr. Abdallah Kigoda, Waziri wa Nchi Herkes alimalizia kwa kusema:”Teknolojia ya ugunduzi mpya, ubia wa muda mrefu, mafunzo na uanagenzi, ikiwa ni pamoja na faida endelevu ni mambo muhimu katika mafanikio ya makampuni ya Kijerumani. Kupitia ubia na makampuni ya Kitanzania, tunahamisha maarifa kuja nchini Tanzania. Hii inamaanisha ajira mpya, hususan kwa kizazi kipya katika nchi hii.”
Mfano mzuri wa ubia baina ya Tanzania na Ujerumani ni kampuni yenye mafanikio ya Tanzania Portland Cement (TPCC), ambayo inaendeshwa na kundi la makampuni ya Heidelberg Cement. Waziri wa Nchi Herkes alishuhudia makabidhiano ya hati ya uwekezaji iliyotolewa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania kwa kampuni ya Tanzania Portland Cement.
Kampuni ya Heidelberg Cement imetangaza uwekezaji wa ziada wa hadi kiasi cha Pesa za Euro milioni 25, sawa na Shilingi bilioni 52.5 katika kiwanda chake kilichopo Wazo Hill, nje kidogo ya Jiji la Dar Es Salaam. Ujumbe huo wa wafanyabiashara pia ulipewa maelezo mafupi kuhusu Mradi wa Mabasi yaendayo kasi Jijini Dar Es Salaam, DART, unaotekelezwa na kampuni ya ujenzi ya Kijerumani ya STRABAG, ambayo imekuwa ikifanya shughuli zake nchini Tanzania kwa miaka mingi.
Biashara baina ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na nchi ya Ujerumani inaendelea kukua, na hivi sasa imefikia kiasi cha jumla ya Pesa za Euro milionni 315, sawa na Shilingi bilioni 661.5. Tanzania na ukanda mzima wa Afrika Mashariki inazidi kuwa shabaha ya vitega uchumi vya makampuni ya Kijerumani.
Ushirikiano wa maendeleo baina ya Tanzania na Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani ulianza zamani za miaka ya 60.
No comments:
Post a Comment