Tangazo

July 17, 2013

Makamu wa Rais aiwakilisha Tanzania katika mkutano wa Umoja wa Afrika, Abuja

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal (pichani), ameiwakilisha Tanzania katika mkutano wa Umoja wa Afrika nchini Nigeria, mkutano uliokuwa na agenda ya kukabiliana na magonjwa ya Ukimwi, Malaria na Kifua Kikuu. 

Mkutano huo unaamini kuwa suala la magonjwa si la nchi moja na namna ya kuyadhibiti inahitaji ushirikiano wa nchi mbalimbali. Kwa sasa hoja hii inatolewa Afrika ili kuhakikisha Bara hili linamudu kukabiliana na magonjwa hayo na kuyadhibiti ili watu wake waweze kuwa imara na wapate uwezo wa kumudu maisha yao.

Katika mkutano huo, Mheshimiwa Makamu wa Rais alifafanua kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa tangu miaka 10 iliyopita ambapo azimio la kukabiliana na magonjwa hayo lilipitishwa jijini Abuja nchini Nigeria na kwamba kwa sasa Tanzania inaungana na nchi za Afrika kukubaliana na ukweli kuwa magonjwa haya yanaathiri wananchi wengi na pia ili kukabiliana nayo inahitajika nguvu ya pamoja kwa nchi zote duniani.

Mheshimiwa Makamu wa Rais alitumia mfano wa Zanzibar kama eneo ambalo limefanikiwa kudhibiti ugonjwa Malaria, lakini akafafanua pia kuwa ugonjwa huo unarudi kutokana na maingilianao ya watu wanaotoka maeneo mengine ambao wana ugonjwa huo. “Ili Kudhibiti kabisa maambukizi mapya lazima nchi zote zikubali kuwa magonjwa haya yanaambukiza na ili kumudu kuyakabili lazima kuwe na jitihada za pamoja kwa nchi zote,” Mheshimiwa Makamu Wa Rais alisema.

Kuhusu ugonjwa wa Ukimwi Mheshimiwa Makamu wa Rais aliieleza Afrika kuwa Tanzania ni nchi ambayo imepiga hatua katika kukabiliana na ugonjwa huo ambapo kwa sasa idadi ya vituo vya upimaji na utoaji nasaha cvimeonghezeka huku poia idadi ya watu wanaopata huduma hizo kuzidi maradufu ukilinganisha na miaka ya nyuma. 

Pia wananchi wa Tanzania wameongeza uelewa kuhusu ugonjwa huo na pia wamefikia hatua kubwa ya kuhakikisha kuwa wanafanya vipimo kabla ya ndoa sambamba na kuhakikisha akina mama wajawazito walio na maambuki wanapata tiba ili kuweka watoto wao salama. Tena mheshimiwa Makamu wa Rais alifafanua kuwa Tanzania ina uwezo wa kuwahudumia wagonjwa wa Ukimwi kwa kuwapatia dawa licha ya kuwa upo umuhimu wa wachangiaji wa huduma za maendeleo kuzidi kuisaidia Tanzania katika jukumu hili kwa kuwa gharama za dawa hizo ni kubwa.

Kuhusu ugonjwa wa Kifua Kikuu, Tanzania imepiga hatua kubwa kukabiliana na ugonjwa huo na sasa wagonjwa kifua kikuu wanapata tiba kirahisi tofauti na ilivyokuwa siku za nyuma. Kwa mujibu wa Makamu wa Rais, Tanzania itafikia malengo ambayo Umoja wa Afrika imejiwekea katika kukabilaiana na Ugonjwa huu licha ya kwamba changamoto kubwa za Kifua Kikuu zinatokana na ukweli kuwa, ugonjwa huu unachangiwa na magonjwa maengine kama Ukimwi.

Katika mkutano huo, viongozi mbalimbali wakiwakilishwa na mwenyeji  Rais Goodluck Jonathan walifafanua kuhusu hali katika nchi zao na wakakubaliana kwa kauli moja kuwa, Azimio la Abuja kuhusu kukabiliana na magonjwa hayo lifanyiwe kazi huku vyombo mbalimbali vinavyohusika katika kusaidia nchi duniani, vikionesha nia ya dhati kwa kuzitaka nchi kuchangia katika mapambano dhidi ya magonjwa hayo.

Tanzania inakabiliana kwa dhati kuhakikisha kuwa akina mama wanajifungua salama na pia watoto wanaozaliwa hawaambukizwi na magonjwa kama Ukimwi na lengo kuu ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2015, Tanzania inakuwa imemudu kuwafikia wagonjwa  milioni moja na laki tano wanaoishi na virusi vya ukimwi kwa kuwaptia dawa za kurefusha maisha.  Katika mkutano huo, Mheshimiwa Makamu wa Rais katikla ujumbe wake [pia alifuatana na Naobu Waziri Wa Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje. Tayari Ujumbe wa Mheshimiwa Makamu wa Rais umerejea nyumbani kukabiliana na majukumu mengine ya Kitaifa.

Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais
Abuja, Nigeria

No comments: