Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki |
Na Eleuteri Mangi- MAELEZO
JUMLA ya miradi 26 yenye thamani ya takribani Sh. bilioni 23.2 za Kitanzania iliyopo katika wilaya za mkoa wa Dar es Salaam, inatarajiwa kuzinduliwa, kufunguliwa na kuwekewa mawe ya msingi wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru.
Hayo yalisemwa leo na Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Said Meck Sadiki wakati akiupokea mwenge huo wa kutoka kwa Mkuu wa mkoa wa Pwani na Skauti Mkuu wa Chama cha Skauti Tanzania Hajati Mwantumu Mahiza katika hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika kwenye Uwanja wa Ndege wa Terminal 1 wa mkoa huo.
“Mkoa wa Dar es Salaam umepokea Mwenge wa Uhuru ukiwa salama, unawaka na wakimbiza mwenge wote sita wakiwa na afya nzuri na salama” alisema Sadiki.
Msafara wa mbio za mwenge kitaifa mwaka huu uliokabidhiwa kwa mkuu wa mkoa wa Dar es salaam unaongozwa na Juma Alli Simai.
Wengine ni Zamda John, kutoka Tanga, Christopher Emmanuel kutoka Kigoma, Separatu Sipulinga kutoka Iringa, Luteni Zuena Abdallah kutoka Kusini Unguja na Mgeni S. Mgeni kutoka Kusini Pemba.
Mkuu huyo wa mkoa alisema mwenge huo, utakuwa wilaya ya Kinondoni, ikifuatiwa na Ilala na hatimaye Temeke.
Mwenge ukiwa Kinondoni utafungua na kuweka mawe ya msingi katika miradi sita yenye thamani zaidi ya Sh. bilioni 2.8, Ilala miradi tisa yenye thamani ya Sh.bilioni 1.3 na Temeke miradi 11 yenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 19.
Kwa upande wake Kiongozi wa msafara wa mwenge, Simai alisema mwenge huo unania njema kwa taifa letu ikizingatiwa kila unapopita umekuwa na mafanikio ya kuzindua, kufungua na kuweka mawe ya msingi katika sekta mbalimbali ikwemo elimu, afya, mifugo na mali asili.
Simai alifafanua kuwa ni vema kuwajengea uwezo vijana ili Tanzania isonge mbele kimaendeleo ikiwa na umoja na ushirikiano.
Kwa upande wake Hajati Mwantumu alisema kuwa mwenge huo ni nuru na utaendelea kuwa nuru inayomulika nchi nzima na kuleta matumini, amani na upendo miongoni mwa Watanzania.
Ujumbe wa Mwenge wa Uhuru mwaka huu ni mahususi kwa lengo la kuleta umoja na mshikamano unaoongozwa na Kauli mbiu inayosema “Watanzania ni wa moja tusigawanyike kwa misingi ya tofauti zetu za dini , itikadi, rangi na rasilimali.”
No comments:
Post a Comment