Tangazo

September 4, 2013

SUMA JKT GUARD YATOA UFAFANUZI KUHUSU KULIPA FEDHA ZA NSSF KWA WAFANYAKAZI WAKE

Na Anna Nkinda – Maelezo

Shirika la Kujenga Taifa (SUMA JK) Guard Ltd imekanusha taarifa zilizoandikwa na gazeti la Dira ya Mtanzania toleo no. 250 la tarehe 2 mwezi huu kwamba SUMA JKT ndani ya kashfa kubwa na kueleza kuwa maafisa wa kitengo hicho wamekuwa wakiwakata fedha za Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) wafanyakazi wake na kutozipeleka  katika mfuko huo na hivyo kuishia mikononi mwa wajanja wachache.

Akitoa ufafanuzi kuhusiana na tuhuma hizo  jana katika ofisi za kitengo cha SUMA JK Guard wakati wa kikao baina ya Kaimu Mhariri wa gazeti hilo, Maafisa wa JKT na waandishi wa habari Mkurugenzi wa kitengo hicho Meja Batram Mgimba alisema kuwa wamekuwa  wakipeleka kila mwezi NSSF makato ya watumishi wake.

Alisema kuwa mwajiri kupeleka mchango wa NSSF kwa wafanyakazi wake ni agizo la Serikali na akishindwa  kufanya hivyo anapewa adhabu kubwa  hivyo basi wao kila mwezi wanapeleka makato hayo ya wafanyakazi wa itengo hicho ambao ni walinzi na mkataba wao wa kazi sio wa kudumu ni wa miezi mitatu mitatu na  alionyesha nakala za risiti za malipo hayo.

 “Mwaka  2011 tulianza kuchangia shilingi milioni nne katika mfuko wa NSSF huku tukiwa na walinzi  saba , tulikuwa na madeni  lakini tuliweza kuyalipa yote hivi sasa tuna wafanyakazi zaidi ya 1000 na kwa mwara ya mwisho tulichangia tarehe 30 Agosti  mwaka huu ambapo tulilipa zaidi ya shilingi milioni 25”, alisema Meja Mgimba.

Alisema kuwa hata kama mfanyakazi hana akaunti NSSF wao wanapeleka makato yake baadaye akijaza fomu na kuwa na akaunti hela yake itawekwa katika akaunti ya muhusika.

Meja Mgimba alisema ofisi zao ziko wazi na aliwaomba  waandishi wa habari pale wanapopata taarifa zozote waende  na kuwaona wahusika ili wapate taarifa sahihi  zitakazowaelimisha wananchi na siyo kupata taarifa kutoka kwa watu wasiohusika ambao zinaweza kupotosha na kuchafua utendaji kazi wa watu.

Kwa upande wake Kaimu mhariri wa gazeti hilo Jimmy Kiango alikiri kuwa habari hiyo ilikuwa na upungufu na haikuwa na maadili ya kitaaluma ya uandishi wa habari  na kuahidi kuifanyia marekebisho katika toleo lijalo.

No comments: