Tangazo

January 13, 2014

Mabinti wadogo watolewa mahari na kuolewa Nkasi

Nkasi, Rukwa.

KILA kabila nchini Tanzania lina mila na desturi zake. Baadhi ya mila na desturi hizi zimekuwa zikienziwa vizazi na vizazi kwa baadhi ya makabila huku nyingine zikipigwa vita kutokana na kukiuka ama haki za kibinadamu na pengine kuonekana hatarishi na zimepitwa na wakati. Ukitembelea jamii za makabila anuai utalibaini hili.

Kimsingi nakubaliana na utaratibu wa kuendelea kuzipiga vita kwa nguvu zote baadhi ya mila hizi, ikiwemo hii ya jamii ya wafugaji wa kisukuma ambao wao hadi leo bado wanaozesha mabinti wadogo hata ambao hawajitambui.
Mtoto mdogo wa kike jamii ya wafugaji wa kisukuma baadhi ya vijiji wilayani Nkasi anaolewa tena kwa mahari na mume asiyemjua. Mazungumzo hufanyika kati ya wazazi wenyewe na kukubaliana mahari kisha kukabidhiana na binti kuchukuliwa akiwa mdogo hivyo hivyo.

Bi. Scholastica Milambo (40) ni mkazi wa Kijiji cha Lunyala wilayani Nkasi, ikiwa ni miongoni mwa vijiji vilivyozungukwa na familia za wafugaji toka makabila ya kisukuma. Anasema katika kijiji hicho jamii za wasukuma wao ni jambo la kawaida kuwaozesha mabinti wao wakiwa kingali watoto.

Anasema wakati mwingine mabinti hao huolewa na wazee kabila bila ya wao kujua, kwa kuwa hulipiwa mali na kuchukuliwa wakiwa wadogo hata hawajitambui. Kinachofanyika ni wazazi wa familia ya muoaji au muoaji mwenyewe kuzungumza na wazazi wa binti kwamba wamempenda binti yake na kisha kupangiwa mahari (idadi ya ng’ombe).

Anasema baada ya hapo waoaji uleta ng’ombe kwa familia ya binti kama walivyopangiwa na kumchukua binti huyo, hata kama ni mtoto wa miaka 7 au chini ya hapo. Bi. Magreth Nkana (32) anasema wasukuma hawa jamii ya kifugaji huweza kuilipia mahari hata mimba (yaani mtoto akiwa tumboni) kwa makubaliano.

“…Hawa watu mila zao ni za ajabu sana maana muoaji anaweza kuzungumza na familia (ya mzazi mjamzito) na kukubaliana kuwa akizaa binti basi atakuwa ni mke wa mtoa mahari, na hii hufanyika hasa familia inapokuwa inazaa mabinti weupe…,” anasema Bi. Nkana akizungumza na mwandishi wa makala haya.    

Anasema wanapooa binti mdogo; muoaji humchukua binti huyo na kwenda kumuhifadhi kwa mama yake mzazi. Pale atakaa pamoja na watoto wengine wa mama wa muoaji hadi anapotimiza miaka 15 ndipo kijana hupewa na kuanza kumchombeza (kuishi naye kinyumba). Jamii hii ya wasukuma wafugaji haioni kabisa umuhimu wa kumwacha binti huyu asome shule.

Naye Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Lunyala, Edger Nkoswe anasema matukio ya jamii ya wafugaji kuoza wa toto ni kitu cha kawaida kwao. Anasema ni vigumu kuyadhibiti wao kwa kuwa wapo mbali na vijiji yaani pembezoni (mashambani).

Hata hivyo anasema wao huyafanya kwa siri kati ya familia ya muoaji na muolewaji jambo ambalo mtu wan je ni vigumu kubaini. “…Utakuta binti huyo mdogo akisha olewa mume amchukui moja kwa moja na kwenda kuishi naye, humpeleka kwa mama yake mzazi na kusubiri hadi anapovunja ungo na kuwenza kuingiliwa, ndipo mwenye mke hubeba na kuanza kuishi naye kama mke,” anasema Mtendaji wa Kijiji cha Lunyala.

“…Ni kweli huku kwetu wasukuma wanaoa watoto wadogo, wakati mwingine wanaweza kuchumbia binti akiwa na miaka 12 na anapolipa mahari humchukua na kwenda kumuweka kwa mama yake mzazi na anapotimiza miaka 15 na 16 humchukua na kuanza kuishi naye, jamii hii haina mpango na shule kabisa hata ukiangalia wanapoishi ni mbali sana (porini) na huduma za kijamii,” anasema Nkoswe.

Oscar Mdenye ni Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, katika mazungumzo na mwandishi wa makala haya anakiri uwepo wa ndoa za utotoni kwa jamii hiyo na wenyeji wenyewe. Anabainisha kuwa tatizo la ndoa za utotoni lipo kwa kiasi kikubwa na si kwa jamii za wafugaji pekee, lakini hata kwa wenyeji hapa (wafipa) wanafanya vitendo hivyo.

“…Unajua ndoa katika umri mdogo zipo na matukio ni mengi yanafanywa na kuungwa mkono na jamii inayowazunguka, kwa maana nyingine sehemu kubwa vijijini wanafanya vitendo hivyo…wakati mwingine unashindwa nani wa kumuwajibisha kwa kuwa kila mmoja anafanya. Unakuta mtoto kaoa mtoto,  wamezaa mtoto na wote wanalia…,” anasema Mdenye.

Anasema Ofisi ya Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na Dawati la Jinsia na Watoto wamekuwa wakijitahidi kutoa elimu juu ya madhara ya ndoa katika umri mdogo pamoja na haki za watoto ili jamii ibadilike na kuzingatia sheria za nchi, japokuwa bado ni changamoto.

“…Tunajitahidi kuelimisha jamii kupitia mikutano, matamasha ya pamoja na nafasi nyingine tunapozipata, tumezunguka na kuelimisha sana juu ya haki za watoto ili kila mmoja azijue labda itakuwa rahisi kuwabainisha wanaozipuuza,” anasema.

Pamoja na hayo anasema bado kuna changamoto kubwa ya jamii kutoa taarifa pindi inapoona kuna ukiukwaji wa haki hizo. Anaongeza kuwa wengi hawaripoti matukio hayo kwenye vyombo vya sheria ili viweze kuchukua hatua.
Lakini pamoja na matukio hayo ya kuwanyima haki ya msingi ya kupata elimu mabinti hawa kwa kuolewa moja kwa moja wakiwa wadogo, bado vitendo vya uhalifu kwa watoto hawa vinafanyika pia hata kwa wale waliopo shuleni.

Wapo wanaowafuata mabinti hawa shuleni na kuwarubuni na hatimaye kuwakatiza masomo yao kwa kuwatia mimba. Ofisa Elimu Msingi, Wilaya ya Nkasi, Bw. Misana Kwangura akizungumzia matukio ya mimba kwa ujumla kwa wanafunzi eneo hilo, anasema japokuwa matukio hayo bado yanaendelea lakini kwa sasa yameanza kupungua.

Anabainisha kuwa hiyo ni kutokana na matukio hayo kupungua kwa sasa ukilinganisha na hapo awali. Anatolea mfano tangu mwezi Januari hadi Novemba 2013 jumla ya wanafunzi 9 wametiwa ujauzito na kukatizwa masomo yao, idadi ambayo ni ndogo ukilinganisha na mwaka 2012 ambapo wanafunzi 11 walitiwa mimba.

 Aidha aliongeza kuwa kwa mwaka 2011 jumla ya wanafunzi 16 wa shule za msingi walitiwa mimba na kukatizwa masomo yao.  “…Kimsingi naweza kusema matukio haya kwa sasa yanapungua ukilinganisha na hapo nyuma, na hii inatokana na elimu ambayo tunaitoa kwa kuzunguka kwenye shule mbalimbali kwa kutumia ofisi ya Ofisa Elimu Sayansi Kimu,” anasema Kwangura.

Kwa upande wake Msimamizi wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Nkasi, Cpl- Anna Kisimba anasema  matukio ya ukatili kwa watoto ikiwemo kuozeshwa yamekuwa yakiripotiwa kwenye dawati hilo na kuyafanyia kazi ikiwemo kuwafikisha watuhumiwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

Anatolea mfano kwa mwaka 2013 hadi mwezi Desemba jumla ya matukio hayo 25 yaliripotiwa kwenye Dawati la Jinsia na watoto na utekelezaji wake upo katika hatua mbalimbali. Anasema kwa matukio ambayo upelelezi wake ulikamilika wameyafikisha mahakamani ili kutoa mwanya sheria kuchukua mkondo wake kwa wahusika.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com kwa ushirikiano na TAMWA.

No comments: