Marehemu Dk. William Mgimwa |
MWILI wa Waziri wa Fedha na Uchumi, William Mgimwa (63)
aliyefariki dunia juzi nchini Afrika Kusini baada ya kuugua kwa muda mrefu
unatarajiwa kuwasili nchini kesho.
Akitangaza ratiba ya kuwasili kwa mwili na maziko ya
Waziri Mgimwa kwa waandishi wa habari jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisema shughuli zote zitafanywa na
serikali.
Lukuvi alisema tayari serikali imeshaunda kamati mbili, moja ipo
jijini Dar es Salaam, ina wajumbe kutoka Ikulu, Wizara ya Fedha na Uchumi,
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa ambayo itaongozwa na yeye.
Alisema kamati ya pili imeundwa mkoani Iringa ambayo
itashughulikia namna ya kuuhifadhi mwili wa marehemu Mgimwa kijijini
kwake Magunga, ambayo itaongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Christine Ishengoma.
Lukuvi alisema mwili wa Mgimwa utawasili kwa ndege ya
Shirika la Ndege la Afrika Kusini, majira ya saa saba mchana katika
Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere (Terminal II) na kupelekwa nyumbani
kwake Mikocheni B, na itakapofika majira ya saa 11 jioni utapelekwa katika
Hospitali ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Lugalo jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti huyo alisema siku ya Jumapili, mwili wa Mgimwa
utawasili nyumbani kwake majira ya saa 5:30, kisha utapelekwa katika Ukumbi wa
Karimjee kwa ajili ya ibada, heshima za mwisho na salamu za rambirambi hadi saa
nane mchana.
Alisema mara baada ya tukio hilo, mwili wa Mgimwa utapelekwa
katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (Teminal I) kwa
ajili ya kusafirishwa kwenda Iringa ambapo unatarajiwa kufika majira ya saa 10
jioni ili kuwapa fursa wananchi wa mkoa huo kuuaga katika Ukumbi wa Siasa ni
Kilimo.
Lukuvi alisema mara baada ya wananchi wa Iringa mjini kuaga,
jioni hiyo hiyo mwili wa Mgimwa utapelekwa kijijini kwake Magunga kwa ajili ya
kupumzishwa kesho yake (Jumatatu).
“Shughuli za kuwasili na hatimaye maziko zinafanywa na serikali
kupitia kamati kuu na ile ya Mkoa wa Iringa, ambayo itapata mwongozo kutoka
huko chini ya Dk. Ishengoma,” alisisitiza Lukuvi.
Akizungumza kwa masikitiko namna alivyomfahamu marehemu Mgimwa,
Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Saada Salum, alisema amejifunza mengi kuhusu
uongozi mara baada ya kuanza kufanya naye kazi walipoteuliwa na Rais Jakaya
Kikwete, Mei mwaka jana.
“Kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu niliofanya kazi na Dk.
Mgimwa, nimejifunza mengi katika uongozi. Kwani kazi kwake lilikuwa jambo
la kwanza, kwa maana wakati mwingine alikuwa akikaa ofisini hadi saa 5 usiku,
si hivyo tu bali hata siku za Jumamosi na Jumapili alikuwa akifanya kazi,”
alisema.
Saada alisema alichojifunza kwake zaidi ni kwamba kama mtu
anapewa dhamana ya uongozi anapaswa kuitimiza bila kuchoka na kulalamika.
Naibu waziri huyo ambaye hakutaka kusema ugonjwa uliosababisha
mauti yake, alisema mara ya mwisho aliwasiliana na marehemu Mgimwa kwa
simu mwezi mmoja uliopita na katika mazungumzo yao alimweleza kuwa anaendelea
vizuri.
Katika hatua nyingine, Chama Cha Mapinduzi
(CCM) Wilaya ya Iringa Vijijini na Mkoa wa
Iringa, kimesema kimepata pigo kwa kifo cha
aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kalenga, William Mgimwa.
Wakati serikali ya Mkoa wa Iringa
ikiendelea na maandalizi ya mazishi ya Waziri Mgimwa, Mkuu wa
Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma amesitisha
likizo yake iliyoanza hivi karibuni kutokana na msiba
huo mkubwa kwa Mkoa wa Iringa na Tanzania kwa ujumla.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi jana
kwa nyakati tofauti mjini hapa, viongozi wa CCM wa
wilaya na mkoa pamoja na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Gerald
Guninita, walisema kifo cha Waziri Mgimwa si pigo tu
kwa familia yake bali pia kwa taifa kwa ujumla.
Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa
Iringa, Jesca Msambatavangu, alisema kuwa CCM mkoani
hapa imepata pigo kubwa kwa kumpoteza
mbunge huyo na waziri na kuwa katika uhai wake
Mgimwa alikuwa mbunge wa tofauti na wengine na
kuwa siku zote hakuwa mbunge wa kujisikia kwa
nafasi yake.
Kwani alisema mbali ya kuwatumikia vema
wakazi wa Jimbo la Kalenga na Watanzania katika nafasi yake
ya uwaziri wa Fedha na Uchumi, bado Mgimwa
alikuwa kiongozi wa kushirikiana vema na chama na
wananchi wake.
Alisema Mkoa wa Iringa umepata
pigo kubwa juu ya kifo hicho na kuwa Chama Cha
Mapinduzi kitaendelea kuenzi mchango wake katika
kuyafanya yale yote ambayo katika uhai
wake alikuwa akiyapigania na siku zote katika ndoto
zake za kuwatumikia wananchi wa Jimbo la Kalenga.
“Tunaamini kila mtu ambaye amepata kufanya
kazi na Dk. Mgimwa anatambua wazi kuwa alikuwa ni
mchapa kazi na kiongozi mpenda watu…Dk.
Mgimwa mbali ya kuwa waziri hakuwa na majivuno
na alikuwa ni kiongozi wa misaada hata katika majukumu yasiyo
rasmi katika nafasi yake…kweli sina cha kusema
zaidi ya kuendelea na maandalizi ya mazishi yake,” alisema Msambatavangu.
Delophina Mwimbile Mtafilalo ni Mwenyekiti wa CCM wa
Wilaya ya Iringa Vijijini, alisema bado
viongozi wa CCM wa wilaya hiyo hawaamini kama Waziri Mgimwa amefariki
dunia kwani tangu alipolazwa hawakupata nafasi ya kumjulia hali.
“Kweli tumepata pigo sana kwa kifo chake
hadi sasa umetukuta tumesimama hapa nje tusijue la
kufanya na hatujui sisi kama viongozi wa Jimbo la
Kalenga ni nani ataziba pengo lake la ubunge,” alisema
Delophina.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Gerald Guninita,
ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kilolo alisema kifo cha
Mgimwa kimepokewa kwa majonzi makubwa.
Mgimwa alifariki dunia juzi nchini Afrika Kusini alikokuwa
amelazwa kwa matibabu.
No comments:
Post a Comment