Tangazo

March 22, 2014

KIKWETE ‘AVURUGA’ MJADALA

 . AONYESHA HISIA ZAKE ZA KUTAKA KATIBA YA SERIKALI MBILI

. WANAOTAKA SERIKALI TATU WAMSUBIRI YEYE AONDOKE MADARAKANI


RAIS Jakaya Kikwete jana alibadili upepo wa mchakato mzima wa Katiba baada ya kutoa maoni yake binafsi, akitaka muundo wa Serikali mbili badala ya tatu zilizopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Akizungumza katika ufunguzi wa Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma, Rais Kikwete alipangua hoja moja baada ya nyingine zilizotolewa na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba wakati akiwasilisha Rasimu ya Katiba bungeni Machi 18, mwaka huu.


Katika hotuba yake hiyo ya saa 2:49 iliyokuwa na maneno ya ‘kuuma na kupuliza’ kuhusu yaliyomo katika Rasimu ya Katiba, Rais Kikwete alisema suala la muundo wa Muungano ndiyo ajenda mama katika Rasimu ya Katiba na kwamba iwapo wajumbe watatoa uamuzi usio sahihi, nchi inaweza kujaa migogoro ambayo haikuwapo.

Huku akishangiliwa na wajumbe wa Bunge hilo, Kikwete alisema kuwa wanaotaka Serikali tatu waangalie changamoto zake na kuzitafutia majibu, kwa maelezo kuwa muundo huo unaweza kuvunjika kirahisi.

Alisema ingawa Jaji Warioba aliwatoa hofu wananchi kuwa Serikali tatu hazitakuwa na gharama kubwa, ukweli ni kwamba muundo huo una gharama na utekelezaji wake ni mgumu na kusisitiza kuwa CCM inaweza kuzimaliza kero za Muungano bila kuhitaji uwapo wa Serikali ya tatu.

Huku akichambua kile kilichoelezwa na Jaji Warioba sambamba na kuwapiga vijembe wenyeviti wa vyama vya upinzani akiwamo Christopher Mtikila (DP) na Freeman Mbowe (Chadema), Rais Kikwete alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba imetoa sababu mbili kubwa za kupendekeza muundo wa Serikali tatu;

“Sababu ya kwanza ni kwamba muundo huo ndiyo matakwa ya Watanzania wengi Bara na Zanzibar. Sababu ya pili muundo huo unatoa majibu ya uhakika na endelevu kwa changamoto za muundo wa sasa wa Serikali mbili zinazolalamikiwa na pande zote mbili.”

Aliongeza, “Wapo wanaokubaliana na tume na kwamba muundo wa Serikali tatu ni matakwa ya wengi na hauepukiki na kwa msemo wa Kiswahili wengi wape. Lakini wapo wanaopingana na takwimu za tume kwamba hazionyeshi ukweli huo.

Mimi nasema maneno yanayosemwa na watu siyo yangu.” Huku akishangiliwa na wajumbe wa Bunge hilo alisema, “Watu wanasema Watanzania waliotoa maoni kwa tume ni 351,664, kati yao 47,820 sawa na asilimia 13.6 ndiyo waliokerwa na muundo wa Muungano. Watu 303,844 sawa na asilimia 86.4 hawakuwa na tatizo na muundo wa Muungano na wala hawakuuzungumzia wakati wa kutoa maoni.”

Alisema hivi sasa watu wanahoji iweje asilimia 13.6 ndiyo wageuke Watanzania walio wengi ambao wametoa maoni ya kutaka Serikali tatu.

“Watu wanahoji mbona taarifa ya tume inayohusu takwimu (ukurasa 66,67), inaonyesha kati ya watu 47,820 waliotoa maoni kuhusu muungano watu 17,280 ndiyo waliotaka Serikali tatu ambao ni sawa na asilimia 37.2 na waliotaka muundo wa Serikali mbili ni asilimia 29.8, Serikali ya mkataba asilimia 25.3 na Serikali moja asilimia 7.7” alisema.

 Alisema taarifa ya tume inaonyesha kuwa watu 772,211 waliotoa maoni ni asilimia 10.4 ndiyo yaliyozungumzia muundo wa Muungano na asilimia 88.6 hawakuzungumzia Muungano, bali mambo mengine.

“Watu wanahoji kama Muungano ni jambo linalowakera sana Watanzania ingethibitika kwenye wingi wa wale waliotoa hoja. Usahihi wa hoja hii ni upi, nawaachie nyie (wajumbe) mjadili” alisema huku akishangiliwa kwa nguvu.

Akizungumzia sababu ya pili ya tume kwamba muundo wa Serikali tatu unajibu changamoto za muundo wa Serikali mbili, huku akifafanua kero zinazotolewa na kila upande wa Muungano alisema; “Nyinyi ndiyo waamuzi, sikilizeni vizuri hoja hizi mtafakari na kuamua. Tume yenyewe imekiri kuwa muundo wa Serikali wa Serikali tatu una changamoto zake ikiwa ni pamoja na gharama kubwa za uendeshaji wa shughuli za umma.”
Source: Gazeti la Mwananchi

No comments: