Tangazo

March 22, 2014

PANGANI FM REDIO YAPONGEZWA KWA KUKUZA KISWAHILI

IMAG0466
Mzee Bakari (mwenye shati ya bluu) wa Kijiji cha Madanga wilaya ya Pangani, akipongeza Kituo cha Redio cha Pangani FM kuendeleza Kiswahili kupitia kipindi cha Lugha ya Kiswahili.

Na. Mwandishi wetu,

Kikundi cha Wazee cha MWEHU katika kijiji cha Madanga wilayani Pangani kimeipongeza redio ya Pangani FM kwa kueleza Kiswahili kupitia kipindi kinachorushwa hewani na kituo hicho.

Wakichangia majadiliano ya kikundi kufuatilia usikivu wa vipindi vya kituo hicho, zoezi linalofanywa kwa pamoja na Redio Pangani FM kwa kushirkiana na Shirika la Kimataifa la UNESCO, wazee hao wamesema wanafurahishwa sana na kipindi cha LUGHA YA KISWAHILI kinachorushwa hewani kila Alhamisi jioni na kurudiwa Jumamosi mchana.

“Kile kipindi cha Kiswahili kinanikosha sana kwa sababu Kiswahili kinachozungumzwa na vijana wa sasa sio Kiswahili kizuri kwa mfano ‘kasheshe, mkwara’… tofauti na Kiswahili tulichosoma cha Hekaya za Abunuwasi kinapendeza sana. Nakipenda kipindi cha Kiswahili kiendelee sana kwa sababu kinaendeleza utashi wa lugha ya taifa”, alisema mzee aliyejitaja kwa jina moja la Mzee Bakari.

Wamesema Kiswahili kinachozungumzwa hivi sasa na kizazi kipya kinapotosha kwa kuingiza na kuondoa baadhi ya maneno, matamshi mabaya kiasi kwamba kinaondoa maana nzima ya kukuza Kiswahili na kuienzi kama lugha ya taifa.
IMAG0463
Mzee Mwehu (koti la suti) wa kikundi cha wazee cha MWEHU kijiji cha Madanga, Pangani akitoa mapendekezo yake ya kuanzishwa kipindi cha wazee chenye lengo la kuibua matatizo yanayowasibu.

Pamoja na kukisifu kipindi cha Kiswahili, wazee hao pia wamempongeza mtayarishaji wa kipindi hicho kwa kusema kwamba yuko makini na umahiri mkubwa katika utayarishaji na utangazaji wake.

Vipindi vingine visivyosifiwa ni pamoja na kipindi cha Urithi wa Pangani, Muziki, Michezo na Taarifa ya Habari.

Zoezi la ufuatiliaji na tathmini ni miongoni mwa utekelezaji wa mradi wa kuzipa uwezo Redio 9 za Jamii za kutumia TEHAMA kutayarisha vipindi vya afya, kilimo na elimu ili kutoa taarifa ya maeneo hayo kwa urahisi na wingi, unaotekelezwa na UNESCO kwa msaada wa Shirika la Maendeleo la Sweden (SIDA).

Hata hivyo wazee hao wamependekeza kuanzishwa kwa kipindi cha wazee jambo ambalo wanasema kuonekana kusahaulika kwa kuwa wana urithi wa mambo mengi yenye busara ambayo ni hazina kwa maendeleo ya wanajamii wa Pangani.

“Mimi masikitiko yangu ni kutokosekana kwa kipindi cha wazee. Tuna matatizo yetu mengi yanayotusibu lakini hakuna pa kuyasemea. Kwa mfano tuna tatizo la maji hapa, tumefuatilia kwa viongozi lakini tunazungushwa tu.

Laiti tungeyazungumza haya kupitia kipindi chetu, tungefikisha ujumbe”, alisema mzee maarufu kwa jina la MWEHU.
IMAG0470
Mzee Hadhrina Hatibu Msiagi wa kijiji cha Madanga akizungumza na Mtangazaji wa Pangani FM, Bi. Maajabu Ali kuhusu umuhimu wa kuwa na msemaji mahiri wa historia za kale za Pangani wakati wa zoezi la ufuatiliaji na tathmini lilioendeshwa kwa pamoja na Redio Pangani na UNESCO hivi karibuni.

Kwa upande wa kipindi cha Urithi wa Pangani, wamependekeza kuboreshwa kwa kipindi hicho kwa kumtafuta msemaji anayeijua kwa kina historia ya kale ya Pangani kinyume cha ilivyo sasa.

Wamesema Pangani ina utajiri wa historia ya kale lakini anayekiendesha kuzungumzia historia ya kale ya jana hivyo kuwanyima wanajamii haki ya kujua na ukweli wa chimbuko lao.

“Kuna mambo mengi ya kale ya Pangani, lakini siyo yanayozungumzwa, yanayozungumzwa ni ya jana kwa hiyo tunataka wapatikane watu wazee wanaozijua habari hizo”, alisema Mzee Hadhrina Hatibu Msiagi.

Kijiji cha Madanga ni miongoni mwa vijiji kongwe vya kwanza kuanzishwa ndani ya wilaya ya Pangani, kilichoanzishwa karne ya 17. Vijiji vingine ni Mwera, Pangani na Bushiri.
SAM_0015
Kikundi cha Wazee cha MWEHU wakiwa katika picha ya pamoja na wanaoendesha zoezi la ufuatiliaji na tathmini ya vipindi vya Pangani FM kijijini Madanga.

No comments: