Mama Salma Kikwete |
Na Anna Nkinda – Maelezo
Wanawake wajasiriamali nchini wametakiwa kutengeneza
bidhaa ambazo zinahitajika kwa wingi na watumiaji na kuacha kung’ang’ania
kutengeneza bidhaa ambazo soko lake ni dogo.
Mwito huo umetolewa na Mwenyekiti wa
Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) Mama Salma Kikwete wakati wa uzinduzi
wa umoja wa vikundi vya kuweka na kukopa Mbagala (UWAMBA) vilivyo chini
ya WAMA uliofanyika katika Ukumbi wa Dar Live jijini Dar es Salaam.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mke wa Rais Jakaya
Mrisho Kikwete alisema changamoto kubwa inayowakabili wajasiriamali wengi ni
upatikanaji wa soko la bidhaa zao lakini kama wataamua kubadilika na kutengeneza
bidhaa ambazo zinahitajika kutapunguza kwa kiasi kikubwa tatizo hilo.
“Ni jambo jema kujifunza kutengeneza bidhaa mbalimbali
, lakini kama utaona bidhaa uliyojifunza haina soko unaweza kutengeneza bidhaa
nyingine ambayo watu wengi wanaihitaji jambo la muhimu ni kuwa makini katika
umaliziaji wa kutengeneza bidhaa nzuri na zinazovutia”, alisema Mama Kikwete.
Akizungumzia kuhusu umuhimu wa vikundi hivyo kwa jamii
Mwenyekiti huyo wa WAMA alisema vikundi hivyo vinatoa mafunzo ya kuweka akiba
na kukopa kwa namna ambayo inamsaidia mwanakikundi kujenga tabia ya kujichunga
katika matumizi ya pesa na hivyo kuwa na mawazo ya kuweka akiba mara kwa mara.
Aidha Mama Kikwete pia aliwataka wanawake hao
kujitokeza kwa wingi kugombea na kushiriki katika chaguzi mbalimbali
zinazokuja ili wapate nafasi ya kutoa maamuzi.
Mwenyekiti wa WAMA alisema , “Mkipendana, kushirikiana
na kusaidiana mtafika mbali, ondoeni tofauti zenu na kila mmoja asimame
na kuweza kumtetea mwenzake, muwe na marafiki wanaopenda maendeleo na kama
mwenzako akifanya vizuri usiache kumsifia”.
Akisoma risala ya UWAMBA Halima Abrahman ambaye ni
katibu wa kikundi cha Faraja kilichopo Tandika alisema umoja huo wenye vikundi
11 huku wanachama wake wengi wakiwa ni wanawake na wachache ni wanaume
ulianzishwa mwaka 2013 wakiwa wanachangia hisa moja kwa shilingi 2000 kwa sasa
wana akiba ya zaidi ya shilingi milioni 15.
“Mbali na hisa mapato ya kikundi chetu yanapatikana
kutokana na wanachama kufanya biashara mbalimbali zikiwemo za utengenezaji wa
sabuni za maji, batiki, mishumaa, vikapu, mifuko ya karatasi, siagi za karanga,
kusuka mikeka, unga wa muhogo na achali”, Halima alisema.
Alizitaja changamoto zinazokikabili kikundi hicho
kuwa ni pamoja na ufinyu wa bajeti, ukosefu wa ofisi na vifaa vya
kuhifadhi taarifa za chama, kushindwa kushiriki katika mafunzo na ukosefu wa
masoko ya bidhaa zao.
Ili kukabiliana na changomoto zinavyovikabili vikundi
hivyo Mama Kikwete aliwakabidhi vyerehani vinne ambavyo vitatumika kuanzisha
mradi wa kushona nguo ambao utawaongezea kipato na Kompyuta moja kwa ajili ya
kuweka kumbukumbu zao.
Vikundi vinavyosimamiwa na Taasisi ya WAMA vimetokana
mradi wa majaribio wa MWANAMKE MWEZESHE ambao ulianza mwaka 2011 uliolenga
kuanzisha mfumo wa vikundi ambavyo vitaweza kutoa fursa za mikopo,
mafunzo na kujenga uwezo wa wanachama kujiendesha wenyewe na kuanzisha miradi
ambayo itawaongezea kipato.
Mradi huo wa majaribio ulifanikiwa na kuweza kuwafikia
watu zaidi ya 1200 kwa kata zilizopo katika maeneo ya Majohe, Gongo la Mboto,
Mbagala , Manzese, Temeke na Tandika. Ambapo jumla ya akiba ya zaidi ya milioni
200 zimekusanywa na mikopo ya shilingi milioni 265 imeweza kufikia vikundi
mwaka 2013.
Pia mradi huo umeweza kuunganisha vikundi na kuvipatia
fursa za kiuchumi na kijamii kwa kutoa mafunzo na semina mbalimbali za
wanavikundi ikiwa ni pamoja na mafunzo ya usindikaji, kuwaunganisha na huduma
ya bima ya afya na ushiriki wa maonyesho ya biashara kwa ajili ya kutangaza
bidhaa zao.
No comments:
Post a Comment