Waziri Migiro akiongea na baadhi ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo. |
Na
Mwandishi Wetu
Serikali
imeanza kusambaza nakala milioni mbili za Katiba Inayopendekezwa nchini kote
ili kuwawezesha wananchi kuisoma na kushiriki katika Kura ya Maoni iliyopangwa
kufanyika tarehe 30 Aprili mwaka huu.
Waziri
wa Katiba na Sheria Dkt. Asha-Rose Migiro amesema leo (Jumatano, Februari 11,
2015) jijini Dar es Salaam kuwa kati ya nakala hizo zilizochapwa jijini Dar es
Salaam, nakala 1,800,000 zinasambazwa Tanzania bara na nakala 200,000 zinasambazwa
Tanzania Zanzibar.
Kwa
mujibu wa Waziri Migiro, hadi kufikia jana (Jumanne, Februari 10, 2015), jumla
ya nakala 707,140 zilikuwa zimesambazwa katika mikoa 12 ya Tanzania Bara na
Tanzania Zanzibar ambayo imepata nakala 200,000 na kuwa kazi hiyo inaendelea
vizuri na inatarajiwa kukamilika katika muda mfupi ujao.
Mikoa
hiyo na nakala ziliozosambazwa katika mabano ni Katavi (15,640), Rukwa
(27,040), Ruvuma (47,740), Mbeya (78,640), Simiyu (34,840), Mara (52,540),
Tabora (58,540) na Kigoma (41,440). Mikoa mingine ni Kagera (54,340), Geita
(36,940), Mwanza (57,040) na Pwani ambapo usambazaji umeanza kwa wilaya ya
Mafia ambayo imepata nakala 2,400.
“Idadi
ya nakala ya Katiba Inayopendekezwa kwa kila mkoa inategemea na wingi wa kata
katika mkoa, ndiyo maana baadhi ya mikoa unaona imepata nakala nyingi,” amesema
Dkt. Migiro ofisini kwake wakati akiongea na baadhi ya waandishi wa Habari
waliotaka ufafanuzi kuhusu hatua iliyofikiwa katika kazi ya uchapishaji na
uasambazaji wa nakala za Katiba Inayopendekezwa.
Kwa
mujibu wa Waziri Migiro, kuna zaidi kata 3,800 nchini kote na lengo la Serikali
ni kusambaza nakala 300 katika kila kata ambazo zitasambazwa kwenye vijiji,
vitongoji na mitaa kupitia Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi wa
Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji.
Kuhusu
taasisi za elimu na dini, Waziri Migiro amesema Serikali imepanga kusambaza
nakala 658,400 kwa taasisi za elimu, dini, vyama vya siasa na asasi za kiraia
na kuwa usambazaji huo utaanza hivi karibuni.
Pamoja
na usambazaji huo, Waziri Migiro amewakumbusha wananchi ambao bado hawajapata
nakala za Katiba Inayopendekezwa, kuisoma kupitia tovuti ya Wizara ya Katiba na
Sheria (www.sheria.go.tz) na tovuti ya
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (www.agctz.go.tz).
No comments:
Post a Comment