TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe.
Bernard Membe, amesema leo kuwa hakuna Mtanzania kati ya watu wanane waliouwawa
katika mashambulizi dhidi ya wageni huko Durban na Johannesburg nchini Afrika
ya Kusini. Mhe. Membe amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa
taarifa zilizosambazwa na baadhi ya vyombo vya habari kwamba Watanzania watatu
wameuwawa katika mashambulizii hayo siyo za kweli.
"Nimehakikishiwa na Waziri wa Usalama wa Afrika kusini,
David Mahlobo, asubuhi hii kuwa hakuna Mtanzania kati ya watu wanane
waliouwawa, ambao ni raia wa Ethiopia, Zimbabwe, Malawi na Swaziland,"
ametaarifu Mhe. Waziri. Amesema serikali ina taarifa kuwa kuna Watanzania
watatu waliofariki dunia nchini Afrika Kusini, lakini hawakuuwawa katika
mashambulizi ya wenyeji dhidi ya wageni.
"Watanzania hao ni Rashidi Jumanne, ambaye imetaarifiwa
alipigwa risasi katika tukio la ujambazi, kilometa 90 nje ya mji wa Durban;
mfungwa Athumani China Mapepe, aliyeripotiwa kuchomwa kisu gerezani wakati wa
vurugu za wafungwa, na Ali Heshima Mohamed, ambaye alifariki hospitalini
kutokana na ugonjwa wa TB," alieleza Mhe. Membe. Mwili wa marehemu Mohamed
ulirejeshwa nchini jana kwa mazishi.
Mhe. Waziri alitaarifu kuwa kuna Watanzania 23 katika kambi
iliyotayarishwa na serikali ya Afrika Kusini huko Durban kuhudumia wageni
wanaokimbia mashambulizi hayo ya wenyeji, na kuwa utaratibu unafanywa
kuwarejesha nyumbani raia 21 walioomba. "Wawili wamesema hawako tayari
kurudi." Mhe. Membe amesema taarifa ya serikali ya Afrika Kusini
inaonyesha kuwa hali ya utulivu imerejea Durban na Johannesburg katika saa 48
zilizopita kutokana na juhudi za Rais Jacob Zuma na kamati maalum ya mawaziri
aliyoiteua kushughulikia mashambulizi hayo.
Mapema jana, Mhe. Membe alimwita Balozi wa Afrika Kusini
nchini Tanzania, Mhe. Thamsanqa Dennis Mseleku, na kuelezea kukerwa kwa
serikali na mauaji ya wageni na akataka hatua madhubuti zichukuliwe kuhakikisha
usalama wa Watanzania nchini Afrika Kusini Alisema Tanzania inaunga mkono
taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika
(SADC), Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, ambayo imelaani vikali mashambulizi ya
Waafrika kutoka nje ya Afrika Kusini. Hata hivyo, Rais Mugabe, ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), amesifia hatua zinazochukuliwa na serikali
ya Afrika Kusini kukomesha mashambulizi hayo na kurejesha utulivu.
Mhe. Membe aliwataka Watanzania waishio Afrika Kusini na
kwingineko nje ya nchi, kujitambulisha kwenye balozi zetu ili iwe rahisi
kufuatilia usalama wao na kuwasaidia pale yatokeapo majanga. "Hatuna
takwimu sahihi za idadi ya Watanzania waishio Afrika kusini kwa sababu wengi
wao wamekwenda huko kwa njia za panya," alisema. Inakadiriwa kuna
Watanzania 10,000 waishio Johannesburg na Durban.
Akijibu swali la mwandishi wa habari, Mhe. Membe alisema
Tanzania inapaswa kutumia utajiri mkubwa wa gesi asilia ilionao ili kuendeleza
viwanda vidogo, vya kati na vikubwa vitakavyotengeneza ajira za kuvutia kwa
vijana ili wasikimbilie nchi za nje na kuhatarisha maisha yao.
Imetolewa na: Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Dar es Salaam
20 April 2015
20 April 2015
Copy and WIN : http://ow.ly/KNICZ
No comments:
Post a Comment