Tangazo

April 25, 2015

TEMBO KUTOWEKA TANZANIA MIAKA 10 IJAYO - NYALANDU

DSC_0089
Pichani juu na chini ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Mh. Lazaro Nyalandu akizungumza na katika mkutano uliohusisha wadau wa mashirika ya Kimataifa na asasi za kijamii ukiwa na lengo la ushirikishaji wa jamii katika masuala ya uhifadhi wa wanyamapori uliofanyika jana katika ukumbi wa mikutano wa Mpingo House uliopo Wizara ya Maliasili na Utalii jijini Dar es Salaam.(Picha zote na Zainul Mzige wa Modewji blog).

Na Modewji blog team

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu amesema kama watanzania wasiposhirikiana katika kudhibiti ujangili wa Tembo waliopo watatoweka kabisa katika kipindi cha miaka 10 ijayo.
Kauli hiyo ameitoa jana kwenye mkutano wa ushirikishwaji wa jamii katika masuala ya uhifadhi wa wanyamapori uliofanyika wizarani kwake.

“Uhifadhi kama tunavyoujua, hautaweza kufanikiwa kama kila mtu kwenye nchi hii atafikiria ni kazi ya serikali kuu peke yake.

Na vilevile kama kila mtu atafikiria ni kazi ya wahifadhi peke yao”. alisema Nyalandu kwenye mkutano huo.

Nyalandu alibainisha kuwa, majadiliano hayo, yatakuwa chachu kubwa ya maendeleo katika wizara hiyo huku akiwashukuru wadau hao mbalimbali wakiwemo wanahabari kwa kufika kwao, ili kuangalia suala la uhifadhi kwa mapana yake.

Alisema wakati ujangili wa Tembo nchini umeshamiri sana, wakati umefika kwa watanzania kuhakikisha kwamba wanakomesha hali hiyo ili taifa kuendelea kuwa na wanyama wake.

Alisema mathalani Tembo katika hifadhi ya Selous wamepungua kutoka Tembo 38,975 katika sensa ya mwaka 2009 hadi Tembo 1,384 kwa sensa ya mwaka 2014 na akasema kwa kasi hiyo katika miaka 10 ijayo Tembo Tanzania wataisha kabisa.

“Hili ni muhimu watu wakafahamu, upana wa hivi vita ni mkubwa kiasi gani na watu wanaohusika ni wengi kiasi gani ndani na nje ya nchi," alisema Nyalandu akiongeza kuwa mitandao ya kihalifu imetanda ulimwenguni kote.

Alisema suala la hifadhi halipo kwa wanyama pekee bali lipo katika upana wote na hata katika misitu.

Alisema ili kukabiliana na ukatwaji hovyo wa miti kutoka katika misitu ya miombo wanajipanga kuhakikisha kwamba miombo inayodaiwa kuingizwa nchini kutoka Zambia inakamatwa ili kulinda miombo iliyopo magharibi ya nchi.

Akizungumzia suala la mifugo na mbuga zinazopakana nazo amesema kwamba wanaanda rasimu ya kuhakikisha kwamba kuna mahusiano mazuri kati ya wenye mifugo na hifadhi wakiwa tayari kuyaachia baadhi ya maeneo kwa lengo la kuhakikisha kwamba wafugaji hawaingizi mifugo yao katika hifadhi.

Aidha amesema kwamba wanajipanga namna ya kuhakikisha kwamba hakuna mgongano wa maeneo kati ya wanyama na binadamu na kwamba wanavijiji wanafundishwa namna ya kuishi na wanyama katika maeneo yenye mwingiliano mkubwa.

Aidha alisema kwamba meno ya Tembo kilo 1,763 yalikamatwa mwaka jana na jitihada zinaendelea za kukabiliana na majangili kwa kutanua mtandao wa kiintelejensia ndani na nje.
Alisema kwa sasa wanamsaka raia wa China anayeshutumiwa kutorosha nyara za serikali kwa kushirikiana na jeshi la Polisi la Kimataifa (Interpol).

Kwa nje ya nchi, meno ya Tembo yaliyokamatwa, Kilo 40 katika miji ya Hong Kong, China.

Aidha alisema watuhumiwa 1,711, walikamatwa kuanzia Januari hadi Desemba mwaka jana na kesi zao zinaendelea katika mahakama mbalimbali hapa nchini. Pia silaha 85 zimekamatwa ikiwemo silaha za kivita ambazo walikuwa wakizitumia mbugani.

Alisema ukichanganya na silaha zilizokamatwa kwenye operesheni tokomeza, jumla silaha 1,199 zimekamatwa.

Kwa upande wake, Ali Said Mosee aliyehudhuria mkutano huo kutoka Tanzania Association on Climate Change, alishauri ushirikishaji wa wadau mbalimbali kutatua migogoro kwenye mipaka ya mbuga na pia mgongano wa kimaslahi kati ya hifadhi na wanadamu.

Aidha wadau walishauri Wizara kuhakikisha inapunguza misafara ya wanyama ya kuhamahama kutoka sehemu moja hadi nyingine ikiwemo kwa kuzalisha miti na mazao yanayopendwa na wanyama hao.

“Wanyama wetu wanatakiwa wafanyiwe utafiti na kujua nini Nyati anapendelea kula porini, basi wapande hiyo miti na vyakula vyake kwa ujumla hata kwa Tembo hivyo hivyo.Wapande hiyo miti hapa hapa kwani hata siye binadamu tunavyovyakula tunavyovipenda, naamini hata kwa wanyama ni hivyo hivyo, rai yangu ni kuwa tufanye utafiti na kujua ili kuzuia misafara hii” alisema Ali Said Mosee.

Tanzania inahifadhi za taifa 16 na asilimia 40 ya ardhi ya nchi ni maeneo yaliyohifadhiwa. Kati ya maeneo hayo yaliyohifadhiwa hadi mwezi uliopita mwaka huu 2015, maeneo 19 yanamilikiwa na wananchi na yameshasajiliwa. Pia alisema kwamba kuna mapori ya akiba, 28 nchi nzima.

“Watu wengi wanadhani kwamba misitu yote inamilikiwa na serikali kuu. Ukweli ni kwamba serikali kuu inamiliki asilimia 35 tu ya misitu ya nchi yetu, misitu mingine yote inamilikiwa na vijiji, wilaya na watu binafsi asilimia 7. " alibainisha waziri huyo.

Aliwataka watendaji wa Serikali za mitaa kukabiliana na changamoto ya kutoweka kwa kasi kwa misitu ili taifa lisitumbukie katika jangwa.
 
DSC_0082
DSC_0096
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mh. Lazaro Nyalandu akifafanua mazungumzo na wadau wa mashirika ya kimataifa na asasi za kijamii ukiwa na lengo la ushirikishaji wa jamii katika masuala ya uhifadhi wa wanyamapori uliofanyika jana katika ukumbi wa mikutano wa Mpingo House uliopo Wizara ya Maliasili na Utalii jijini Dar es Salaam.
DSC_0135
Naibu Waziri wa Maliaisli na Utalii, Mahmoud Mgimwa akitoa salamu kwa wadau wa taasisi za kirai. Kushoto Waziri wa Maliasili na Utalii, Mh. Lazaro Nyalandu.
DSC_0124
Mratibu wa Uhakiki wa Ubora kutoka Haki Elimu, Robert Mihayo akitoa maoni kwa Waziri Mh. Nyalandu ambapo amemuomba kushirikisha wadau wa elimu katika kutoa elimu ya uhifadhi wa wanyamapori kuanzia ngazi ya elimu ya msingi ili kuwaanda vijana ambao ni taifa la kesho.
DSC_0110
Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Civil Society, Francis Kiwanga akishiriki kutoa maoni katika masuala ya uhifadhi wa wanyamapori pamoja na kutokemeza ujangili wa Tembo.
DSC_0105
Mwandishi wa gazeti la Daily News, Diriham Kimathi akiuliza swali kwa Waziri Nyalandu (hayupo pichani).
DSC_0129
Pichani juu na chini ni baadhi ya wadau kutoka asasi za kijamii na mashirika ya kimataifa waliohudhuria mkutano ulioitishwa na Waziri Nyalandu ambao umefanyika jana katika ukumbi wa mikutano wa Mpingo House uliopo ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
DSC_0131
DSC_0059
DSC_0005
DSC_0143   DSC_0149  
Waziri Nyalandu akisalimiana na baadhi ya wadau kutoka mashirika ya kimataifa na asasi za kijamii waliohudhuria mkutano huo.
  DSC_0158
Mdau kutoka Tanzania Association on Climate Change, Ali Said Mosee akitoa maoni yake juu ya kuhusiana na nini kifanyike katika masuala ya uhifadhi wa wanyamapori katika mkutano uliotishwa na Waziri Nyalandu (hayupo pichani).

No comments: