Beki wa
timu ya wasichana wa Temeke Eva Wailes, akiwatoka wachezaji wa Arusha wakati
timu hizo zilipokutana katika ufunguzi wa michuano ya Airtel Rising Stars
kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam jana. Temeke
walishinda magoli 8-0.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
*Mwanza
yaibamiza Kinondoni bao 1-0
Pazia la michuano Taifa ya soka ya vijana chini ya umri
wa miaka 17 ya Airtel Rising Stars jana lilifunguliwa katika uwanja wa Kukumbukumbu
ya Karume jijini Dar es Salaam ambapo timu ya wasichana
ya Temeke ilitoa onyo kali kwa timu shiriki kwa kuifunga Arusha 8-0.
Mchezo huo ulifuatiwa na mechi ya wavulana kati ya
Mwanza na Kinondoni na Mwanza kuibuka na ushindi wa goli 1-0. Goli la Mwanza
lilifungwa na Lazaro Richard katika dakika ya 42 kufuatia krosi iliyopigwa
kutoka upande wa kushoto.
Katika mchezo wa kwanza, Temeke walianza kwa kasi ya
aina yake na kupeleka mashambuliazi ya mara kwa mara langoni mwa Arusha huku
Arusha wakionekana kuzidiwa katika kila idara.
Temeke waliandika bao la kwanza kupitia kwa Oppah
Clement kaika dakika ya 24, baada ya kuwahadaa mabeki wa Arusha na kuachia
shuti kali ambalo lilimshinda kipa wa Arusha.
Temeke awalipata bao lao la pili kupitia kwa Rose Mpoma
mnamo dakika ya 27 ambaye aligongeana mpira kwa uzuri na Oppah Clement na kisha
kumchambua kipa wa Arusha kwa umaridadi wa hali ya juu na kuukwamisha mpira huo
kimiani.
Alikuwa ni Oppah Clement tena, ambaye aliiandikia
Temeka bao la tatu mnamo dakika ya 28 baada ya kuunganisha krosi iliyochongwa
na Shamimu Hamisi kutoka upande wa kushoto mwa uwanja na kuendeleza karamu ya
magoli kwa Temeke.
Shamimu Hamisi aliifungia Temeke bao la nne katika
dakika ya 51 na kuzidi kuzamisha jahazi la Arusha ambao walinekana kama vile
wamesimama wakati mchezo ukiendelea.
Rosea Mpoma aliwaliza kwa mara nyingine tena Arusha
baada ya kuifungia Temeke bao la tano katika dakika ya 53 baada ya kuachia
shuti kali na kuzama moja kwa moja wavuni.
Temeke waliendeleza kupeleka kilio kwa Arusha baada ya
Asia Juma kufunga goli la sita na la saba baada ya kuwatoka mabeki wa Arusha
kwa nyakati tofauti na kuwapa raha mshabiki wao.
Shamimu Hamisi alihitimisha karamu ya magoli kwa Temeke
baada ya kufunga bao la nane na kuamsha nderemo na vifijo kwa maelfu ya
mashabiki wao waliohudhura uwanjani hapa.
Baada ya mchezo huo, kocha wa Temeke Daudi Siang’a alisema kuwa walistahili kushinda kutokana na
kuwaandaa vijana wake kikamilifu kwa ajili ya mashindano haya, hivyo haoni kama
kuna timu ya kuwazuia msimu huu.
“Timu yangu ilicheza vizuri na ilistahili ushindi kwa
sababu kisaikolojia wachezajji wangu wako vizuri, lakini vile vile niliwapa
muda mrefu wa maandalizi yenye mbinu madhubuti, kwa ushindi wa leo kwetu si wa kubahatisha”,
alisema Siang’a.
Kwa upande wake, kocha wa Arusha Gefrey Mrope alisema
kuwa, hofu ya mashindano juu ya vijana wake ndio sababu kubwa ya kupoteza
mchezo wa leo kwa kuungwa idadi kubwa ya mabao lakini aliaahidi kufanya
marekebishao katika hilo.
“Kisaikolojia wachezaji wangu wengi ni wapya hivyo
hawana uzoefu wa kucheza katika kadamnasi kubwa ya watu kama hii, lakini
naahidi kulifanyia kazi jambo hilo ili katika mchezo ujao, tuweze kupata
ushindi”, alisema Mrope
No comments:
Post a Comment