Na Hamza Temba-Dar es Salaam
...................................................................................
SERIKALI kupitia wizara zake nne
tofauti imedhamiria kukabiliana na changamoto mbalimbali za utoaji wa huduma kwa
wageni wanaiongia na kutoka nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius K. Nyerere (JNIA) jijijini Dar es Salaam.
Changamoto hizo ni
pamoja na msongamano na joto katika eneo la kuchukulia mizigo, muda mrefu wa
upatikanaji wa hati za kusafiria kwa wageni wanaoingia nchini pamoja na
changamoto ya ufinyu wa eneo la kusubiri huduma uwanjani hapo.
Mawaziri wa Wizara hizo ambao wamefanya
ziara ya pamoja katika uwanja huo jana na kukagua shughuli za utoaji huduma ni Waziri
wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, Waziri wa Mambo ya Ndani,
Dk.Mwigulu Nchemba, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Dk.Susan Kolimba na Naibu
Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye.
Akizungumza uwanjani
hapo, Dk. Kigwangalla alisema wamefikia hatua ya kukutana mawaziri hao baada ya
wageni hasa watalii wanaiongia nchini kulalamika kuwa wanatumia muda mwingi
kuhudumiwa katika eneo la uwanja huo kiasi cha kuwapotezea muda.
Dk.Kigwangala amesema
kutokana na malalamiko hayo ya muda mrefu na mengine kadhaa hatua mbalimbali
zimechukuliwa tangu Agosti 8 mwaka 2017 manaibu waziri wa wizara hizo nne walipofanya
ziara uwanjani hapo kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi changamoto hizo na kwamba kukutana
kwao jana ni muelendezo wa kushughulikia kero hizo ambapo mafanikio yameanza
kuonekana.
Dk.Kigwangala amesema
ipo haja ya kuweka mikakati ya kuboresha huduma katika viwanja vya ndege nchini
ukiwamo JNIA huku akisisitiza umuhimu wa watendaji na watoa huduma katika
nafasi mbalimbali kuwa wakarimu kwa wageni.
Amesema ni vema hata
Polisi walioko uwanjani hapo wakimkamata mgeni basi badala ya kutumia nguvu
wawe na ukarimu kwani ni muhimu kumdhibiti mgeni bila kutumia nguvu ili
ikibainika hana kosa aachiwe na asiwe na malalamiko ya kunyanyaswa.
Dk.Kigwangala amesema
kuna haja kwa wageni wanapokuja Tanzania wakirudi makwao wasimulie ukarimu na
uzuri wa nchini yetu.
Ameongeza anatamani
kuona kuanzia uwanjani hapo hadi hotelini ambako mgeni anakwenda anatumia muda
mchache, anapata nafasi ya kuona picha za viongozi mbalimbali ambazo zitakuwa
uwanjani, picha za wanyama na video ambazo zinaonesha utalii wa Tanzania.
Amesema kumpokea mgeni
jambo moja lakini namna ya kumhudumia ni jambo jingine na ndilo muhimu zaidi na
akafafanua hata teksi ambayo mgeni ataitumia kusafiri dereva awe na ukarimu
hata wa kumsalimia na wakati mwingine kutabasamu.
Kwa upande wake, Waziri
wa Mambo ya ndani Ndani Dk. Mwigulu Nchemba akizungumza baada ya ziara hiyo alisema
jitihada mbalimbali zinafanywa kutatua changamoto hizo.
Ametaja hatua ambazo
wizara yake inachukua ni kuharakisha utoaji huduma wa hati za kusafiria kwa
njia ya kieletroniki.
Pia wameamua kuongeza
idadi ya madawati ya kutolea huduma kwa wageni ikiwa sambamba na kuongeza
watoaji huduma ili kurahisisha utoaji huduma wa muda mfupi.
“Taarifa zinaonesha
kuwa kwa sasa kuna unafuu mkubwa wa kutoa huduma kwani badala ya saa tatu
ambazo zilikuwa zinatumia awali hivi sasa muda wa utoaji huduma umeshuka hadi
saa moja, lengo letu ni kushuka zaidi.
“Mbali ya kuboresha
huduma tutahakikisha pia tunaongeza ulinzi na usalama katika viwanja vyetu
vyote nchini ili kudhibiti wageni wenye nia ovu na nchi yetu.
“Tunafahamu mataifa
mengi yameitikia mwito wa uwekezaji nchini hasa katika mikakati ya kufikia
Serikali ya Viwanda na uchumi wa kati.
“Hivyo wageni wanakuja
kwa nia njema ya kuwekeza lakini hatutaki wale wenye nia mbaya kutumia mwanya
huo.Hivyo tutaendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika viwanja vyetu,”amesema.
Kwa upande wa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Susan Kolimba amesema
wanaridhishwa na hatua ambazo zinachukuliwa katika kuondoa changamoto
zinazoelezwa kuwapo uwanjani hapo.
Amesema wizara yao
inatamani kuona idadi ya wageni inaongezeka zaidi na wakati huo huo wakifurahia
huduma ambazo wanazipata wakifika nchini kwetu. Alisema Wizara yake itaendelea
kuitangaza Tanzania na vitutio vyake ili idadi ya watalii iweze kuongezeka.
“Tumefanya ziara na
binafsi niseme tu nimeridhishwa na hatua ambazo zinachukuliwa katika kuondoa
changamoto hizo,”amesema Dk.Kolimba.
Naye, Naibu Waziri wa
Ujenzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye amesema wizara yao tayari
imechukua hatua mbalimbali za kuondoa changamoto zilizopo ikiwamo ya kufunga
viyoyozi (AC) kwa ajili ya kuondoa hali ya joto.
“AC zilizopo ni za
muda mrefu kwani ziliwekwa tangu majengo ya uwanja huo yalipojengwa. Hivyo
tayari zimeanza kufungwa AC mpya na ndio maana joto limepungua” amesema.
Pia amesema wamepata
kampuni ambayo itakayofanya ukarabati kwa kuongeza eneo la kukaa wageni
wanaosubiri huduma mbalimbali kabla ya kutoka uwanjani.
Amesema kuna jitihada
mbalimbali Serikali inafanya jitihada za kuondoa msongamano wa wageni ikiwamo
ya kuharakisha ujenzi wa jengo jipya la kusafiria wageni la Terminal III ambalo
litahudumia watu milioni sita badala ya jengo la sasa ambalo wakati
linajengwa lengo lake lilikuwa kuhudumia
watu milioni moja.
“Ujenzi wa jengo jipya
umekamilika kwa asilimia 70 na litakapokuwa tayari kwa asilimia 100 litaanza
kutumika kwa kuwa kasi ya ujenzi inakwenda vizuri,’amesema.
Waziri wa Maliasili na
Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla akiteta jambo na Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi Dk. Mwigulu Nchemba wakati wa ziara ya pamoja ya kukagua Changamoto
mbalimbali wanazokumbana nazo wageni hususan watalii wanaoingia nchini kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa
wa Dar es Salaam JNIA jana kwa ajili ya kukabiliana nazo.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi
Kigwangalla akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam jana wakati
wa ziara ya pamoja ya kukagua Changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wageni
hususan watalii wanaoingia nchini
kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam JNIA kwa ajili ya kukabiliana nazo. Wengine
walioshiriki ziara hiyo ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Mwigulu Nchemba (wa
pili kulia), Naibu Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye
(wa tatu kulia) na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Susan Kolimba (wa nne kulia).
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla (wa pili kulia) akiteta jambo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Susan Kolimba jijini Dar es salaam jana wakati wa ziara ya pamoja ya kukagua Changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wageni hususan watalii wanaoingia nchini kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam JNIA kwa ajili ya kukabiliana nazo. Wengine walioshiriki ziara hiyo ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Mwigulu Nchemba (wa tatu kushoto) na Naibu Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (wa pili kushoto) .
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla (wa tatu kulia) akiteta jambo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Susan Kolimba jijini Dar es salaam jana wakati wa ziara ya pamoja ya kukagua Changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wageni hususan watalii wanaoingia nchini kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam JNIA kwa ajili ya kukabiliana nazo. Wengine walioshiriki ziara hiyo ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Mwigulu Nchemba (kulia) na Naibu Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (wa pili kulia).
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Dkt. Susan Kolimba kulia akitoa maelezo kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dk. Mwigulu Nchemba kushoto, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Atashasta Nditiye (wa pili kushoto) na Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla (wa pili kulia) wakati wa ziara hiyo.
No comments:
Post a Comment