Tangazo

January 11, 2012

ICTR KUJIKITA ZAIDI KATIKA KESI ZA RUFAA 2012

Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) jijini Arusha.
Na Nicodemus Ikonko, Hirondelle, Arusha

 Baada ya kuhitimisha idadi kubwa ya kesi zake katika ngazi ya mahakama ya awali, mwaka 2012 Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) inatarajiwa kuelekeza nguvu zake kwenye kesi za rufaa.

Kwa mujibu wa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 1966 la Desemba 2010, ICTR haina budi kuhitimisha kesi zake katika ngazi ya usikilizwa na kutolewa hukumu ya awali ifikapo mwishoni mwa 2012 na kesi za rufaa kuhitimishwa ifikapo mwishoni mwa 2014.

Katika ngazi ya usikilizaji wa kesi, ni kesi moja tu dhidi ya Waziri wa zamani wa Mipango wa Rwanda, Augustin Ngirabatware ndiyo bado inaendelea kusikilizwa kwa upande wa utetezi. Lakini pia zipo kesi nyingine mbili zinazowahusu, aliyekuwa Waziri wa Vijana, Callixte Nzabonimana na afisa wa zamani wa jeshi la Rwanda, Idelphonse Nizeyimana zinasubiri kupangiwa tarehe ya kutolewa hukumu.

Idadi kubwa ya kesi za rufaa ni ngumu na zinahusisha kesi zinazowakabili watuhumiwa zaidi ya mmoja na zinawahusu waliokuwa vigogo nchini Rwanda
wakati wa mauaji ya kimbari mwaka 1994.

Kesi za rufaa zinazowahususu Meja Aloys Ntabakuze, Kapteni Ildephonse Hategekimana na mfanyabiashara Gasperd Kanyarukiga zilisikilizwa mwishoni mwa mwaka 2011 ambapo sasa majaji wanaendelea kujadiliana juu ya hoja zilizotolewa kabla ya kupanga tarehe ya kutolewa hukumu.Hata hivyo kesi nyimgine sita za rufaa bado zinasubiriwa kupangiwa tarehe za kusikikilizwa.

Kesi za rufaa zinazosubiri kusikilizwa ni kama zifuatazo:

Kesi ya maafisa wanne wa jeshi ijulikanayo kama Military II. Kesi hii inawahusu aliyekuwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Rwanda, Jenerali Augustin Bizimungu aliyehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela, Mnadhimu Mkuu wa jeshi la Polisi, Jenerali Augustin Ndindiliyimana alipewa adhabu ya muda aliokwishatumikia wakati alipokuwa kizuizini na hivyo kuachiwa huru na Meja Francois-Xavier Nzuwonemeye na Kapteni Innocent Sagahutu ambao kila mmoja wao alihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela.

Kesi ya Butare inayohusisha watu sita. Kesi hiyo inajumuisha aliyekuwa Waziri wa Familia na Masuala ya Wanawake ambaye ni mwanamke pekee kuwahi kushitakiwa na mahakama ya ICTR, Pauline Nyiramasuhuko na mtoto wake wa kiume Arsene Shalom Ntahobali. Wote wawili walihukumiwa vifungo vya maisha jela.Wengine katika kundi hili ni pamoja na meya wa zamani Elie Ndayambaje ambaye pia alihukumiwa kifungo cha maisha, meya mwingine Joseph Kanyabashi kapewa miaka 35, na wakuu wawili wa zamani wa mikoa, Alphonse Nteziryayo alihukumiwa kifungo cha miaka 30 na mwenzake Sylvain Nsabimana aliyepewa adhabu ya kifungo cha miaka 25.

Kesi ya mawaziri wanne ijulikanayo kama Government II. Mawaziri hao, Justine Mugenzi wa Biashara na Prosper Mugiraneza wa Utumishi wa Umma walihukumiwa vifungo vya miaka 30 jela kila mmoja wao na wamekata rufaa.Mawaziri wenzao wawili ambao waliachiwa huru ni pamoja na Casimir Bizimungu aliyekuwa Waziri wa Afya na Jerome Bicamumpaka wa Mambo ya Nje.Mwendesha Mashitaka ameamua kutokata rufaa.

Kesi ya vigogo wa MRND. Kesi hiyo inawahusu Rais wa chama tawala cha MRND nchini Rwanda mwaka 1994, Matthieu Ngirumpatse na makamu wake Edouard Karemera ambao wamehukumiwa vifungo vya maisha jela kwa kuhusika kwao katika mauaji hayo.

Kesi nyingine mbili za mtu mmoja mmoja nazo zinasubiri kusikilizwa katika ngazi ya rufaa. Kesi hizo zinawahusu afisa wa zamani wa jeshi la Rwanda, Luteni Jean-Baptiste Gatete aliyehukumiwa kifungo cha maisha jela na Meya Gregoire Ndahimana aliyehukumiwa kifungo cha miaka 15 jela.

No comments: