Tangazo

January 11, 2012

IKULU HAIHUSIKI NA UGAWAJI VITALU VYA UWINDAJI WA KITALII

Ikulu ya jijini Dar es Salaam
Gazeti la kila siku la Mtanzania la jana Jumanne, Januari 10, 2012 katika ukurasa wake wa kwanza limechapisha habari yenye kichwa cha habari “Ikulu Yazuliwa Jambo”.

Habari hiyo inayowakariri wafanyabiashara wasiotajwa majina mjini Dallas, Texas, Marekani, imedai kuwa Ikulu imeagiza kuwa makampuni kadhaa ya kigeni ambayo yalikosa mgawo katika ugawaji wa vitalu vya uwindaji wa kitalii warejeshewe vitalu vyao na kuwa barua za kuwarejeshea zitaanza kutolewa leo Jumatano, Januari 11, 2012.

Ikulu inapenda kuwajulisha wananchi kuwa habari hii siyo ya kweli. Ni habari ya uongo kwa sababu Ikulu haihusiki, haijahusishwa na haitahusika ama kuhusishwa na ugawaji wa vitalu vya uwindaji.

Kwa mujibu wa Kifungu 38 (11) cha Sura ya 283 ya Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 na Kanuni ya 9 (2) ya Kanuni za Uwindaji wa Kitalii za mwaka 2010,  kazi ya kugawa vitalu ni wajibu uliotolewa kisheria kwa Waziri wa Maliasili na Utalii. Yeye ndiyo uamuzi wa mwisho. Yeye hukaribisha maombi, yeyé hupokea maombi, yeye hutoa maamuzi wa nani apewe ama nani asipewe kitalu kwa mujibu wa sheria na kanuni za sheria husika.

Mwombaji aliyekosa kitalu asiporidhishwa na uamuzi wa Waziri anazo njia mbili za kufanya. Moja ni kutumia haki yake ya kuwasilisha rufani kwa Waziri wa Maliasili na Utalii ili kuomba maombi yake kupitiwa upya (Administrative Review) na njia ya pili kama hataridhika tena na uamuzi wa Waziri kufuatia maombi yake ya rufani basi anayo haki ya kukata rufani Mahakama Kuu.

Hakuna mahali popote ambako Ikulu ama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anahusika katika kutoa vitalu vya uwindaji. Na wala hakuna sababu ya Rais ama Ikulu kuhusishwa katika ugawaji vitalu. Kama tulivyoeleza hiyo ni kazi ya Waziri wa Maliasili na Utalii; inaanza na inaishia kwake, na Rais anazo shughuli nyingi za kutosha kuliko kujihusisha na kugawa wala kutoa vitalu vya uwindaji.

Ikulu inapenda kuwahakikishia wananchi kuwa hakutatokea mabadiliko yoyote katika Sheria hiyo na kanuni zake chini ya Rais huyu wa sasa. Hakuna barua yoyote itakayotolewa na Ikulu kugawa vitalu iwe ni kwa Jumatano ya leo ama Jumatano zote za mwaka huu wa 2012 ama za miaka minne ijayo ya uongozi wa Rais wa sasa.

Aidha, Ikulu inapenda kuwaomba wananchi kupuuza habari. Ni uongo na uzushi mtupu.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
10 Januari, 2012

No comments: