Tangazo

May 29, 2012

CUF yalaani Vitendo vya Uvunjifu wa Amani Zanzibar

                                                THE CIVIC UNITED FRONT
                              (CUF- Chama Cha Wananchi)
 

Office of the Secretary General
Party Headquarters,  P.O.  Box 3637, Zanzibar, Tanzania
E-mail:cufhabari.co.uk   Homepage: www.cuftz.org


Our Ref:      CUF/HQ/ONKM/U/003/2012/13                                     Date:                     29/05/2012

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Umma unashuhudia hali tete ya machafuko ambayo hayakutarajiwa yakiibukia tena Zanzibar, wakati ambapo Nchi ilishaanza kunawiri matunda ya utulivu na maridhiano, chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Pamoja na sababu au visingizio mbali mbali vilivyotajwa kuwa chanzo cha hali hiyo, zikiwamo za hamasa za wananchi, chuki binafsi, ukosefu wa hikma, matumizi ya nguvu za dola, na hata uchochezi wa makusudi wa wale wanaoonekana kutopendelea Maridhiano ya Kisiasa ya Zanzibar.

Kwa thamani yoyote hakuna asiyeweza kubaini umuhimu wa hali ya amani na utulivu, na madhara ya kukosekana kwake, hasa katika Visiwa hivi vya Unguja na Pemba ambavyo vimewahi kuelemezewa athari kubwa ya machafuko kwa muda mrefu.

Chama cha Wananchi,CUF, kama sehemu muhimu ya Umma wa Watanzania, hakiwezi kukaa kimya kutokana na mwelekeo mzima wa hali tete ya amani katika nchi, ingawa ni dhahiri wapo baadhi ya watu wasioitakia mema Zanzibar wakibainika kufurahia mazingira hayo, kwa maslahi binafsi, na pia kutoa kauli za kutatanisha za kisiasa.

Chama cha CUF, kinatoa wito kwa wananchi wote kuwa watulivu, wavumilivu, na kuitumia fursa ya kutoa mawazo yao bila ya jazba, pamoja na kutowanyima wengine nafasi ya kuwasilisha mitazamo yao.

Vitendo vya watu wachache kuchoma makanisa na kuharibu mali za watu ni vya uvunjifu wa sheria na kinyume na Utamaduni wa Kizanzibari; uchunguzi wa kina ufanyike na waliohusika wachukuliwe hatua za kisheria, bila uonevu wala upendeleo.

Tahadhari iwepo ya kuepuka matumizi ya mabavu yanayoweza kuleta hamasa kwa wananchi, hatimaye ikachochea vitendo vya hujuma dhidi ya watu na mali zao, na pia kuepuka tabia isiyokuwa ya haki, ya kuwabambikizia kesi wananchi.

Ni lazima kwa wakati huu, na haraka iwezekanavyo, Serikali ikazungumza na Masheikh, bila ya kuona muhali, na kwa uwazi kabisa, ili kutafuta suluhu ya kudumu, kwa faida ya Nchi na Taifa kwa Ujumla.

HAKI SAWA KWA WOTE


…………………………………….
Salim  A Bimani
Mkurugenzi wa Haki za Binaadamu, Habari na
Uenezi na Mahusiano na Umma

No comments: