Tangazo

February 12, 2015

JAMII YATAKIWA KUWASAIDIA WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUM - MAMA SALMA

Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete (pichani), ameitaka jamii kutumia sauti zao  kuwasemea watoto wenye mahitaji maalum kwani watoto hao wanakabiliwa na changamoto  mbalimbali na hawana mtu wa kumwambia matatizo yao.

Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alitoa rai hiyo jana alipotembelea kitengo cha wanafunzi wenye mahitaji maalum kilichopo shule ya Msingi Mpilipili wilaya ya Lindi mjini.

Alisema watoto wenye mahitaji maalum wanakabiliwa na changamoto nyingi ukilinganisha na watoto wengine  pia matatizo yao hayafanani hivyo basi ni jukumu la kila mtu katika jamii kuwasaidia watoto hao ili waweze kuishi kama watoto wengine. 

“Katika kitengo hiki kuna watoto wenye tatizo la usonji (Autism) na wasiosikia (viziwi), kila mtoto anahitaji lake na  pale anapokabiliwa na tatizo anatakiwa kusaidiwa kwa haraka  ili asijisikie kunyanyapaliwa. Nawapongeza walimu mnaowafundisha watoto hawa kwani kazi hii ni ngumu na inahitaji moyo wa ziada”, alisema Mama Kikwete.

Akisoma taarifa ya kitengo cha wanafunzi wenye mahitaji maalum mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mpilipili Fadhili Mtitima alisema kitengo hicho kilianzishwa mwaka 1993 kikiwa na wanafunzi watano na hivi sasa kuna wanafunzi 20 wenye tatizo la usonji 16 kati yao wavulana ni 16 na wasichana wawili na wasiosikia (viziwi) wawili msichana mmoja na mvulana mmoja.

Mwalimu Mtitima alisema njia zinazotumika kuwapata wanafunzi hao ni wanafunzi wa kawaida kutoa taarifa ya uwepo wa watoto wenye mahitaji maalum katika mitaa yao kwa walimu, wazazi ambao wamehamasika huwaleta watoto kujiunga na shule, kutoa hamasa na matangazo kwa jamii katika maadhimisho ya wiki ya elimu kwa wote na kupitia sensa ya watoto inayofanyika  kila mwaka.

“Changamoto zinazotukabili ni watoto wengi wanaoishi mbali na kitengo wanakosa fursa ya kupata elimu kutokana na umbali uliopo, baadhi ya wazazi wa watoto wenye ulemavu hawawaandikishi watoto wao wakiwa na imani kuwa watoto hawa hawafundishiki, idadi ya walimu haitoshelezi kwani kuna walimu wawili kati ya wanne wanaohitajika kufundisha watoto wenye tatizo la usonji.

“Kitengo hakina mwalimu mtaalamu wa elimu ya walemavu wasiosikia na walimu kutojitokeza kujiendeleza katika mafunzo ya kufundisha wanafunzi wenye mahitaji maalum”, alisema Mwalimu Mtitima.

Akiwa shuleni hapo Mama Kikwete aliwaita na kuwasalimia wanafunzi wa kawaida na kuwahimiza kusoma kwa bidii, kufuata sheria za shule na kuwatii walimu wao kwa kufanya hivyo watafanya vizuri katika masomo yao na kufika hadi elimu ya Chuo kikuu.

“Licha ya kusoma kwa bidii na kuhudhuria darasani mwanafunzi bora anatakiwa kuwahi shuleni na kufanya kazi za shule ikiwa ni pamoja na kusafisha eneo lake”, alisisitiza.

No comments: