Tangazo

September 25, 2015

Nkone, Lissu, Mwangila waahidi makubwa Tamasha la Amani Dar

 Mwenyekiti wa maandalizi ya Tamasha la Kuombea Amani katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, Alex Msama akifafanua jambo kuhusu maandalizi ya tamasha hilo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni mwimbaji wa nyimbo za injili, Christopher Mwahangila na Upendo Nkone. (Picha na Francis Dande)
 Mwimbaji wa nyimbo za injili, John Lissu akiimba kwa hisia moja ya nyimbo zake wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuhusu maandalizi ya Tamasha la kuombea Amani Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, tamasha hilo limeandaliwa na Kampuni ya Msama Promotions na litakafanyika Oktoba 4 kwenye Uwanja wa Taifa. Kushoto ni mwimbaji Christopher Mwahangila na Upendo Nkone.
Mwimbaji wa nyimbo za injili, Jesca Honore 'BM' akiimba wimbo wa 'Napokea' Jesca ni mmoja wa waimbaji watakaopamba tamasha la Amani la kuombea Uchaguzi Mkuu na Taifa.


NA MWANDISHI WETU

WAIMBAJI  mahiri wa nyimbo za injili nchini waliotajwa kushiriki Tamasha la Uchaguzi Mkuu litakalofanyika Oktoba 4, katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, wameelezea walivyojipanga kufanikisha malengo ya tukio hilo la kihistoria.

Wakizungumzia Tamasha hilo kwa nyakati tofauti katika mkutano wa utambulisho wao, baadhi ya waimbaji waliothibitishwa, wameelezea kufurahia kuwa miongoni mwa waimbaji watakaotumbuiza maelfu katika tamasha hilo la kuombea amani na utulivu Uchaguzi Mkuu.

Kwa upande wake Upendo Nkone, alisema ni faraja kwake kuwa miongoni mwao waimbaji katika tukio hilo la kumsihi Mungu ajalie hali ya amani na utulivu wakati na baada ya uchaguzi mkuu kwani amani ndio msingi wa mafanikio ya kila kitu.

“Nafarijika kuwemo katika orodha ya waimbaji katika Tamasha hilo. Watanzania tukumbuke taifa linahitaji maombi kwani linapita katika kipindi kigumu ambacho bila msaada wa Mungu, ni mtihani mgumu ambao katika nchi nyingi tu, umekuwa chanzo cha mifarakano,” alisema Upendo.

Naye Christopher Mwangila, mbali ya kushukuru kupata nafasi hiyo, pia amewasihi wapendwa katika Kristio Yesu, wapenzi na mashabiki wa muziki wa injili kujitokeza kwa wingi siku hiyo ya kupaza sauti kwa Mungu autangulie uchaguzi huo uwe wa amani.

Kauli hiyo iliungwa mkono na mwimbaji mwingine, John Lissu ambaye pamoja na shukrani kupata nafasi ya kushiriki, pia ametumia fursa hiyo kuwasihi wapenzi na mashabiki wa muziki wa njili na wote wenye upendo kwa nchi yao kujitokeza siku hiyo.

Naye Matha Mwaipaja, alisema anamshukuru Mungu kupata fursa na kumjalia kipaji cha uimbaji, hivyo ana kila sababu kushiriki tukio muhimu kama hilo la kuombea amani ya nchi kwa kuzingatia kuwa, viongozi hutoka kwa Mungu.

Mwimbaji mwingine aliyetoa neno kuelekea Tamasha hilo, ni Jesca Boniface Magupa ‘BM’ akisema amejiandaa vizuri kuipamba siku hiyo akishirikiana na wengine mahiri wa ndani na nje ya nchi akiamini sauti za kumsihi Mungu uchaguzi uwe wa amani, hazitapotea bure.

No comments: