Jovina Bujulu- MAELEZO.
Dar es Salaam.
Wavuvi waishio ukanda wa maeneo ya Pwani ya Bahari ya Hindi upande wa Tanzania Bara na Zanzibar wanatarajia kunufaika na elimu ya ukuzaji viumbe kwenye maji na teknolojia sahihi ya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi kupitia mradi wa Udhibiti wa Uvuvi na Maendeleo Shirikishi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFISH).
Hayo yamesemwa jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara ya Maendeleo ya Uvuvi, Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi Bi. Fatma Sobo alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa mradi wa Udhibiti Uvuvi na Maendeleo Shirikishi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi, ulioanza kutekelezwa mwezi Juni mwaka huu.
Amesema lengo la mradi huo ni kuwasaidia wavuvi wadogo wa ukanda huo ili waweze kunufaika na shughuli hiyo na kuwa na uvuvi endelevu wenye kuongeza faida kiuchumi, kijamii na kimazingira.
‘Lengo la mradi huu ni kuhakikisha kuwa wavuvi wa ukanda wa Pwani wanakuwa na uvuvi endelevu na wananufaika na rasilimali za bahari kwa kuimarisha uwezo wa Taasisi za Kikanda na Serikali” Amesema.
Ameeleza kuwa katika kufuatilia utekelezaji wa mradi huo , Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi,imeanzisha mpango wa uongozi na usimamizi wa uvuvi ambapo wavuvi wanapatiwa elimu kuhusu aina za samaki, aina ya nyavu za kuvulia, muda wa kuvua, mauzo na uhifadhi wa samaki.
Ameongeza kuwa mradi huo utaimarisha mfumo wa taarifa za uvuvi kama vile mavuno, nguvu ya uvuvi inayotumika , mauzo ya ndani na nje nchi yatokanayo na shughuli hizo.
Bi. Fatma aliongeza kuwa kipaumbele cha mradi huo kimewekwa katika uvuvi wa samaki aina ya pelagiska, Jodari, Kamba miti, samaki mwamba, pweza na ukuzaji viumbe kwenye maji bahari ambapo eneo la majaribio litakuwa katika wilaya za Mkinga, Pangani, Tanga, Bagamoyo mjini na Lindi Vijijini.
Aidha, amesema mradi huu utatekelezwa kwa miaka 6, kuanzia 2015 hadi 2021 na umefadhiliwa na Mfuko wa Mazingira Duniani na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo kwa jumla ya Dola za Kimarekani milioni 36,000 ambapo utazihusisha wilaya 16 kutoka ukanda wa bahari ya Hindi, mkoa wa Tanga hadi Mtwara.
Ameongeza kuwa mradi huo ukizishirikisha Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi (Tanzania Bara), Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Zanzibar) na Mamlaka ya Kusimamia Bahari Kuu utakomesha uvuvi haramu wa kutumia Mabomu.
Taasisi zitakazotelekeza mradi huo ni Wakala wa Mafunzo ya Elimu ya Uvuvi, Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Kitengo cha Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu, Vikundi vya Ujasiriamali na Jamii za watu wa Pwani.
No comments:
Post a Comment