Tangazo

February 24, 2016

BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU: UTARATIBU WA KUPOKEA NA KUSHUGHULIKIA MALALAMIKO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU

1.0        UTANGULIZI
Kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wadau wakiwemo wanafunzi wa elimu ya juu kuhusu kuchelewa au kutokushughulikiwa kwa malalamiko yao yanayohusu mikopo ipasavyo katika ngazi za vyuo na katika ofisi za Bodi. Kufuatia malalamiko hayo, Bodi imeboresha utaratibu wa kushughulikia maswali au malalamiko katika ngazi zote ili kuongeza ufanisi.

Hata hivyo, kabla ya kueleza kuhusu utaratibu huu ulioboreshwa, tungependa kueleza sifa na vigezo vinavyotoa  ustahili kwa Wanafunzi kupata mkopo.

2.0        SIFA ZA MWOMBAJI
Utoaji mikopo unaongozwa na Sheria Na. 9 ya 2004 ya Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (kama ilivyorekebishwa) Na. 9 ya 2004 hususani vifungu vyake vya 16 na 17.  Pamoja na mambo mengine, sheria hii inaitaka Bodi kutoa msaada wa kifedha kwa njia ya mkopo kwa mwanafunzi mwenye sifa ambaye ameomba kupewa mkopo huo umwezeshe kugharamia mahitaji yake yote au baadhi katika masomo yake ya elimu ya juu. Hivyo basi, kila mwaka Serikali kupitia Bodi, huandaa vigezo na sifa zitakazotumika katika kutoa mikopo kwa mwaka husika kwa kuzingatia matakwa ya sheria. Kimsingi vigezo ambavyo vimebainishwa na sheria ni:
a)            Awe mtanzania;
b)           Awe ameomba mkopo kupitia mtandao wa Bodi (Online Loan and Management System (OLAMS));
c)            Awe amechaguliwa kujiunga na masomo katika chuo chenye ithibati kinachotambuliwa na kusajiliwa na TCU au NACTE kama mwanafunzi “full time”;
d)           Awe ni mwanafunzi anayeendelea na masomo ambaye amefaulu mitihani inayomwezesha kuendelea na mwaka unaofuata wa masomo;
e)            Asiwe ni mnufaika wa mkopo au ruzuku kutoka  taasisi nyingine au watu wengine;
f)             Aliyemaliza kidato cha sita, mafunzo ya ufundi au ualimu .....
g)           Kwa kuzingatia idadi ya waombaji na uwezo wa Bodi ya kibajeti, mikopo hutolewa kwanza kwa:

Sheria iliyoiunda Bodi imeipa mamlaka ya kutengeneza vigezo vya nyongeza vinavyoboresha zoezi la utoaji wa mikopo ambapo kila mwaka Bodi huandaa na kutangaza Mwongozo wa Ukopeshaji wa mwaka unaofuatia ambao hutangazwa kabla ya msimu wa wanafunzi kuomba mikopo kuanza. Mwongozo uliotangazwa kuongeza uchambuaji maombi ya mikopo kwa ajili ya mwaka wa masomo 2015/16, ulitoa sifa zinazowapa waombaji ustahili kama ifuatavyo:

·         Wanafunzi wanaosoma programu za kipaumbele kwa taifa ambao hupata asilimia 100. Programu hizo ni Sayansi za Tiba, Ualimu wa Masomo ya Sayansi na Hisabati, Uhandisi wa Umwagiliaji na Uhandisi wa Gesi na mafuta;
·         Yatima;
·         Wenye ulemavu
·         Wanafunzi wanaosoma programu nyingine hupangiwa mikopo kwa kuzingatia uchambuzi unafanywa kwa kutumia king’amuzi uwezo (Means Testing).

3.0     UTANGAZAJI WA WAOMBAJI WALIOFANIKIWA KUPANGIWA MIKOPO NA UANDAAJI WA MALIPO

3.1     UTANGAZAJI WA MAJINA YA WAOMBAJI WALIOPANGIWA MIKOPO
Baada ya uchambuzi wa taarifa zote za waombaji kwa kuzingatia mwongozo uliotolewa kufanyika taarifa za, waombaji waliofanikiwa. Kupangiwa mikopo (loan allocation) hutumwa vyuoni, hupokelewa na Menejimenti za vyuo na kufikishwa kwenye madawati ya mikopo (Loan Officers) ya vyuo husika huitangaza orodha hiyo kwa Wanafunzi halali wa vyuo husika kwa njia mbalimbali kama kubandika kwenye ubao wa matangazo (notice board) na kupeleka ofisi za Serikali za Wanafunzi.. Aidha, orodha hiyo huwekwa kwenye mtandao wa Bodi (OLAMS) ili wanafunzi waweze kuiona.

3.2     UANDAAJI WA MALIPO
Malipo hufanywa kwa waombaji waliofanikiwa kupata Mikopo malipo yaoo hupelekwa  kwenye chuo ili chuo kiwalipe baada ya kuwatambua vizuri kuwa ni Wanafunzi halali wa chuo hicho kwa kuangalia vitambulisho vyao. ambapo Bodi ya Mikopo hufanya malipo kwa njia ya ‘cheque’ kwa kukilipa chuo husika ambacho huwajibika kuwalipa wanafunzi ndani ya siku saba (07) tangu kipokee fedha kutoka Bodi ya Mikopo.

3.3     MAJUKUMU YA ‘LOAN OFFICER’
Mnamo mwaka 2011 serikali iliunda Tume ambayo ilitazama namna ya kuboresha mfumo mzima wa Utoaji wa Mikopo. Pamoja na mambo mengine, tume ilipendekeza kuanzishwa kwa madawati ya Mikopo kwenye kila chuo. Watumishi katika madawati hayo walitakiwa kuitwa Maafisa Mikopo.

Majukumu yao yanatakiwa kuwa ni:

                   a.            Kutunza kumbukumbu ya wanafunzi wote wanaopata mikopo kutoka Bodi ya Mikopo;
                  b.            Kuhakiki uwepo wa wanafunzi waliopangiwa mikopo katika chuo chake kabla wanafunzi hao hawajapokea malipo;
                   c.            Kuanzisha na kutunza kumbukumbu ya wanafunzi wanufaika wa mikopo na wanaoacha masomo kwa sababu mbalimbali (Kifo, uhamisho, kuahirisha n.k). Aidha, ‘Loan Officer’ huyu, anapaswa kuandaa taarifa hizi na kuziwasilisha Bodi ya Mikopo kila mwisho wa robo mwaka wa masomo;
                  d.             Kuratibu uandaaji wa matokeo ya mitihani ya wanafunzi na kuyawasilisha Bodi ya Mikopo ndani ya siku 30 kabla ya kuanza kwa mwaka mpya wa masomo na kwa matokeo ya marudio 9Supplimetary Examinations), angalau siku 30 baada ya chuo kufunguliwa;
                   e.            Kuratibu uandaaji na uwasilishaji wa Ankara na Madai (Invoices and Claims) kwa wanafunzi wenye mikopo kwa ajili ya malipo;
                   f.            Kuhakikisha wanufaika halali wanathibitisha upokeaji mikopo kwa kutia saini kwenye karatasi za malipo na kuhakikisha kwa wale ambao hawajasaini, fedha zao zinarudishwa Bodi ya Mikopo; na
                  g.            Kupokea na kuyafanyia kazi maswali na malalamiko kutoka kwa wanafunzi yanayohusu utoaji wa mikopo na kuyatolea ufafanuzi. Ikiwa yanahitaji ufafanuzi wa ziada, kuwasilisha kwa Bodi ya Mikopo kwa hatua zaidi

4.0     UTARATIBU ULIOBORESHWA WA KUSHUGHULIKIA MALAMAMIKO YA WANAFUNZI

Kama tulivyosema hapo awali, ili kuboresha ufanisi wa utoaji mikopo, mwezi Agosti mwaka 2011, Serikali kupitia iliyokuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ilivielekeza vyuo vyote za elimu ya juu kuanzisha madawati yatakayoratibu na kusimamia masuala ya mikopo na ruzuku kwa wanafunzi wa vyuo husika. Agizo hili limetekelezwa vizuri kiasi na hivi sasa kila chuo cha elimu ya juu kina Afisa anayesimamia masuala ya mikopo na ruzuku kwa wanafunzi wao wanaokopesheka.

Hivyo, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) inapenda kuwakumbusha wadau wake wote, wakiwemo wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu, kuhusu utaratibu wa kuwasilisha malalamiko au maswali yanayohusu mikopo na ruzuku kwa wanafunzi wa elimu ya juu kama ifuatavyo hapa chini.

     i.        KWANZA, mwanafunzi yeyote anayefadhiliwa na Serikali kupitia Bodi ya Mikopo mwenye swali au malalamiko anatakiwa kuwasilisha suala lake kwa Afisa mhusika anayesimamia Dawati la Mikopo/Ruzuku (Loan Officer) aliyepo chuoni kwake. Hao ‘Loan Officers’ hivi sasa wana uzoefu wa masuala ya mikopo na ruzuku zitolewazo na Bodi;

  ii.        PILI, baada ya swali au malalamiko kupokelewa, ‘Loan Officer’ huyo anapaswa kuyapokea na kuyatafutia suluhisho malalamiko hayo na kumjibu mwanafunzi ndani ya siku mbili (02), kama siyo siku hiyo hiyo, tangu apokee swali au malalamiko hayo;

 iii.        TATU, ikiwa siku mbili (02) zitapita bila mwanafunzi kupata jibu, mwanafunzi awasilishe malalamiko yake kwa mamlaka ya juu ya huyo ‘Loan Officer’ ambaye naye anapaswa kutoa majibu au kuchukua  hatua ndani ya siku mbili (02), kama siyo siku hiyo hiyo;

 iv.        NNE, ikiwa kiongozi wa chuo husika cha elimu ya juu atakuwa hana jibu la swali au malalamiko yaliyowasilishwa kwake, anapaswa kuwasilisha suala hilo Ofisi ya Bodi ya Mikopo ya Kanda iliyo karibu na chuo chake. Ofisi ya Kanda itawajibika kutoa jibu siku hiyo hiyo ya kupokea maswali au malalamiko hayo au kuwasilisha suala hilo Makao Makuu ya Bodi ya Mikopo kama hana maelezo yake;

  v.        TANO, kwa vyuo vya elimu ya juu ambavyo havipo karibu na ofisi za Kanda za Bodi ya Mikopo, uongozi wa chuo husika unapaswa kuwasiliana na makao Makuu ya Bodi ya Mikopo moja kwa moja kwa njia ya barua pepe ifuatayo: malalamiko@heslb.go.tz ;

 vi.        SITA, baada ya kupokea malalamiko hayo, Bodi ya Mikopo Makao Makuu  itatoa majibu kwa malalamiko/maswali yaliyowasilishwa siku hiyo hiyo au ndani ya siku mbili (02) tangu kupokelewa kwa malalamiko au maswali hayo; na

vii.        SABA, mara tu baada ya kupokea majibu ya swali au malalamiko yaliyowasilishwa kutoka Bodi ya Mikopo, uongozi wa chuo cha elimu ya juu utayafikisha majibu hayo kwa mwanafunzi husika siku hiyo hiyo kupitia kwa ‘Loan Officer’ wa chuo husika.

3.0        HITIMISHO
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inasisitiza kuwa ni muhimu kwa wanafunzi na wadau wote kuzingatia utaratibu huu ili kuongeza ufanisi katika kushughulikia malalamiko ya wanafunzi.


IMETOLEWA NA:
BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU

FEBRUARI, 2016

No comments: