Tangazo

August 1, 2011

Askofu Mkombo awashangaa wanaolibeza Jeshi la Polisi

Askofu Mkuu wa Kanisa la House of Prayer Shield of Faith Christian Fellowship, Mulilege Mkombo, akiombea watu baada ya kumaliza kuhubiri katika Mkutano wa Injili uliofanyika katika Uwanja wa CCM ulioko Rwanda-Nzonve mjini Mbeya juzi. Mkutano huo ulikuwa na lengo la kuombea amani na utulivu katika mkoa wa Mbeya. (Picha kwa hisani ya huduma ya Revelation Tanzania)

Na Jackson Malugu, Mbeya

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la House of Prayer Shield of faith Christian Fellowship, Mulilege Mkombo, amesema anasikitishwa na baadhi ya wananchi, wakiwemo wanasiasa, wanaobeza utendaji wa Jeshi la Polisi kwani amani iliyopo nchini ni matokeo ya uwajibikaji wa jeshi hilo.


Akihubiri katika Mkutano wa Injili uliofanyika katika Uwanja wa CCM, Rwanda-Nzonve, mjini hapa juzi Jumapili, askofu huyo alisema kuwa, matukio machache yanayojitokeza kama dosari katika utendaji wa jeshi hilo haupaswi kutumika kulibeza.


“Mimi ninawashangaa sana wanaolibeza jeshi letu (la polisi). Hawa wenzetu pamoja na mazingira magumu ya kazi yao bado wanahakikisha wananchi wako salama. Watu wanafanya shughuli zao huku wakijua wanalindwa na askari. Hali kama hii haipo katika nchi nyingi tu. Kwa kweli tunapaswa kuwapongeza badala ya kuwabeza,” alisema Askofu Mkombo.


Alisema, mapungufu yanayojitokeza kwa jeshi hilo katika baadhi ya maeneo ni changamoto ambazo serikali na jamii kwa ujumla inapaswa kuzishughulikia kama ambavyo imekuwa ikishughulikia maeneo mengine.


“Tunayo matatizo katika utendaji wa sekta mbalimbali. Tunalalamikia mahakimu katika mahakama, tunalalamikia walimu katika baadhi ya maeneo, tunalalamikia watendaji katika hospitali zetu, tumeanza kulalamikia hata Bunge. Wakati mwingine ni matatizo ya kimaadili ambayo yamegubika jamii yote, na hatupaswi kubeza utendaji wa jumla,” alisema Askofu Mkombo alipotakiwa na mwandishi wa habari hizi kufafanua mahubiri yake.


Askofu huyo pia alikemea kile alichoita kitendo cha baadhi ya watu kulaani viongozi wa serikali kwa hoja kuwa serikali haijafanya lolote kwa wananchi. Alisema, viongozi wa serikali wamewekwa na Mungu hivyo sio jambo la hekima kuwalaani.


“Eti tunawabeza viongozi wetu wa serikali. Tunasema serikali haijafanya lolote. Lakini ngoja niwaambie ukweli, serikali yetu imefanya mengi sana kwa wananchi wake. Serikali imetoa fursa nyingi za mikopo, watoto wetu wanasoma kwa mikopo tofauti na nchi nyingi tu, kama ni mapungufu ni mambo ya kawaida ambayo yanaweza kurekebishwa,” alisema na kuongeza:


“Tatizo ninaloliona ni baadhi ya wananchi kupenda kukaa vijiweni bila kufikiria shughuli za kimaendeleo kisha wanailalamikia serikali. Wananchi wamepewa fursa nyingi za kujitafutia kipato, kama ni mapungufu ni changamoto za kawaida ambazo zinapaswa kushughulikiwa na serikali kwa kushirikiana na wananchi wenyewe.”


Akiuzungumzia mkoa wa Mbeya, Askofu Mkombo aliwataka wakazi wa mkoa huo kuachana na ubinafsi pamoja na siasa za chuki na badala yake wafikirie zaidi maendeleo yao. Alisema, ubinafsi na tamaa miongoni mwa wakazi wake umechangia kukithiri kwa vitendo vya mauaji na ushirikina, hivyo kuathiri maendeleo ya mkoa huo.


Mkutano huo uliokuwa na lengo la kuombea amani na utulivu katika mkoa wa Mbeya ulifanyika kwa siku sita mfululizo kuanzia Julai 26 hadi 31, mwaka huu.





No comments: