Katibu Mkuu TASWA, Amir Mhando |
CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kinapenda kutangaza kuwa kampuni ya usafirishaji ya Al Saedy High Classic Bus Services imejitokeza kudhamini mafunzo kwa ajili ya waandishi wa habari za michezo yatakayofanyika mkoani Morogoro Oktoba 1 na 2 mwaka huu.
Al Saedy ambayo inasafirisha abiria kati ya Dar es Salaam-Morogoro, Dar es Salaam - Mpwapwa, Dar es Salaam-Kahama, Dar es Salaam-Mbeya, Dar es Salaam-Kilosa, Dar es Salaam-Ifakara, Dar-Ulanga na Dar –Malinyi, imekubali kuwasafirisha washiriki kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na kurudi Dar es Salaam.
Washiriki hao wataondoka Dar es Salaam kuelekea Morogoro Ijumaa mchana ya Septemba, 30, 2011 na kurejea Dar es Salaam baada ya kufungwa mafunzo hayo alasiri ya Oktoba 2, 2011.
TASWA inaishukuru kampuni hiyo kwa hatua hiyo kwani imeonesha jinsi gani ilivyo karibu na wana habari, ambapo bado chama kinaomba wengine wajitokeze kusaidia kudhamini mafunzo hayo.
Tayari Kampuni ya simu za mkononi Vodacom imetangaza kudhamini mafunzo hayo kwa sh. Milioni saba, lakini kutokana na idadi kubwa ya washiriki nguvu zaidi zinahitajika.
WASHIRIKI WA MAFUNZO
Kamati ya Utendaji ya TASWA ilikutana Dar es Salaam Jumamosi, Septemba 17 na kuteua majina 40 ya washiriki wa mafunzo hayo kwa mikoa ya Pwani, Dar es Salaam na Morogoro.
Uteuzi umezingatia zaidi washiriki ambao hawakuwahi kushiriki mafunzo yaliyopita, pia uwiano wa vyombo vya habari.Majina yatatangazwa Jumatano baada ya washiriki wote kujulishwa kwa barua kwanza na kuthibitisha.
Pia kamati imekubaliana mafunzo ya Arusha yafanyike Novemba 11,12 na 13 yakihusisha washiriki 50 kutoka mikoa ya Kilimanjaro, Tanga, Arusha, Manyara na Dar es Salaam ambayo itakuwa na idadi kubwa zaidi ya washiriki kutokana na kuwepo kwa vyombo vingi vya habari na wanachama wengi wa TASWA.
Pia mafunzo ya Arusha yahusishe zaidi waandishi wa habari za michezo ambao ni wazoefu wa taaluma na uteuzi wake usiangaliwe ambao wamewahi kushiriki.
Mafunzo hayo yatafuatiwa na yale ya wahariri wa habari za michezo, ambayo tayari sekretarieti ya TASWA imeagizwa kufanyia kazi kwa kuangalia mkoa ambao yatafanyika na bajeti yake, huku msisitizo ukiwa isiwe zaidi ya Desemba 15, 2011 na mikoa iwe Kilimanjaro, Tanga au Pwani.
Kamati imekubaliana kuwa mafunzo ya Morogoro yahusishe masuala ya maadili ya uandishi wa habari,, masuala ya sheria za mambo ya habari na sheria za michezo mbalimbali pia washiriki wataelimishwa namna ya kuripoti habari za michezo ya mpira wa wavu, netiboli na ngumi.
Tayari wakufunzi wameshapatikana, ambao ni walimu wa mambo ya habari, wahariri wazoefu, wanasheria na wakufunzi wa michezo mbalimbali nchini.
Imetolewa na: .
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
18/09/2011
No comments:
Post a Comment