Tangazo

December 29, 2011

Kibanda ajiengua Kamati ya Kutafuta Vazi la Taifa

Mhariri Mtendaji Free Media Ltd na Mwenyekiti Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda.
UTANGULIZI

Itakumbukwa kwamba Desemba 15 mwaka huu, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi aliniteua kuwa mjumbe katika Kamati ya Kitaifa ya Kukamilisha Mchakato wa Kupata Vazi la Taifa.

Siku chache baada ya uteuzi huo, nilipokea wito wa kuitwa na kuhojiwa na Jeshi la Polisi kutokana na makala ambayo ilichapishwa katika gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Novemba 30 mwaka 2011.

Kufuatia mahojiano hayo, Desemba 21 nilifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambako polisi na wanasheria wa serikali walinifungulia mashtaka ya kuwachochea askari kutoitii Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Nilipata dhamana katika kesi hiyo ambayo imeahirishwa hadi Januari 19, 2012 itakapotajwa tena.

MSIMAMO NA UAMUZI WANGU

Baada ya kutafakari kwa kina kuhusu uteuzi wa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo sambamba na uamuzi wa serikali kunihoji na kunifungulia mashitaka, busara yangu binafsi na kwa kuzingatia ushauri nilioupata kutoka kwa wahariri wenzangu, nimefikia uamuzi wa kujitoa katika Kamati ya Kutafuta Vazi la Taifa.

Nimelazimika kufikia uamuzi huo kwa sababu zifuatazo:

1. Mosi, uamuzi wa serikali kupitia Jeshi la Polisi na Waendesha Mashitaka kunifungulia kesi ya kuchochea uasi inanifanya niamini kwa dhati kwamba, haina imani nami binafsi na ina nia ya dhati ya kuhakikisha ninaadhibiwa na hivyo kukinzana na imani ambayo Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ameionyesha kwangu kupitia uteuzi wake.

2. Pili, nimelazimika kufikia uamuzi huo wa kujitoa katika kamati hiyo baada ya kujiridhisha pasipo shaka kwamba mchakato mzima uliohusisha sakata langu kama Mhariri Mtendaji kuhojiwa na kufunguliwa mashitaka na polisi na hatimaye kufikishwa kwangu mahakamani usingeweza kufikiwa pasipo kuishirikisha Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ambayo inaongozwa na Waziri Nchimbi.

3. Tatu, kwa kuyatambua hayo nimeona itakuwa ni uamuzi wenye hekima kujitoa katika kamati hiyo kwa kuzingatia uhalisia kwamba nitashindwa kutimiza wajibu wangu ipasavyo nikiwa mjumbe katika kamati hiyo, sababu kubwa ikiwa ni kuwapo kwa hali ya kutoaminiana na kutiliana shaka kati ya wizara na waziri Nchimbi kwa upande mmoja na mimi mteule katika kamati huyo kwa upande mwingine.

4. Mwisho, wakati nikichukua uamuzi huo mgumu, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru sana Waziri Nchimbi kwa kuonyesha imani nami hata kuniteua kuwa miongoni mwa wajumbe wanane wanaounda Kamati ya Kitaifa ya Vazi la Taifa.

Imetolewa na:
Absalom Kibanda
Mhariri Mtendaji Free Media Ltd na Mwenyekiti Jukwaa la Wahariri

No comments: