Tangazo

March 7, 2012

ICTR YAMWACHIA HURU MUVUNYI KABLA YA MUDA WA ADHABU KUISHA

Tharcisse Muvunyi
Na Shirika la Habari la Hirondelle

Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) Jumanne ilimwachia huru mmoja wa wafungwa wake, Luteni Kanali Tharcisse Muvunyi kabla ya kumalizika muda wake wa adhabu wa miaka 15 jela baada ya kutumikia zaidi ya miaka 12 ya adhabu hiyo.

‘’Kuachiwa huru mapema sasa ni muafaka kwa sababu zaidi ya robo tatu ya adhabu dhidi ya Muvunyi imeshatumikiwa,’’ inaeleza sehemu ya taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari ikimnukuu Rais wa ICTR, Jaji Vagn  Joensen.

Taarifa hiyo ilieleza kwamba Aprili 18, 2011, Muvunyi alimwandikia Rais wa ICTR, akimwomba aachiwe huru mapema kabla ya muda wa adhabu aliyopewa kwa vile alikuwa ameshatumikia theluthi mbili ya adhabu hiyo.

Katika mashitaka yaliyosikilizwa awali, Muvunyi alihukumiwa kifungo cha miaka 25 jela baada ya kutiwa hatiani kwa mauaji ya kimbari, uchohezi wa kufanya mauaji hayo na vitendo vingine vya uhalifu dhidi ya binadamu.

Lakini Mahakama ya Rufaa alibadilisha hukumu iliyotolewa na mahakama ya awali Agosti 29, 2008 na kuamuru kusikilizwa upya kwa shauri hilo kwa shitaka moja tu la kuchochea mauaji ya kimbari na kuyatuplilia mbali mashitaka mengine kwa maelezo kuwa yamekosewa katika hati ya mashitaka.

Shitaka hilo moja la uchochezi wa mauaji ya kimbari linahusiana na hotuba aliyotoa Muvunyi katika Kituo cha Biashara cha Gikore, mkoani Butare, Kusini mwa Rwanda, Mei, 1994.Anadaiwa kutumia misemo ya lugha ya Kinyarwanda kuwahamasisha Wahutu kuwaua Watutsi.

Mahakama baada ya kusikiliza kwa mara ya pili shauri hilo kufuatia amri ya Mahakama ya Rufaa, ilimtia hatiani Muvunyi na kumtwika adhabu ya kifungo cha miaka 15 jela huku muda aliokwishatumikia akiwa kizuizini tangu kutiwa mbaroni mwaka 2000 ukihesabiwa kwamba ni sehemu ya adhabu ambayo tayari ameitumikia.

Wafungwa wengine wawili wa ICTR wameshaachiwa huru kabla ya kumalizika kwa muda wao wa dhabu walizopewa. Nao ni aliyekuwa Mkuu wa Mamlaka ya Chai nchini Rwanda, Michel Bagaragaza aliyeachiwa huru Desemba 1, 2011 na Meya wa zamani Juvenal Rugambarara aliyeachiwa Februari 8, 2012.

Bagaragaza alitumikia adhabu yake nchini Sweden wakati Rugambarara alitumikia nchini Benin.Tofauti na wenzake hao wawili ambao walikiri kwa hiari mashitaka yaliyokuwa yanawakabili, Muvunyi alikana mashitaka dhidi yake.

Kwa mujibu wa Msemaji wa ICTR, Roland Amoussouga, Muvunyi aliachiwa huru kama ilivyoamriwa na kwamba alishawasili kwenye nyumba maalum ya ICTR wanayoishi kwa muda watu waliochiwa huru na wale waliomaliza muda wa kutumikia adhabu zao

No comments: